Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile amewapitisha washiriki wa
mafunzo ya Usuluhishi kuhusu sheria, kanuni na miongozo ya usuluhishi inayotoa mwelekeo
wa utatuzi na utambuzi wa kiini cha
mgogoro inayofikishwa Mahakamani.
Mhe. Rwizile ametoa mada hiyo leo
tarehe 14 Aprili, 2026 mkoani Kigoma kwa washiriki 16 wa mafunzo ya usuluhishi wa migogoro yanayoendelea Mahakama
Kuu Kigoma.
“Tunazo sheria, kanuni na miongozo ya
usuluhishi inayotoa welekeo wa utatuzi na utambuzi wa kiini cha mgogoro
inayofikishwa Mahakamani, hata hivyo zipo hatua nne muhimu za usuluhishi
zikifuatwa na kuzingatiwa na msuluhishi yeyote basi mgogoro uliopo mbele ya msuluhishi
utaleta matokeo mazuri,” amesema Jaji Rwizile.
Ameongeza kuwa, ni muhimu kwa Msuluhishi
kuwa na ufahamu mkubwa wa kanuni za usuluhishi ili kufikia makubaliano ya
usuluhisi wa mgogoro, na kwamba wasifungwe na uelewa mbalimbali unaotokana na kanuni,
sheria na miongozo mingine inayotumika katika usuluhishi wa migogoro kutoka
nchi mbalimbali duniani bali wajielekeze kwenye utatuzi wa mgogoro husika.
Kwa upande wake Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa amewasilisha mada juu ya utambuzi
wa kiini cha mgogoro, ikiwa ni kuwasikiliza walengwa wa mgogoro, nini
wanahitaji kila mmoja katika mgogoro huo, kisha kuwapa nafasi kila mdau kuweza
kutoa mawazo ya kile anachohitaji katika kusuluhisha mgogoro huo, kuwapatia
kila mmoja kile ambacho ataridhika nacho ili kumaliza migogoro iliyopo mahakamani.
Aidha, alifafanua mbinu mbalimbali wanazopaswa kutumia wasuluhishi hao ili kuendelea kuwa bora katika usuluhishi, hasa kutengeneza mazingira rafiki kwa walengwa wa mgogoro, mpangilio wa kuketi katika chumba cha usuluhishi, utoaji wa taarifa juu ya kila kitu kitakachofanyika katika usuluhishi, kuwaeleza malengo ya usuluhishi huo na jukumu lao la msingi katika usuluhishi, kuwatambua wadau wenye mgogoro husika bila upendeleo wala ubaguzi ikiwa ni sambamba na matarajio yao kupitia usuluhishi huo, kuwapa muda sawa wa kuzungumza, kujieleza na uwazi usio na mashaka.
Leo ni siku ya pili ya mafunzo kwa washiriki hao, wakiendelea kunolewa kwa ufasaha ili waje kuwa Wasuluhishi maridadi wa kutatua migogoro iliyopo hapa nchini.
Washiriki wa mafunzo hayo ni Mahakimu
wa Kanda za Kigoma, Bukoba, Musoma na Mwanza.
Washiriki wa mafunzo wakitoa mfano halisi wa jinsi Msuluhishi na Mdau wanaweza kukaa na kuzungumza juu ya jambo fulani linalohitaji usuluhishi.
Moja ya picha inayotumika na wakufunzi katika chumba cha kutolea mafunzo ya usuluhishi Mahakama Kuu Kigoma.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni