Ijumaa, 17 Aprili 2026

LINDI YAWASISITIZA WADAU KUIMARISHA USHIRIKIANO, KUBORESHA UTOAJI HAKI

Na. HILARI GDIYE NA WINIFRIDA KISAMO – Mahakama, Lindi

Wadau wa Sekta ya Haki mkoani Lindi wamehimizwa kuongeza na kuimarisha ushirikiano katika uendeshaji wa mashauri ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati mapema ipasavyo na kwa ufanisi.

Akizungumza katika kikao cha wadau kilichofanyika hivi karibuni, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Lindi Mhe. Sylester Kainda alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu miongoni mwa wadau wote wa Sekta ya haki ili kutotoa nafasi ya kuchelewesha mashauri yanapofunguliwa mahakamani.

Mhe. Kainda amesema kuwa, mafanikio ya Mahakama yanategemea mchango wa pamoja wa kila mdau. Alibainisha kuwa kikao hicho kililenga kuweka mkakati madhubuti wa namna bora ya kuendesha shughuli za Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Lindi kwa ufanisi, uwazi na kasi na kuhakikisha huduma za haki zinatolewa kwa wakati mapema ipasavyo na kwa viwango vinavyotarajiwa.

Aidha, Jaji Mfawidhi alieleza kuwa, Mahakama haiwezi kusimama peke yake bila ushirikiano wa wadau wake, akiwataka wadau wote kutambua nafasi zao katika kuhakikisha mchakato wa haki unakuwa thabiti na wenye matokeo chanya kwa jamii.

Vilevile, Mhe. Kainda alisisitiza umuhimu wa kumaliza mashauri kwa wakati ili kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi bila ucheleweshaji usio wa lazima, kwa mujibu wa takwimu Mkoa wa Lindi una mashauri machache, hali inayotoa fursa kwa Mahakama kuhakikisha kesi zote zinakamilika kabla ya mwezi Disemba, 2026.

“Kwa idadi ndogo ya mashauri yaliyopo ni matarajio yetu kwamba, Mahakama zetu zifike hatua ya kumaliza kesi zote kwa wakati na hata kuwa, katika nafasi ya kusubiri mashauri mapya,” alisema Jaji Kainda.

Jaji Mfawidhi huyo, alifafanua kuwa, mfumo wa kimahakama hupima ufanisi kwa kuzingatia muda unaotumika kusikiliza na kumaliza mashauri, hivyo Mahakama zinapaswa kuepuka uwepo wa kesi za muda mrefu zinazoleta mlundikano wa mashauri.

Akizungumzia suala la mashahidi, Mhe. Kainda alisema kuwa, matumizi ya teknolojia yamerahisisha usikilizwaji wa mashahidi kwa njia ya mtandao (remote hearing), hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya umbali na gharama.

Hata hivyo, alionya kuwa baadhi ya mashauri huathirika kutokana na mapungufu katika uendeshaji wake, akiwataka Mahakimu na wadau kuongeza umakini katika maandalizi na usikilizwaji wa mashauri ili kulinda haki za wahusika wote katika shauri husika. Pia alikemea vitendo vya rushwa na ucheleweshaji wa majalada ya kesi, akisisitiza kuwa maadili na uadilifu vinapaswa kupewa kipaumbele katika utoaji wa haki.

Katika jitihada za kurahisisha huduma kwa wananchi, Jaji Kainda alieleza kuwa, utambulisho wa wadhamini unaweza kuthibitishwa kwa kutumia Kitambulisho cha Taifa (NIDA) pekee, bila ulazima wa kuwasilisha barua za utambulisho kutoka kwa viongozi wa vijiji au Serikali za mitaa.

Kwa upande wa maboresho ya mifumo kiteknolojia, Mhe. Kainda alisema kuwa, Mahakama Kuu Lindi na Mahakama zake za chini zimeshanza kutumia mfumo wa kielektroni (paperless), hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kupunguza matumizi ya karatasi.

Jaji Mfawidhi huyo, ameyahimiza mabaraza ya ardhi kuhakikisha yanatoa nakala za hukumu kwa wakati ili kuwawezesha wananchi kupata haki zao bila ucheleweshaji usio wa lazima.

Wadau walikubaliana juu ya umuhimu wa ushirikiano, uwajibikaji na matumizi ya teknolojia katika kuimarisha utoaji wa haki, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa Mahakama katika utoaji wa haki kwa wananchi.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Lindi akiwasilisha Mada wakati wa Kikao na Wadau. Wengine ni Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Lindi Mhe. Elia Joseph Mrema (kushoto) na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Lindi Bi. Quip Godfrey Mbeyela (kulia)

Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Lindi Mhe. Elia Joseph Mrema akizungumza jambo wakati wa kikao hicho.


Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Lindi Bi. Quip Godfrey Mbeyela (aliyesimama) akizungumza jambo wakati wa kikao hicho.

Mdau wa Mahakama Kutoka Ofisi ya Huduma ya Uangalizi wa Jamii Bi. Wilhelmina Qambalo akitoa hoja wakati wa kikao hicho.

Wadau wakifuatilia kwa Makini Mada zilizokuwa zinawasilishwa wakati wa kikao.


Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Lindi Mhe. Sylivester Kainda (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa Mahakama.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama) 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni