WANANCHI WAMIMINIKA MAHAKAMA KUU KUPATA ELIMU
Na
ARAPHA RUSHEKE-Mahakama Kuu, Dodoma
Wananchi
kutoka viunga mbalimbali jijini Dodoma, jana tarehe 14 Aprili 2026, walijitokeza
kwa wingi kushiriki na kujifunza kuhusu njia mbadala ya utatuzi wa migogoro.
Katika
mwendelezo huo, wananchi, wanasheria na watumishi kutoka Taasisi tofauti
wameonekana kuguswa na umuhimu wa usuluhishi, wakionesha hamasa kubwa ya
kufahamu namna bora ya kutatua migogoro kwa njia ya maelewano badala ya kutumia
njia ya kawaida, ambayo ni ndefu mahakamani.
Watoa
elimu wameweka wazi kuwa usuluhishi si tu unapunguza muda na gharama, bali pia
hujenga mahusiano bora kati ya wahusika, hali inayochangia kudumisha amani
katika jamii. Aidha, Usuluhishi unasaidia kupunguza msongamano wa mashauri
mahakamani na kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki.
Baadhi
ya washiriki wamesema elimu hiyo imekuwa chachu ya mabadiliko ya fikra,
wakiahidi kuwa mabalozi wa kueneza uelewa wa usuluhishi katika maeneo yao, ili
jamii iweze kunufaika zaidi na fursa hii muhimu.
Kwa
mtazamo mpana, juhudi hizi zinaakisi dhamira ya dhati ya Mahakama ya Tanzania
ya kuhakikisha haki haitafutwi kwa gharama kubwa au kwa muda mrefu, bali
inapatikana kwa njia rahisi, ya haraka na yenye kuzingatia utu.
Kwa kasi hii, ni wazi kuwa usuluhishi si mbadala
tena bali ni suluhisho halisi la migogoro katika jamii ya sasa.
Maadhimisho ya Wiki ya Usuluhishi yanayoendelea kuanzia tarehe 13 hadi 17 Aprili, 2026 kwenye maeneo mbalimbali nchini. Maadhimisho hayo yanaenda sambamba na kaulimbiu isemayo, “Kutumia Njia Mbadala ya Utatuzi wa Migogoro kama Mbinu Inayopendelewa ya Kutatua Migogoro nchini Tanzania.”
Wananchi kutoka sehemu mbalimbali
Mkoa wa Dodoma na Mikoa Jirani wakimsikiliza kwa makini mtoa mada ya usuluhishi,
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Dodoma, Mhe. Thurston Kombe, wakati wa
kutoa elimu ya usuluhishi katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma (IJC).
Mkazi
wa Dodoma, Bi. Ashura Salumu, akiuliza swali wakati wa utoaji wa elimu ya
usuluhishi katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni