- Wafanya Tathmini ya mwenendo wa mashauri ya Jinai
Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma hivi karibuni ilifanya
Kikao cha Kusukuma Mashauri ya Jinai kilichoongozwa na Naibu Msajili wa Kanda hiyo,
Mhe. Fadhili Mbelwa kikilenga kutathimini na kuimarisha usimamizi na ufanisi wa
utoaji haki kwa wananchi mapema ipasavyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mbelwa alibainisha
kuwa kikao hicho kilijikita kuweka mikakati ya kuhakikisha mashauri ya jinai
kwa ngazi ya Mahakama Kuu yanasikilizwa haraka ili kuepuka mashauri ya mlundikano
huku zikiendelea juhudi za kuhimizana wadau kila mmoja kutimiza wajibu wake
katika mnyororo wa haki jinai ili waisaidie Mahakama kutekeleza jukumu lake la
msingi haraka iwezekanavyo.
“Tunafahamu kwamba, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George
Masaju alikwishaelekeza umri wa mashauri
kwa kila ngazi ya Mahakama, hivyo mashauri yanapaswa kumalizika ndani ya muda
uliowekwa, hivyo sote tushirikiane kuhakikisha kwamba ukomo wa muda kwa kila
ngazi ya Mahakama unazingatiwa ili mashauri ya mlundikano ibaki historia kwa
Mahakama Kanda ya Kigoma,” alisema Naibu Msajili huyo.
Kwa upande wake, Mjumbe mwalikwa kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Mkoa wa Kigoma ambaye ni Ofisa Uhifadhi Wakimbizi, Bw.
Aganyira Rugemarila, aliishukuru Mahakama na kuipongeza kwa jinsi ilivyojipanga
kiuhudumia mashauri ya wakimbizi kutoka nchi za Jirani.
“Tunaipongeza Mahakama Kigoma, kwa hakika mnafanya kazi
nzuri sana kwenye mashauri ya wakimbizi kwani mnasikiliza na kutoa hukumu
kwa wakati, hata hivyo tumeona wakimbizi
wengi wanaokutwa na hatia, Mahakama imekuwa ikitoa vifungo mbadala yaani kifungo
cha nje chini ya Idara ya Huduma kwa Jamii, wakimbizi wanafanya adhabu hizo
kisha wanamaliza salama badala ya kukaa gerezani kwa muda wote waliofungwa,”
alisema Bw. Rugemarila
Aidha, shukrani hizo zilienda sambamba kwa wadau wa haki
jinai kwa ushirikiano wanaoutoa katika kutatua changamoto za wakimbizi
zinapojitokeza, kwani wadau wa haki jinai wamekuwa mstari wa mbele kushirikiana
na Idara ya Wakimbizi katika kuhakikisha maisha ya wakimbizi Mkoa wa Kigoma yanafuata sheria za nchi ndani
na nje ya Kambi walizohifadhiwa Mkoani
Kigoma.
Waliohudhuria kikao hicho ni wajumbe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Magereza, Polisi, Ofisi ya Upelelezi
Mkoa, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Kigoma (NPS), Ustawi wa Jamii, Chama
cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Idara ya Marekebisho ya Tabia, Ofisi ya Mganga
Mkuu wa Mkoa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mjumbe
kutoka UNHCR Mkoa wa Kigoma.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa akizungumza jambo hivi karibuni wakati wa Kikao cha Kamati ya Haki Jinai ya Mahakama Kanda ya Kigoma.
Mkuu wa Gereza la Mkoa wa Kigoma, Bw. Bosco Lupala akisikiliza kwa makini mjadala uliokuwa ukiendelea wakati wa Kikao cha Kamati ya Haki Jinai Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.
Sehemu ya wajumbe wakifuatilia kwa makini taarifa yaliyokuwa yakijiri wakati wa Kikao cha Kamati ya Wadau wa Haki Jinai Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.
Mjumbe mwalikwa kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Mkoa wa Kigoma, Bw.Aganyira Rugemarila akitoa pongezi na shukrani kwa Wadau wa Haki Jinai wakati wa Kikao cha Kamati ya Haki Jinai.
Ofisa Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Uhamiaji, Bw. Rudger Kilala akifuatilia taarifa za kikao wakati wa Kikao cha Kamati ya Wadau wa Haki Jinai kilichofanyika hivi karibuni Mahakama Kuu Kigoma.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni