Jumatatu, 20 Aprili 2026

MAHAKIMU WAPATIWA MAFUNZO KUHUSU TARATIBU UCHUKUAJI MAELEZO YA UNGAMO

Na ARAPHA RUSHEKE, Mahakama Kuu Dodoma.

Mahakama Dodoma tarehe 17 Aprili, 2026 iliendesha mafunzo ya taratibu za uchukuaji wa maelezo ya ungamo, yakihusisha Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kutoka Dodoma na Singida.

Mafunzo hayo yaliyoendeshwa kwa mfumo mseto, yalifanyika katika ukumbi wa Mahakama uliopo Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma.

Baadhi ya washiriki walihudhuria ana kwa ana ukumbini, huku wengine wakishiriki kwa njia ya mtandao kupitia kiunganishi maalumu. Hatua hiyo iliwezesha ushiriki mpana zaidi wa Mahakimu, wakiwemo wale ambao hawakuweza kufika eneo la mafunzo.

Akifungua mafunzo hayo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo, alisisitiza umuhimu wa Mahakimu kuzingatia kikamilifu taratibu za kisheria katika uchukuaji wa maelezo ya ungamo ili kulinda haki na kuhakikisha ushahidi unaokubalika mahakamani.

“Ubora wa uamuzi wa Mahakama huanza na ubora wa ushahidi unaowasilishwa, ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa maelezo ya ungamo yanachukuliwa kwa kuzingatia kikamilifu sheria, miongozo na kanuni zilizowekwa,” alisema Dkt. Masabo.

Katika hotuba yake, aliwashukuru kwa dhati wawezeshaji wa mafunzo hayo kwa kujitoa kwao, hususan wale waliowezesha mafunzo kwa njia ya mtandao, akiwemo Naibu Msajili na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za Mahakama, Ukaguzi, Mrejesho kwa Umma na Maadili, Mhe. Maira Kasonde, pamoja na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mombo, ambaye pia ni mwezeshaji wa mafunzo hayo.

Aidha, alitambua na kushukuru ushiriki wa Viongozi wa juu wa Mahakama waliohudhuria kwa njia ya mtandao, akiwemo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Singida, Mhe. Ayubu Mwenda, ambaye alifuatilia mafunzo hayo kama sehemu ya kuimarisha utoaji haki katika maeneo yao.

Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea Mahakimu uelewa wa kina kuhusu taratibu sahihi za kisheria katika uchukuaji wa maelezo ya ungamo, pamoja na kuwapa mbinu bora za vitendo zitakazosaidia kuepuka makosa ya kiutaratibu yanayoweza kuathiri ushahidi na uamuzi wa Mahakama.

Kupitia mafunzo hayo, Mahakimu wamekumbushwa umuhimu wa kufuata miongozo ya sheria katika kila hatua ya uchukuaji wa maelezo ya ungamo, ikiwemo kuhakikisha mtuhumiwa anafahamishwa haki zake, kurekodi maelezo kwa usahihi, na kuthibitisha uhalali wa maelezo hayo kwa mujibu wa sheria.

Mafunzo hayo yameacha alama muhimu kwa washiriki, yakiwakumbusha wajibu wao mkubwa katika kulinda haki za Wananchi kupitia uzingatiaji sahihi wa sheria na taratibu.

Kwa kuzingatia mabadiliko ya mifumo ya utoaji haki na changamoto zinazoendelea kujitokeza, utoaji wa mafunzo hayo kwa njia ya ana kwa ana pamoja na mtandao unaonesha dhamira ya Mahakama ya Tanzania katika kuhakikisha Mahakimu wanakuwa na uelewa wa kisasa unaokidhi mahitaji ya wakati.

Hatua hiyo si tu inalenga kuboresha utendaji kazi wa Mahakimu, bali pia inalenga kuimarisha imani ya jamii kwa Mhimili wa Mahakama, ambapo haki haitolewi tu bali inaonekana ikitendeka kwa uwazi, weledi na uadilifu.

Akimhitimisha mafunzo hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Mhe. Zabibu Mpangule, amewashukuru washiriki kwa ushiriki wao mzuri, akisisitiza kuwa mafunzo hayo yatachangia kuleta mabadiliko chanya katika utoaji wa haki na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa Mahakama.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masab,o akisoma hotuba ya ufunguzi wa mafunzo ya taratibu za uchukuaji wa maelezo ya ungamo (Extra-Judicial Statements) kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo Dodoma.

 

Meza kuu ikiongoza na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo Dodoma Mjini waliohudhuria mafunzo hayo. Kulia kwake ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Mhe. Zabibu Mpangule na kushoto kwake ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Dodoma, Mhe Thurstone Kombe.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni