Jumatatu, 20 Aprili 2026

MAHAKAMA SONGEA YAZINDUA MAJENGO MATATU YA MAHAKAMA ZA MWANZO

Na NOEL SYLIVESTER – Mahakama, Songea

Mahakama ya Tanzania katika Mkoa wa Ruvuma, tarehe 17 Aprili, 2026 imezindua Mahakama za Mwanzo tatu kwenye Wilaya mbalimbali baada ya ujenzi wake kukamilika.

Uzinduzi huo uliongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Songea, Mhe. James Karayemaha, ambao ulifanyika kwa pamoja katika Viwanja vya Mahakama ya Mwanzo Lilondo katika Wilaya ya Songea.

Mahakama nyingine zilizozinduliwa ni Mahakama ya Mwanzo Likuyusekamaganga iliyopo katika Wilaya ya Namtumbo na Mahakama ya Mwanzo Nalasi iliyopo Wilaya ya Tunduru.

Uzinduzi wa Mahakama hizo unalenga kurahisisha upatikanaji wa haki kwa Wananchi, kupunguza umbali wa kufuata huduma za kimahakama na kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki kwa wakati na garama nafuu.

Katika hafla hiyo, Jaji Mfawidhi aliongelea dhima ya Mahakama katika kutoa haki kwa wakati unaostahili bila kuchelewesha huduma hizo za msingi kwa Wananchi.

Vilevile, Mhe. Karayemaha aliwaasa Watumishi na Wananchi wa maeneo hayo  kuhakikisha wanayatunza majengo hayo na miundombinu yake ili yaweze kudumu kwa muda mrefu.

“Kuanzishwa kwa Mahakama hizi kutasaidia kupunguza msongamano wa mashauri na kuharakisha utoaji wa haki. Hatua hii ni sehemu ya juhudi za Mahakama na Serikali ya Tanzania kuhakikisha kila Mwananchi anapata haki kwa wakati na kwa ghalama nafuu,”alisema.

Kwa upande wake, mgeni maalumu katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Kapenjama Ndile, aliwaasa Wananchi kushirikiana na Watumishi wa Mahakama kwa ajili ya kulinda msingi wa amani na kudumisha ustawi wa utoaji haki kwa Wananchi.

“Mahakama ni mali ya Wananchi, hivyo ni wajibu wetu sote kushirikiana na kuyatunza majengo ya Mahakama zetu pamoja na miundombinu yake kwa ujumla,” alisema Mhe. Ndile.

Katika taarifa yake, Mtendaji wa Mahakama Songea, Bw. Allan Mwela, alitoa ufafanuzi kuhusu majengo hayo ambayo yamezinduliwa na gharama zilizotumika mpaka kukamilika kwa ujenzi wa majengo hayo yote matatu.

Alibainisha kuwa Mahakama ya Mwanzo Lilondo mpaka kukamilika kwake imetumia 985,625,739/=. Mahakama ya Mwanzo Likuyusekamaganga imegharimu 961,400,162/= na Mahakama ya Mwanzo Nalasi imegharimu 1,007,033,928.18/=, hivyo kufanya  jumla ya 2,954,059,829.18/=

Hafla hiyo pia ilihudhuliwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama Kuu Songea, Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru, pamoja na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Songea, Mhe. James Karayemaha akihutubia katika hafra ya uzinduzi wa Mahakama za Mwanzo tatu baada ya ujenzi wake kukamilika.

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Kapenjama Ndile, akihutubia katika hafla hiyo.

Mtendaji wa Mahakama Songea, Bw. Allan Mwela, akisoma taarifa ya ujenzi wa Mahakama hizo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Songea, Mhe. James Karayemaha (wa tatu kutoka kushoto) akikata utepe kuashiria kuzinduliwa wa Mahakama hizo.

Sehemu ya Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama waliohudhulia hafla hiyo.

Kikundi cha Ngoma za Asili kikitumbuiza wakati wa halfa hiyo.

Sehemu ya Wananchi wa Lilondo wakishuhudia uzinduzi wa Mahakama hizo.

Sehemu ya Wanafunzi waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa Mahakama hizo. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Songea, Mhe. James Karayemaha (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa Serikali waliohudhuria katika hafla hiyo.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni