·
Ni kutoka Wizara ya
Katiba na Sheria
·
Wizara hiyo yaipatia pia
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Magari Matano na Kompyuta Mpakato 30
·
Mahakama na Tume…
waishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa vitendea kazi hivyo
Na
MARY GWERA & HABIBA MBARUKU, Mahakama-Dodoma
Mahakama ya Tanzania leo tarehe 15 Aprili,
2026 imekabidhiwa jumla ya Kompyuta Mpakato 150 kutoka Wizara ya Katiba na
Sheria, vifaa ambavyo vimekabidhiwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe.Dkt.
Juma Homera (MB) ikiwa ni jitihada za Serikali za za kuendeleza matumizi ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuimarisha utoaji haki kwa ufanisi.
Hafla
ya kukabidhi Kompyuta hizo iliyofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba jijini
Dodoma imeenda sambamba na kukabidhi jumla ya magari Matano na Kompyuta mpakato
30 vifaa ambavyo wamepatiwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Akizungumza
wakati wa hafla hiyo, Mgeni Rasmi, Mhe. Dkt. Homera amesema tukio hilo linathibitisha dhamira
ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuendelea kuimarisha Sekta
ya Sheria ili kuhakikisha
haki inapatikana kwa wananchi wote na kwa wakati bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
“Serikali
chini ya uongozi mahiri wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, imeweka kipaumbele katika
kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa kuhimiza kutumia fursa iliyopo
ya maendeleo ya TEHAMA nchini katika kuimarisha mifumo ya
kitaasisi ya utoaji wa huduma kwa umma kwa njia za kielekroniki. Fursa ya maendeleo
ya TEHAMA iliyopo ni kichocheo kikuu cha maendeleo ya
kiuchumi na kijamii. Hivyo, kwa
upande wa Sekta ya Sheria, matumizi
ya TEHAMA siyo ya hiari
tena, bali ni hitaji la msingi katika kujenga Mfumo wa Haki unaokwenda sambamba na mahitaji ya karne ya 21,”
amesema Mhe. Dkt. Homera.
Waziri huyo amesema kuwa, katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara hiyo yenye dhamana ya kusimamia masuala ya Katiba na Sheria, wameendelea kushirikiana na Taasisi zake katika kutekeleza majukumu yake, hususan kuimarisha mifumo ya utoaji haki na usimamizi wa haki nchini. Ametaja Taasisi hizo ni pamoja na Mahakama ya Tanzania ambayo imepewa jukumu la utoaji haki chini ya Ibara ya 1 07A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977; na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inayohamasisha hifadhi ya haki za binadamu, kwa kufanya uchunguzi na kupokea malalamiko ya uvunjaji wa haki za binadamu chini ya Ibara ya 1 29 na 1 30 ya Katiba.
Mhe. Dkt. Homera ameongeza kuwa, katika kutekeleza majukumu yake, Mahakama ya Tanzania na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora zinakutana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa vitendea kazi kama vile magari na kompyuta hivyo kushindwa kufikia malengo waliyojiwekea kiutendaji.
“Hivyo, katika
kutumia fursa hizo Wizara imekuwa
ikitafuta na kuingia makubaliano na wadau mbalimbali wa
maendeleo kutekeleza miradi na afua mbalimbali zinazolenga kuimarisha utendaji
wa Sekta ya Sheria. Katika
hili, Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo
la Umoja wa Mataifa (UNDP) imeona ni
vyema kuziwezesha taasisi hizi kwa kuzipatia vitendea kazi vichache ili kuimarisha uwezo wa kitaasisi katika
kuhudumia watanzania,” ameeleza.
Amesema, ana imani kwamba, vitendea kazi hivyo vitaenda kuboresha na kuimarisha utekelezaji wa majukumu na kuleta matokeo chanya na hatimaye kuwezesha Sekta ya Sheria kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050.
Aidha, Waziri huyo amebainisha kuwa, lengo la upatikanaji na utumiaji wa vifaa hivyo ni kutekeleza kwa vitendo Sera ya Serikali ya kujenga Mfumo Jumuishi, shirikishi na unaotumia teknolojia katika utoaji wa huduma za kisheria.
Mhe. Dkt. Homera ametoa rai kwa wanufaika wa magari na vifaa hivyo kuhakikisha vinatunzwa na kutumiwa vizuri ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya akitoa neno la shukrani kwa
niaba ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema vifaa hivyo
vitasaidia kuboresha utendaji kazi wa Mahakama, hususan katika matumizi ya
mifumo ya kielektroniki.
Ameeleza
kuwa, kompyuta hizo zitachangia kurahisisha usajili wa mashauri, usimamizi wa
kumbukumbu pamoja na uendeshaji wa mashauri kwa njia ya mtandao (video
conference), hatua itakayopunguza mlundikano wa kesi na kuongeza uwazi katika
utoaji wa haki.
Aidha,
amebainisha kuwa, matumizi ya TEHAMA ni nyenzo muhimu katika kuongeza kasi na
ufanisi wa utoaji wa huduma za Mahakama nchini.
Kwa
mujibu wa Msajili Mkuu, hatua hiyo pia itawezesha wananchi kupata huduma za Mahakama
kwa urahisi zaidi bila kulazimika kufika mahakamani, ikiwemo kufungua mashauri,
kufanya malipo na kufuatilia mwenendo wa mashauri.
Ameongeza
kwamba, maboresho ya kimahakama yamechangia kupungua kwa muda wa usikilizwaji
wa mashauri. Aidha, amebainisha kuwa tayari maboresho ya kimahakama yameanza
kuleta matokeo chanya, ambapo muda wa wastani wa kusikiliza na kuamua mashauri
umepungua hadi siku 68 mwaka 2025 kutoka viwango vya mwaka 2015.
Amesema
kuwa, katika Mahakama za Mwanzo, ambazo hushughulikia zaidi ya asilimia 70 ya
mashauri yote, muda wa usikilizwaji umepungua hadi wastani wa siku 30, hali
inayoonesha kuongezeka kwa ufanisi katika utoaji wa haki.
Katika
hafla hiyo, Msajili Mkuu aliambatana na baadhi ya Viongozi na Maofisa kutoka Makao
Makuu ya Mahakama. Viongozi wengine walioshiriki ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu
wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Franklin Rwezimula, Katibu Mtendaji wa Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bw. Patience Ntwina, Viongozi na watumishi
wengine wa Wizara hiyo pamoja na watumishi wa Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera (MB) akizungumza jambo wakati wa hafla ya Kukabidhi Magari na Vitendea Kazi kwa Mahakama ya Tanzania na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyofanyika leo tarehe 15 Aprili, 2026 katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Meza kuu ikiongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera (MB) (katikati). Wa pili kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Franklin Rwezimula, wa pili kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, wa kwanza kushoto ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bw. Patience Ntwina na wa kwanza ni kulia ni Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Bw. Shigeki Komatsubara wakiwa katika .
Meza kuu ikiongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi wa Mahakama walioambatana na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya (wa pili kulia) wakati wa hafla ya kukabidhi Magari na Vitendea Kazi kwa Mahakama ya Tanzania na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyofanyika leo tarehe 15 Aprili, 2026 katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Picha za pamoja wakati wa hafla ya kukabidhi Magari na Vitendea Kazi kwa Mahakama ya Tanzania na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyofanyika leo tarehe 15 Aprili, 2026 katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.














Hakuna maoni:
Chapisha Maoni