- Naibu Waziri asema usuluhishi nguzo muhimu katika mfumo wa utoaji haki nchini
Na HALIMA MNETE-Mahakama, Dar es Salaam
Serikali imesisitiza umuhimu wa
matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro, hususan usuluhishi, kama njia bora
ya kuharakisha upatikanaji wa haki na kudumisha amani katika jamii.
Msisitizo huo umetolewa tarehe 9 Aprili, 2026 na Naibu
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainabu Katimba, wakati akitoa salamu zake
katika hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Usuluhishi 2026 uliofanyika katika ukumbi
wa Golden Jubilee Tower, jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju, ambaye alikuwa mgeni rasmi pamoja na Viongozi
mbalimbali wa Mahakama, Serikali, sekta binafsi na Wadau wa Sheria.
Uzinduzi wa Wiki ya Usuluhishi ulikuwa na kauli mbiu
isemayo: “Kutumia njia mbadala za utatuzi wa migogoro kama mbinu
inayopendelewa nchini Tanzania.”
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Katimba
amesema usuluhishi umeendelea kuwa nguzo muhimu katika mfumo wa utoaji haki
nchini kutokana na uwezo wake wa kupunguza gharama, kuokoa muda na kulinda
mahusiano ya kijamii na kiuchumi.
Aidha, ameeleza kuwa jitihada za kuimarisha usuluhishi
zinaendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga
kujenga mfumo wa haki wenye ufanisi na unaoweza kutoa huduma kwa wakati kwa Wananchi
wote.
“Matumizi ya usuluhishi ni sehemu ya dhamira ya Serikali
kuhakikisha Mahakama inakuwa chombo chenye ufanisi katika utoaji wa haki kwa
mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Mhe. Katimba.
Amefafanua kuwa tofauti na mwenendo wa kawaida wa mashauri
mahakamani, usuluhishi hutoa fursa kwa pande zinazohusika kufikia makubaliano
kwa hiari, kwa haraka na kwa gharama nafuu, hali inayochangia kuimarisha
mshikamano na utengamano katika jamii.
Kwa mujibu wa Mhe. Katimba, Serikali kupitia Wizara ya
Katiba na Sheria itaendelea kuunga mkono na kuimarisha matumizi ya njia mbadala
za utatuzi wa migogoro kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania pamoja na Wadau
mbalimbali.
Katika hatua nyingine, amesema Wiki ya Usuluhishi
inayotarajiwa kufanyika kuanzia Aprili 13 hadi 17, 2026, itatoa fursa kwa Wananchi
kupata elimu na huduma za usuluhishi bure katika Mahakama mbalimbali nchini.
Amesema hatua hiyo inalenga kuwahamasisha Wananchi kutumia
zaidi njia za maelewano katika kutatua migogoro yao, badala ya kutegemea
mashauri marefu na yenye gharama kubwa mahakamani.
Aidha, amewahimiza Wadau wa sekta ya sheria, wakiwemo Mawakili,
Wasuluhishi na Watumishi wa Mahakama, kuendelea kuhamasisha matumizi ya
usuluhishi pamoja na kutoa elimu kwa umma ili kuongeza uelewa na imani ya Wananchi
katika mfumo huo.
Kwa upande wa Serikali, Mhe. Katimba amesema juhudi
zinaendelea kufanyika katika kuboresha sekta ya sheria ikiwa ni pamoja na
kuimarisha miundombinu ya Mahakama, kuongeza rasilimali watu na kuendeleza
matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuhakikisha haki
inapatikana kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.
Amesisitiza pia umuhimu wa maadili, weledi na uadilifu kwa Wasuluhishi
ili kuhakikisha mchakato wa usuluhishi unafanyika kwa haki, uwazi na kwa
kuzingatia misingi ya sheria.
Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Katimba ametoa wito kwa Wananchi
kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Wiki ya Usuluhishi na kutumia fursa hiyo
kumaliza migogoro yao kwa njia ya amani na maelewano.
Uzinduzi huo umeacha mwamko mpya miongoni mwa wadau wa sekta
ya sheria na jamii kwa ujumla, ukiashiria hatua muhimu katika juhudi za
Serikali za kuimarisha upatikanaji wa haki kwa njia mbadala na endelevu nchini.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainabu Katimba, akitoa salama katika hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Usuluhisho 2026 uliofanyika tarehe 9 Aprili 2026 katika ukumbi wa Golden Jubilee Tower jijini Dar es Salaam.
Viongozi mbalimbali wa Mahakama, Serikali, Sekta binafsi na wadau wa sheria walioudhuria katika hafla ya Wiki ya Usuluhishi 2026 iliyofanyika katika ukumbi wa Golden Jubilee Tower, jijini Dar es salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni