Na MICHAEL RITTE, Mahakama-Bukoba
Mahakimu, Waendesha
Mashtaka na Maofisa Ustawi wa Jamii kutoka Mikoa ya Kagera, Geita, Rukwa na
Katavi wameanza kupatiwa mafunzo maalum ya siku tatu yenye lengo la kuwajengea
uwezo wa kuepuka kutonesha majeraha kwa waathirika wa ukatili wa kingono wakati
wa mchakato wa utoaji haki.
Mafunzo hayo yaliyoanza tarehe
20 Aprili, 2026 yalifunguliwa na yamefunguliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu
Masjala Ndogo ya Bukoba, Mhe. Immaculata Banzi kwenye ukumbi wa Mahakama
Kuu Kanda ya Bukoba.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi hayo, Mhe. Banzi alisisitiza umuhimu wa wataalamu wa sheria kuwa
makini wanaposhughulikia mashauri ya ukatili wa kingono huku akibainisha kuwa
ukatili huo huacha madhara makubwa ya kihisia na kisaikolojia kwa waathirika.
“Unyanyasaji wa kingono
na ukatili wa kijinsia huacha majeraha makubwa ya kihisia na kisaikolojia kwa
waathirika. Tusipokuwa waangalifu hata mchakato wa kisheria unaweza kuwaongezea
maumivu manusura,” alisema Jaji Mfawidhi huyo.
Ameongeza kwa kusema kuwa, “Tusipokuwa waangalifu,
mchakato wa kisheria wenyewe unaweza kuwaongezea maumivu manusura wa ukatili wa
kingono. Hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha wanajisikia vizuri, wanasikilizwa na
kuheshimiwa.”
Sambamba na hilo, mafunzo kama hayo yanafanyika pia Sumbawanga ambapo yamefunguliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Sumbawanga, Mhe. Frederick Kapela Manyanda.
Kwa upande wake, Mhe. Manyanda
alieleza kuwa, mazingira yasiyo rafiki pamoja na maswali yasiyo na staha wakati
wa usikilizwaji wa mashauri yanaweza kuwaumiza zaidi manusura wa ukatili wa
kingono.
Alisisitiza kuwa,
wahusika wa mifumo ya haki wana wajibu mkubwa wa kulinda utu na ustawi wa
waathirika katika hatua zote za shauri.
Kwa mujibu wa Mratibu wa
Mafunzo, Mhe. Gloria Shuma amesema
kwamba, washiriki watapatiwa maarifa na mbinu za kitaalamu ikiwemo
matumizi ya lugha yenye huruma na staha pamoja na namna ya kujenga mazingira
rafiki ya kimahakama kwa waathirika wa ukatili wa kingono.
Lengo kuu la mafunzo hayo
ni kuhakikisha kuwa waathirika wanapatiwa mazingira salama yenye kuheshimu utu
wao na yanayowawezesha kutoa ushahidi bila hofu wala shinikizo la kisaikolojia.
Mafunzo ya aina hiyo
tayari yameshafanyika katika mikoa mbalimbali ikiwemo Tanga, Dodoma, Dar es
Salaam, Kigoma, Mtwara, Mbeya, Mwanza, Morogoro, Arusha, Musoma na Songea.
Jitihada hizi ni sehemu
ya mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa kuimarisha utoaji haki kwa kuzingatia
misingi ya huruma, usawa na ujumuishi, hususan kwa makundi maalum kama
waathirika wa ukatili wa kijinsia.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya ‘Irish Rule of Law International’ (IRLI) kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania. Hii ni sehemu ya awamu ya tano ya mafunzo hayo yanayoendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali nchini.
Hakimu Mkazi ambaye ni Mratibu wa Mafunzo ya Mahakama, kutoka Chuo cha Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Gloria Shuma akitoa neno la utangulizi wakati wa Ufunguzi wa mafunzo kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba.
Sehemu ya washiriki/ wawakilishi katika mafunzo hayo. Wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Missenyi, Mhe. Nelson Bagenda, na wadau mbalimabali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mshataka (NPS) na Ofisi ya Ustawi wa Jamii wakiwa katika mafunzo hayo yanayoendeshwa kwenye Ukumbi wa Mahakama Kuu Bukoba.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba, Mhe. Immaculata Banzi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba, Mhe. Lilian Itemba (kushoto), Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba, Mhe Ferdinand Kiwonde (kulia). Waliosimama nyuma kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba, Mhe. Said Mkasiwa katikati ni Naibu Msajili kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu Dodoma, Mhe Mwajabu Mvungi na kushoto ni Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma ambaye pia Mwezeshaji wa Mafunzo, Mhe Fadhili Mbelwa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba, Mhe. Immaculata Banzi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba, Mhe. Lilian Itemba (kushoto), Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba, Mhe Ferdinand Kiwonde (kulia). Waliosimama ni Wawakilishi kutoka Ofisi ya Mashtaka, Bw. Robert Neophitus (kushoto) na Scholastica Teffe.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni