Alhamisi, 9 Aprili 2026

JENGENI UTAMADUNI WA KUKUTANA MARA KWA MARA KAMA KATIBA INAVYOELEKEZA; JAJI KIONGOZI

Na. HABIBA MBARUKU- Mahakama, Dodoma

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani ambaye pia ni Mlezi wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Masjala Kuu, amewataka wanachama wa chama hicho kujenga utamaduni wa kukutana mara kwa mara ili kulinda uhai wa chama hicho.

Mhe. Dkt. Siyani ameyasema hayo wakati alipofungua mafunzo na michezo kwa Wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Masjala Kuu, leo tarehe 9 Aprili, 2026 katika ukumbi wa mikutano, Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Mhe. Dkt. Siyani amesema kuwa, upo umuhimu wa wanachama wa TMJA Tawi la Masjala Kuu kukutana mara kwa mara, kama ambavyo vyama katika Taasisi nyingine hufanya, hivyo ni muhimu kuhakikisha kwamba vikao vya Chama vinaandaliwa na wajumbe wanakutana kama ambavyo Katiba ya Chama inaelekeza huku akiwahimiza wanachama na wajumbe kuhudhuria vikao vya chama bila visingizio.

“Umuhimu wa kukutana mara kwa mara, uhai wa vyama hivi kama ilivyo kwa taasisi nyingine unategemea wajumbe wake kukutana, inategemea uwepo wa vikao, chama au taasisi yoyote ambayo haikutani uhai wake unakuwa mashakani, kwa hiyo tawi hili kama matawi mengine yote yanao wajibu wa kikatiba kwa mujibu wa Katiba yetu ya chama kukutana, ni muhimu kuhakikisha kwamba vikao hivi vinaandaliwa na watu wanakutana, ujengwe huo utamaduni na tusirudi tena kwenye historia ya kukaa muda mrefu bila kukutana ili kulinda uhai wa chama” amesema Mhe. Dkt. Siyani.

Aidha, Mhe. Dkt. Siyani ameongeza kuwa, kama ambavyo kila mmoja hulinda afya yake, ni muhimu kila mwanachama kuanza kuitazama afya ya akili na kuipa kipaumbele kwa sababu tatizo la afya ya akili linaweza kuathiri utendaji wa shughuli za kila mmoja na hasa zile za kiofisi, hivyo ni vyema kuanza kutazama mambo yanayoweza kupunguza msongo wa mawazo ili kutunza afya ya akili.

Akizungumza kuhusu umuhimu wa mafunzo yatakayotolewa, Mhe. Dkt. Siyani ameeleza kuwa, mafunzo hayo yatawasaidia kutambua ni shughuli gani wanaweza kufanya ili kujiongezea kipato bila kuathiri uwajibikaji wao kama Maofisa Mahakama, kupitia mada mbalimbali zitakazotolewa ikiwemo masuala ya uwekezaji salama na wenye tija na kuwataka wajumbe kuchangia kwa uhuru na kuachana na utamaduni wa kutotoa mawazo au hoja na kuongeza kuwa jamii itapiga hatua katika maendeleo kama kila mtu atatoa mawazo na kuzungumza katika majadiliano.

Kupitia mada ya utafiti wa sheria kwa njia ya mtandao itakayofundishwa wakati wa mafunzo, Mhe. Dkt. Siyani ameeleza kuwa, Maofisa Mahakama hawataweza kutimiza wajibu wao bila kufanya utafiti na kwamba utafiti utawasaidia kujenga hoja na kuonesha sababu za kufanya maamuzi fulani, hivyo suala la utafiti lina umuhimu mkubwa katika kujenga uelewa wa kutosha jambo linatalosaidia wakati wa kutoa maamuzi yaliyo sahihi na kutenda kwa haki.

Aidha, Mhe. Dkt. Siyani amewahimiza wajumbe waliohudhuria mafunzo hayo kushiriki katika michezo itakayofanyika jioni baada ya mafunzo kukamilika ili kuendelea kulinda afya ya akili na kuimarisha afya ya mwili.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani ambaye pia ni Mlezi wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Masjala Kuu, akizungumza wakati alipofungua mafunzo na michezo kwa Wanachama wa TMJA Tawi la Masjala Kuu, leo tarehe 9 Aprili, 2026 katika ukumbi wa mikutano, Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Naibu Msajili Mahakama Kuu na Mkurugenzi wa Menejimenti ya Mashauri ya Mahakama ya Tanzania Mhe. Desdery Kamugisha ambaye pia ni Mwenyekiti wa TMJA Tawi la Masjala Kuu akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani ambaye pia ni Mlezi wa TMJA Tawi la Masjala Kuu ili afungua mafunzo na michezo kwa wanachama wa Tawi hilo.

Meza Kuu wakiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Masjala Kuu.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani ambaye pia ni Mlezi wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Masjala Kuu (katikati), kulia ni Mkurugenzi wa Menejimenti ya Mashauri ya Mahakama ya Tanzania na Mwenyekiti wa TMJA Tawi la Masjala Kuu Mhe. Desdery Kamugisha na kushoto ni Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Amani Aboud. 

Meza Kuu wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Masjala Kuu.

Meza Kuu wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe Wanawake wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Masjala Kuu.


Meza Kuu wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Masjala Kuu.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)





 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni