Ijumaa, 10 Aprili 2026

KIKAO CHA BARAZA LA WAFANYAKAZI DODOMA CHAFANYIKA

Na ARAPHA RUSHEKE, Mahakama Kuu Dodoma

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Suleimani Haji Hassan, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia uadilifu, weledi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma za haki, akibainisha kuwa misingi hiyo ni nguzo kuu ya utendaji wa Mahakama nchini.

Mhe. Hassan ameyasema hayo leo tarehe 10 Aprili, 2026, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kanda ya Dodoma uliofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi.

Amesema kuwa kila mfanyakazi wa Mahakama ana nafasi muhimu katika kutekeleza jukumu la kikatiba la utoaji haki, akirejea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayoweka wajibu wa kuhakikisha Wananchi wanapata haki bila ubaguzi.

Aidha, ameipongeza Menejimenti ya Mahakama kwa kuendelea kutekeleza matakwa ya kisheria ya uendeshaji wa mabaraza ya wafanyakazi, ikiwa ni pamoja na Tamko Na. 1 la mwaka 1970 na kanuni mbalimbali za utumishi wa umma zinazolenga kuwashirikisha katika maamuzi ya kiutendaji.

Jaji huyo amesisitiza kuwa mabaraza ya wafanyakazi yana jukumu la kuishauri Serikali kuhusu usimamizi wa rasilimaliwatu, kuboresha mazingira ya kazi, kulinda haki na wajibu wa Mwajiri na Mwajiriwa pamoja na kuimarisha ustawi wa Watumishi mahali pa kazi.

Amepongeza Wafanyakazi wa Mahakama kwa mchango wao katika utoaji wa haki na kutambua Wafanyakazi hodari wa mwaka 2026, akisema hatua hiyo ni chachu ya kuongeza ari ya utendaji kazi.

Kuhusu maadili, amesisitiza kuwa Watumishi wa Mahakama wanapaswa kuzingatia kanuni za maadili ya utumishi wa umma ili kuhakikisha utoaji wa huduma bora, akibainisha kuwa Mahakama ni chombo kinachobeba dhamana ya haki kwa Wananchi wote bila kujali hali, jinsia, dini au rangi.

Ameeleza kuwa Dira ya Mahakama ni kuhakikisha haki inapatikana kwa wote kwa wakati, akirejea misingi ya kikatiba inayolenga kulinda amani, usalama, maadili na umoja wa kitaifa.

Katika kuimarisha utendaji kazi, Jaji huyo amesisitiza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), akibainisha kuwa Mahakama inaelekea katika mfumo wa Mahakama Mtandao (e-Judiciary) utakaowezesha utoaji wa huduma za haki kwa njia ya kidijitali.

Amewataka Viongozi wa Mahakama ngazi zote kwenye Kanda hiyo kuhakikisha Watumishi wanapatiwa mafunzo ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi, uwazi na kasi ya utoaji haki pamoja na kupunguza mlundikano wa mashauri.

Aidha, Mhe. Hassan amerejea maelekezo ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyotolewa Februari 2, 2026, akisisitiza umuhimu wa kuongeza matumizi ya mifumo ya TEHAMA pamoja na kuzingatia uadilifu katika usimamizi wa sheria na utoaji haki.

Pia ametoa maelekezo kwa Viongozi katika Kanda hiyo kuhakikisha utekelezaji wa sera mbalimbali za mafunzo ya utumishi wa umma na Mahakama pamoja na mipango mkakati inayolenga kuboresha utendaji kazi.

Katika hatua nyingine, amesisitiza umuhimu wa Watumishi kulinda na kutumia kwa uangalifu rasilimali za Mahakama, akirejea wito uliotolewa kwa madereva wa Mahakama kuhusu kuzingatia nidhamu, usalama na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema Mahakama ina wajibu wa kuendelea kuwaelimisha Wananchi kuhusu taratibu na huduma zinazotolewa ili kuongeza uelewa na upatikanaji wa haki kwa urahisi zaidi.

Amehimiza Watumishi kufanya kazi kwa bidii, kuzingatia maadili na kutoa huduma bora kwa wakati, akisisitiza kuwa wao ni Waajiriwa wa Wananchi na wanapaswa kuwahudumia kwa uadilifu na weledi wa hali ya juu.

Vilevile katika baraza hilo kulikuwa na uchaguzi wa Viongozi ambao ni Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Dodoma, Mhe Dickson Tigalyoma, Naibu Katibu Baraza, Bi. Irine Msafiri pamoja na Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa Bi. Arapha Rusheke. Aidha katika Mkutano huo Wafanyakazi Hodari wa Mkoa wa Dodoma waliweza kutambuliwa.

Kabla ya Kufungwa kwa kikao hicho cha Baraza wajumbe mbalimbali pamoja na waalikwa walitoa neno la shukrani kwa Viongozi kwa kufanikisha kikao hicho. Baada ya kikao hicho wajumbe wote walirejea katika sehemu zako za kazi.


Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Suleimani Haji Hassan akisalimiana na wajumbe wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi mara baada ya kuwasili katika Viwanja vya Mahakama ya Wilaya Bahi.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Suleimani Haji Hassan akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Bahi.

 Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Suleimani Haji Hassan (katikati mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kutoka Mahakama Kuu Dodoma.

 

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Suleimani Haji Hassan, akifuatilia kwa makini kikao cha Baraza la Wafanyakazi katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi.

Meza kuu ikiongozwa na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Suleimani Haji Hassan (katikati), kulia kwake ni Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerald Gamba na kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Tughe Mkoa wa Dodoma, Bw. Maulid Kipeneku, wakiimba nyimbo ya mshikamano katika Baraza hilo lilofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Bahi.

Meza kuu ikiongozwa na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Suleimani Haji Hassan (aliyesimama) akisema neno wakati wa kikao hicho.  Kulia kwake ni Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Dodoma Mhe Gerald Gamba na kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Tughe Mkoa wa Dodoma Bw. Maulid Kipeneku, wakiimba nyimbo ya mshikamano katika baraza hilo lilofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Bahi.

Katibu anayemaliza muda wake, Mhe. Gerald Gamba (kulia) akimkabidhi mkataba Katibu Mpya, Mhe Dickson Tigalyoma, mara baada ya uchaguzi wakati wa kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya Wilaya ya Bahi.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam. 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni