Na SETH KAZIMOTO – Mahakama Arusha.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali amesema kuwa, usuluhishi wa migogoro ya kijamii ni njia bora ya utatuzi na kujenga jamii bora yenye amani, utengamano na maendeleo ya kudumu.
Mhe. Mahimbali aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa uzinduzi rasmi wa Wiki ya Usuluhishi nchini uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.
Akizungumza na umati wa wananchi na wadau mbalimbali wa Mahakama waliohudhuria uzinduzi huo, Jaji Mahimbali alisema kuwa, Mahakama ya Tanzania imezindua rasmi Wiki ya Usuluhishi ambayo itafanyika kuanzia tarehe 13 hadi 17 Aprili, 2026 ambapo tayari Mahakama imefanya uchambuzi wa mashauri yote yanayofaa kufanyiwa usuluhishi na kwamba wadaawa wote wanaohusika na mashauri hayo wamepewa taarifa na wako tayari kwa usuluhishi.
“Moja ya malengo yetu ni kuwajengea uelewa wananchi kwamba si lazima mashauri yaliyoletwa Mahakamani yaishe kwa uamuzi wa Mahakama, hivyo mashauri yote yanayofaa kufanyiwa usuluhishi yatafanyiwa hivyo, kwahiyo wadau wa Usuluhishi hususan pande mbili zinazohusika katika migogoro wanapaswa kuwa tayari kwa majadiliano” aliongeza Jaji Mfawidhi huyo.
Vilevile Mhe. Mahimbali aliainisha kwamba, malengo yanayotarajiwa kufikiwa baada ya kukamilika kwa Wiki ya Usuluhishi kuwa ni pamoja na: Kujenga uelewa na umuhimu wa usuluhishi katika utatuzi wa migogoro, kuelimisha umma juu ya umuhimu na fursa zinazotokana na matumizi ya njia ya usuluhishi, kuharakisha upatikanaji wa haki mapema ipasavyo na kuongezeka kwa wigo wa usuluhishi wa migogoro iliyopo katika hatua mbalimbali mahakamani.
Malengo mengine ya Wiki ya Usuluhishi katika Kanda ya Arusha ni kupunguza msongamano wa migogoro ambayo inaweza kutatuliwa kwa njia ya usuluhishi na kuweka misingi ya maridhiano ya kudumu, kwamba usuluhishi lazima ujikite katika makubaliano ya pande zote mbili.
Yapo manufaa mengi yanayopatikana pale migogoro ya wananchi inapotatuliwa kwa njia ya usuluhishi. Manufaa hayo ni pamoja na ongezeko la uwajibikaji wa watoa huduma za usuluhishi na wenye migogoro kwa lengo la kumaliza kwa haraka, kwa njia ya amani na utulivu. Pia, kuongezeka kwa soko la ajira kupitia kutambulika kwa wasuluhishi binafsi ambao ni watu wasio Mahakimu au Majaji lakini wana maarifa na weledi wa kutosha katika kutatua migogoro katika jamii.
Kwa Kanda ya Arusha, Wiki ya Usuluhishi itasaidia kuchochea mazingira wezeshi ili kuokoa na kufungua rasilimali zilizoshikiliwa kutokana na uwepo wa migogoro kama vile mashauri ya kibenki na migogoro ya kibiashara. Pia, usuluhishi wa haraka wa migogoro utawawezesha wananchi kutumia muda mchache mahakamani na kupata muda mwingi wa kushiriki kazi za kiuchumi, kuvutia wawekezaji na kuharakisha maendeleo ya watu na Taifa kwa ujumla.
Hali kadhalika, moja ya faida kubwa inayopatikana kwa kutatua migogoro ya kijamii kwa njia ya usuluhishi ni kuongezeka kwa imani ya wananchi kwa mfumo wa utoaji haki nchini. Wananchi wanapoona migogoro yao inatatuliwa kwa haraka, kwa haki na kwa njia ya amani, imani yao kwa Mahakama na Mfumo mzima wa Utoaji Haki inaongezeka kwa kiasi kikubwa.
Aidha, uwepo wa Wiki ya Usuluhishi nchini ni kutekeleza jukumu la Kikatiba chini ya Ibara ya 107 A (2) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) ambapo kupitia Wiki ya Usuluhishi, Mahakama inatekeleza jukumu lake la kukuza na kuendesha usuluhishi nchini.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni