Jumatano, 8 Aprili 2026

SUMBAWANGA YAMKARIBISHA MSAJILI MPYA

Na SHARIFU MOKIWA, Mahakama-Sumbawanga

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga ilifanya kikao cha watumishi chenye lengo la kuwatambulisha watumishi wapya pamoja na kutoa maelekezo ya kuboresha utendaji kazi wa utoaji huduma kwa wananchi.

Kikao hicho kilichofunguliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Mhe. Frederick Manyanda na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Thadeo Mwenempanzi, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Bw. Machumu Essaba, Naibu Msajili Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Pamela Mazengo pamoja na Watumishi wa Mahakama.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Manyanda aliwakaribisha watumishi wapya waliopangiwa kufanya kazi Mahakama Kanda ya Sumbawanga kutoka maeneo mbalimbali ya nchi akisisitiza umuhimu wa kuzingatia kanuni na maadili ya utumishi wa Umma.

Alieleza kuwa, kila mtanzania ana haki ya kuishi na kufanya kazi popote nchini ilimradi anazingatia sheria na taratibu, huku akiwahimiza watumishi kupenda maeneo yao ya kazi na kuyachukulia kwa mtazamo chanya. “Tanzania ni nchi yetu sote kila mtu ana haki ya kuishi mahali popote ilimradi havunji sheria za nchi.” Amesema Mhe. Manyanda.

Aidha, Mhe. Manyanda alisisitiza uwajibikaji, uadilifu na weledi na pia kujiongeza (Proactivity) katika utekelezaji wa majukumu pamoja na umuhimu wa kujifunza na kujiendeleza kitaaluma.

Naye, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Bw. Machumu Essaba aliwasilisha mrejesho wa kikao cha bajeti kilichofanyika tarehe 16 hadi19 Februari, 2026 kilichofanyika Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.

Bw. Essaba alieleza kuwa, rasilimali fedha ni chache hivyo matumizi yake yanapaswa kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa ili kuhakikisha shughuli za Mahakama zinaendelea kwa ufanisi.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa ushurikiano wa karibu katika utendaji kazi kati ya Mtendaji na Naibu Msajili katika kuimalisha utekelezaji wa majukumu ya kimahakama. “Naibu Msajili ni injini ya utekelezaji wa majukumu ya kimahakama katika Kanda,” aliongeza Mtendaji huyo.

Bw. Essaba alisema kuwa, masuala ya kiutawala ikiwemo usimamizi wa matumizi ya fedha kwa kuzingatia bajeti, matengenezo na usalama wa magari ya Mahakama, na utunzaji wa mazingira ya ofisi, vilevile alikumbusha umuhimu wa nidhamu ya mahudhurio kazini, ambapo kutosaini siku tano mfululizo huhesabika kama utoro.

Vilevile, Bw. Essaba alitumia fursa hiyo kumkaribisha Naibu Msajili mpya wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Mhe. Pamela Mazengo aliyehamia kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Tabora ili kuchukua nafasi ya Mhe, Joseph Luambano aliyehamia Mahakama Kuu, Kanda ya Njombe.

Mara baada utambulisho huo Mhe. Mazengo alisema kuwa, amekuja kujifunza, kushirikiana na watumishi katika kuhakikisha utoaji wa haki kwa wananchi unafanyika kwa ufanisi. “Nimekuja kujifunza na kushirikiana nanyi tusimame pamoja katika jukumu la kutenda haki kwa wateja wetu kwa upendo.”

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Mhe, Thadeo Mwenempazi aliwakumbusha watumishi wapya kuwa ajira ni jukumu la mtu binafsi na kila mtumishi anapaswa kuwajibika kikamilifu katika nafasi yake. Alisisitiza matumizi ya muda na umuhimu wa kujifunza kwa bidii ili kujenga msingi mzuri wa maisha ya baadae.

Katika hatua nyingine Jaji mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Mhe. Manyanda aliwasilisha tuzo aliyopokea kama pongezi na shukrani kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Katavi kama kielelezo cha mchango wake katika kuisimamia na kuilea Mahakama hiyo hadi kufikia hatua ya kujitegemea kiutendaji.

Jaji Mfawidhi Mahakama ya Sumbawanga Mhe. Frederick Manyanda (aliyesimama) akitoa nasahaa kwa watumishi wapya kuhusu uwajibikaji, maadili na utumishi bora. Wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Mhe.Thadeo Mwenempazi (kushoto), Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Bw. Machumu Essaba (wa kwanza kulia) na Naibu Msajili Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Pamela Mazengo.

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Mhe.Thadeo Mwenempazi akizungumza neno wakati wa kikao cha watumishi.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Bw. Machumu Essaba akiwasilisha mrejesho wa kikao cha bajeti na kusisitiza mtumizi sahihi ya rasilimali za umma.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Mhe. Pamela Mazengo akizungumza baada ya kutambulishwa rasmi mbela ya watumishi.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Mhe. Frederick Manyanda akizindua Kitabu cha Utendaji kazi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga kwa mwaka 2025.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Mhe. Frederick Manyanda akiwasilisha tuzo aliyopokea kama pongezi na shukrani kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Katavi kwa mchango wake katika kuisimamia na kuilea Kanda hiyo.

Watumishi wapya wa Mahakama waliosimama wakati wa utambulisho ili kutengeneza namna bora ya kuwajengea uelewa wa pamoja wa majukumu yao.

 



 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni