Na DHILLON UISSO-Mahakama, Dar es Salaam na REHEMA AWET-Mahakama, Mwanza
Baraza la Elimu ya
Sheria nchini, chini ya Mwenyekiti, ambaye pia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, hivi karibuni lilifanya ziara maalum, kukagua Vyuo
Vikuu vitatu, kama sehemu ya juhudi za kuimarisha ubora wa elimu ya sheria nchini.
Wajumbe wa
Baraza hilo walifanya ukaguzi katika Chuo
cha Kimataifa Kampala, Chuo Kikuu Huria Tanzania na Chuo cha St. Augustine
Mwanza.
Ziara hiyo ni sehemu ya mpango mpana
wa Baraza la Elimu ya Sheria wa kutembelea na kukagua mazingira ya vyuo
mbalimbali nchini ili kuhakikisha elimu ya sheria inatolewa kwa viwango
vinavyokubalika na vinavyoendana na mahitaji ya jamii
Akizungumza wakati wa ziara hizo, Mwenyekiti
wa Baraza la Elimu ya Sheria alisema kuwa lengo kuu ni kukagua na kuboresha
mifumo ya ufundishaji, mitaala, pamoja na miundombinu inayotumika kufundishia
sheria ili kuhakikisha wahitimu wanakidhi viwango vinavyotakiwa kitaifa na
kimataifa.
Alisema kuwa Baraza la Elimu ya Sheria lina jukumu la
kusimamia na kudhibiti ubora wa elimu hiyo nchini, hivyo ziara kama hizo ni
muhimu katika kubaini changamoto na kuweka mikakati ya kuzitatua kwa
kushirikiana na Taasisi husika.
Wakuu wa vyuo hivyo walipongeza ziara
hiyo, wakieleza ni fursa muhimu kwao ya kubadilishana mawazo na kupokea ushauri
utakaosaidia kuboresha utoaji wa elimu ya sheria.
Katika ziara hizo, Baraza pia
lilipata nafasi ya kukutana na Wanafunzi wa kitivo cha sheria vyuoni hapo na
kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili, pamoja na kupokea mapendekezo
yao ya namna ya kuboresha mazingira bora ya kujifunzia ili kuweza kupatikana
wanasheria bora.
Baraza pia lilipata wasaa wa kutembelea
baadhi ya maeneo katika vyuo vikuu hivyo, ikiwemo Moot Court, Maktaba, Mabweni ya
Wanavyuo, Ofisi za Viongozi pamoja na Walimu.
Aidha, Baraza
hilo lilifanya mazungumzo na uongozi wa vyuo hivyo na kupokea taarifa ili kuona
namna wanavyoweza kuboresha mitaala ili kuendana na soko la ajira.
Pamoja na hayo, Mwenyekiti wa Baraza alishauri namna bora ambayo inaweza kusaidia uhusiano mzuri kati ya vyuo hivyo, Mahakama na Taasisi mbalimbali za elimu katika kuandaa Wanafunzi bora na wenye tija katika soko la ajira.
Mapokezi ya Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza la Elimu ya Sheria
nchini katika Chuo Kikuu cha Kimataifa Kampala.
Wajumbe wa Baraza la Elimu ya Sheria pamoja na Wanafunzi wa Chuo
Kikuu Kampala.
Mwenyekiti wa Baraza la Elimu ya Sheria nchini, Mhe. Dkt
Mustapher Mohamed Siyani (katikati), Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kimataifa Kampala, Prof.
Honoratha Mushi (tatu kushoto) pamoja na Wajumbe wa Baraza la Elimu ya Sheria
nchini.
Mapokezi ya Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza la Elimu ya Sheria
nchini katika Chuo Kikuu Huria Tanzania.
Wajumbe wa Baraza la Elimu ya Sheria pamoja na Uongozi wa Chuo
Kikuu Huria Tanzania.
Mwenyekiti wa Baraza la Elimu ya Sheria nchini akitembelea
Maktaba ya Chuo Kikuu cha St. Augustine.
Mwenyekiti wa Baraza la Elimu ya Sheria nchini, Mhe. Dkt
Mustapher Mohamed Siyani (katikati), Mkuu wa Chuo cha St. Augustine, Padre.
Prof. Juvenalis Asantemungu (tatu kushoto) pamoja na Wajumbe wa Baraza la Elimu
ya Sheria nchini.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni