Jumatatu, 20 Aprili 2026

MAHAKAMA GEITA YAPOKEA UGENI KUTOKA DIVISHENI YA BIASHARA, MASJALA NDOGO SINGIDA

Na DOTTO NKAJA – Mahakama, Geita

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita, imeendelea kujipambanua katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), baada ya kupokea ugeni kutoka Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara ya Dar es Salaam pamoja na Mahakama Kuu Masjala Ndogo Singida.

Lengo la ziara hizo lilikuwa ni kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu matumizi ya TEHAMA katika uendeshaji wa shughuli za Mahakama.

Ugeni wa kwanza uliwasili tarehe 16 Aprili, 2026 ukitokea Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, ukiwa na wajumbe wanane ukiongozwa na Naibu Msajili, Mhe. Suzan Kihawa, pamoja na Mtendaji wa Mahakama, Anatory Kagaruki.

Ugeni wa pili ulitoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo Singida, ukiwa na Watumishi tisa, wakiongozwa na Naibu Msajili, Mhe. Evodia Kyaruzi, pamoja na Mtendaji wa Mahakama, Filbert Matotay.

Katika ziara hiyo, kulifanyika mafunzo yaliyofunguliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Geita, Mhe. Kevin Mhina, ambaye aliwakaribisha wageni na kuwashukuru kwa kuchagua Geita kama Kituo cha kujifunza.

Alieleza kuwa ziara hiyo ni fursa muhimu ya kubadilishana mawazo na uzoefu kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma za Mahakama kwa kutumia TEHAMA.

Jaji Mhina alibainisha kuwa mafanikio ya Mahakama Kuu Geita yametokana na misingi madhubuti iliyowekwa tangu kuanzishwa kwake, ikiwemo maelekezo ya Viongozi wakuu wa Mahakama, yaliyosisitiza umuhimu wa kuifanya Mahakama kuwa ya kisasa kidijitali.

Aliongeza kuwa matumizi ya TEHAMA yameongeza uwazi, yamepunguza gharama za uendeshaji, yamerahisisha upatikanaji wa taarifa na kuboresha mifumo ya ukaguzi wa shughuli za Mahakama.

Aidha, Jaji Mfawidhi alieleza kuwa mafanikio hayo yanatokana na mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa mara kwa mara wa mifumo, usimamizi thabiti wa Watumishi, ufuatiliaji wa karibu wa utendaji kazi, utoaji wa motisha, pamoja na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa Watumishi bila kujali kada zao.

Mafunzo hayo yalihusisha jumla ya mada tano zilizowasilishwa na Watumishi mbalimbali wa Mahakama, kwa lengo la kupeana uzoefu na kuboresha utendaji wa kazi.

Mada hizo zilitolewa na Naibu Msajili, Mhe. Fredrick Lukuna, Mtendaji wa Mahakama Bi. Masalu Kisasila, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Geita, Mhe. Mujuni Muchunguzi, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Nyankumbu, Mhe. Ally Mgomba, pamoja na Mtunza Kumbukumbu wa Mahakama Kuu Geita, Bi. Winfirda Ng’humbu.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mhe. Lukuna, alisisitiza kuwa mafanikio ya Taasisi yoyote yanategemea mshikamano wa pamoja miongoni mwa Watumishi wake.

Alieleza kuwa ni muhimu kuwa na malengo ya pamoja, kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu, kukubali makosa na kujifunza kutokana nayo, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa vitendea kazi vya kutosha.

Aidha, alihimiza utambuzi wa mapema wa changamoto zinazoweza kujitokeza ili zisikwamishe utekelezaji wa malengo yaliyowekwa.

Kwa upande wa mada ya utawala na matumizi ya TEHAMA, Mtendaji wa Mahakama Geita alieleza kuwa wamefanikiwa kuendesha shughuli nyingi za kiutawala bila matumizi ya karatasi.

Alifafanua kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa Watumishi wote pamoja na utayari wao wa kuendana na dira ya uongozi wa Mahakama Kuu Geita ya kuimarisha matumizi ya TEHAMA.

Akizungumza kwa niaba ya wageni, Mhe. Kihawa alitoa shukrani kwa mapokezi mazuri pamoja na mafunzo waliyoyapata, akieleza kuwa uzoefu huo utasaidia kuboresha utendaji katika Mahakama zao.

Naye Mhe. Kyaruzi alieleza kuridhishwa na mafunzo hayo na kuahidi kutumia maarifa hayo kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika Masjala zao.

Wageni walipata fursa ya kujionea kwa karibu namna Mahakama Kuu ya Geita ilivyofanikiwa kufikia hatua ya matumizi kamili ya TEHAMA katika utoaji wa huduma zake.

Kupitia uzoefu huo, wageni hao waliondoka wakiwa na matarajio na dhamira ya kutekeleza maboresho makubwa zaidi katika maeneo yao ya kazi, wakilenga kuiga na kuendeleza mifumo waliyoishuhudia.

Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa wanakuwa sehemu ya mabadiliko chanya yatakayochochea utoaji wa huduma za haki kwa Wananchi kwa ufanisi zaidi, uwazi ulioboreshwa na kwa wakati muafaka.

Kwa mtazamo wa jumla, ziara hizi zimekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA ndani ya Mahakama za Tanzania.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Geita, Mhe. Kevin Mhina akifungua mafunzo.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita, Mhe. Fredrick Lukuna, akitoa ufafanuzi juu ya ushirikiano biana ya Viongozi na Watumishi unavyoleta mafanikio katika kuongeza ufanisi wa matimizi ya Tekinolojia ya Habari na mawasiliano (TEHAMA).

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Suzan Kihawa akitoa shukrani wakati wa ziara waliyoifanya Mahakama Kuu Geita.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Singida, Mhe. Evodia Kyaruzi akieleza jinsi Geita ilivyowavutia kwenye matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Mtendaji wa Mahakama Geita, Bi. Masalu Kisasila, akielezea namna utawala Mahakama Geita ulivyoachana na matumizi ya karatasi.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Geita, Mhe. Mujuni Muchunguzi, akieleza jinsi Mahakama za Wilaya wanavyotumia mifumo katika Mahakama za Wilaya.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Nyankumbu, Mhe. Ally Mgomba, akieleza jinsi Mahakama za Mwanzo zilivyoachana na matumizi ya karatasi kwa kubuni Mfumo wa Mahakama za Mwanzo.

Picha ya pamoja ya Watumishi wa Mahakama Kuu Geita na Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara.


 Picha ya pamoja ya Watumishi wa Mahakama Kuu Geita na Mahakama Kuu Singida.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni