- Wahimiza njia za amani kutatua migogoro
Na HALIMA MNETE-Mahakama, Dar es Salaam
Wadau wa sekta ya sheria nchini wameeleza kwa kina namna
usuluhishi unavyoendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuhakikisha Wananchi
wanapata haki kwa haraka, nafuu na kwa njia ya amani, huku wakisisitiza umuhimu
wa kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu mfumo huo.
Maelezo hayo yametolewa tarehe 9 Aprili 2026, katika
uzinduzi wa Wiki ya Usuluhishi 2026 uliofanyika katika ukumbi wa Golden Jubilee
Tower, jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe.George Masaju.
Katika hafla hiyo, kulikuwepo na mjadala kabambe ulioongozwa
na Jaji wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Dkt. Eliamani Laltaika, ulioshirikisha
Wadau mbalimbali waliotoa mitazamo yao kuhusu nafasi ya usuluhishi katika mfumo
wa utoaji haki nchini.
Akichangia mada hiyo, Mtaalamu wa Usuluhishi na Mwanzilishi
wa Taasisi ya ESS Creative and Legal Foundation, Bw. Eric Mukiza, alisisitiza
kuwa mawasiliano ndiyo msingi mkuu wa mafanikio ya usuluhishi.
Alibainisha kuwa ujumuishi (inclusion) ni jambo la
msingi, hasa kwa watu wenye ulemavu, ili kuhakikisha kila mmoja anapata fursa
sawa ya kusikilizwa na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa utatuzi wa
migogoro.
Kwa upande wake, kiongozi wa dini, Sheikh Zaila Hassan,
alieleza kuwa usuluhishi una mizizi ya kiimani, akisisitiza kuwa ni wajibu wa Wasuluhishi
kuzingatia haki, uadilifu na hofu ya Mungu katika kutekeleza majukumu yao.
Naye Chifu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mtemi Henry Mazengo wa
Pili, aligusia umuhimu wa mila na desturi katika kuendeleza utatuzi wa migogoro
kwa njia ya maelewano, akibainisha kuwa jamii nyingi za kiafrika zimekuwa
zikitumia mbinu hizo tangu zamani kudumisha amani na mshikamano.
Akizungumza kwa upande wa sekta ya fedha, Bw. Ramadhani
Myonga kutoka Benki Kuu ya Tanzania alieleza kuwa hapo awali kulikuwepo
changamoto za mifumo ya kushughulikia migogoro ya kifedha kutokana na
kukosekana kwa miongozo mahsusi (internal guidelines), hali
iliyosababisha malalamiko kutoka kwa wananchi.
Hata hivyo, alisema maboresho yaliyofanyika yamewezesha
kuanzishwa kwa mfumo wa “Sema na BoT” unaorahisisha Wananchi kuwasilisha na
kutatua malalamiko yao bila gharama.
Kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Peter Ernest Mogoro
alieleza kuwa moja ya majukumu ya Wizara hiyo ni kusaidia Wananchi kutatua
changamoto zao kupitia njia mbadala za utatuzi wa migogoro, ikiwemo usuluhishi.
Aliongeza kuwa programu kama “Mama Samia Legal Aid” zimekuwa msaada mkubwa kwa Wananchi
katika kupata haki.
Naye Bw. Lucas Malunde kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI,
alisisitiza kuwa Taasisi hiyo inalenga kuhakikisha uwepo wa utangamano ndani ya
jamii kwa kuhimiza matumizi ya usuluhishi katika ngazi za chini za utawala.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika
(TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, alibainisha kuwa chama hicho kinaendelea
kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa usuluhishi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za
kupunguza migogoro inayofikishwa mahakamani.
Kwa ujumla, Wadau hao walikubaliana kuwa usuluhishi umeleta
manufaa makubwa kwa wananchi kwa kuokoa muda na gharama, huku ukitoa nafasi ya
kufikia suluhu za kudumu kwa njia ya maelewano badala ya migogoro ya muda mrefu
mahakamani.
Uzinduzi wa Wiki ya Usuluhishi 2026 umefanyika chini ya
kauli mbiu isemayo: “Kutumia njia mbadala za utatuzi wa migogoro kama mbinu
inayopendelewa nchini Tanzania,” ikiwa ni jitihada za kuhamasisha matumizi
ya mfumo huo kwa manufaa ya jamii nzima.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni