- Ujenzi, ukarabati kufanyika kwa awamu kusogeza huduma za haki karibu na wananchi
Na HALIMA MNETE- MAHAKAMA DODOMA.
Serikali imesema inaendelea kutekeleza mpango wa ujenzi na
ukarabati wa majengo ya Mahakama nchini ili kuboresha utoaji wa huduma za haki
kwa Wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 21 Aprili, 2025 jijini Dodoma
na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba, wakati akijibu maswali
ya Wabunge katika kikao cha Bunge la Kumi na Tatu jijini Dodoma kuhusu hali ya
miundombinu ya Mahakama.
Amesema kuwa Mahakama ya Tanzania inaendelea kutekeleza
ujenzi na ukarabati wa majengo kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2025/2026,
kufuatia kuwepo kwa uhaba wa majeng,o hususan Mahakama za Mwanzo katika maeneo
mbalimbali nchini.
Naibu Waziri ameeleza kuwa utekelezaji huo unafanyika kwa
awamu, ambapo kwa sasa Serikali inakamilisha maandalizi ya awamu ya tatu ya
mpango huo wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya mahakama.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Nanyamba, Abdallah
Chikota, alihoji kuhusu mpango wa Serikali kujenga Mahakama ya Mwanzo katika Wilaya
hiyo, huku akishauri pia kujengwa kwa nyumba za Watumishi wa Mahakama ili
kuboresha mazingira ya kazi.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri alisema kuwa ujenzi wa Mahakama
ya Mwanzo wilayani Nanyamba utazingatiwa katika mpango wa awamu ya tatu.
Aidha, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu Ado, aliuliza
swali la nyongeza akitaka kufahamu sababu za kusimama kwa ujenzi wa Mahakama ya
Wilaya hiyo kwa takribani miezi mitano na ni lini utakamilika.
Katika majibu yake, Mhe. Katimba alisema kuwa mradi huo upo
katika awamu ya pili ya utekelezaji na tayari mkandarasi yupo eneo la kazi
akiendelea na ujenzi, huku Serikali ikiwa na dhamira ya kuhakikisha Wananchi
wanapata majengo ya kisasa yatakayowezesha upatikanaji bora wa haki.
Kwa upande wake, Mbunge wa Muleba Kaskazini, Mhe. Adonis
Alfred Bitegeko, alihoji lini jengo la Mahakama ya Wilaya hiyo litaboreshwa
kutokana na changamoto ya uchakavu na ufinyu wa nafasi.
Akijibu, Naibu Waziri alisema kuwa Serikali ina mpango wa
kuboresha jengo hilo ili Wananchi wa Muleba waweze kupata huduma za mahakama
katika mazingira bora zaidi.
Naye Mbunge wa Kiteto, Mhe. Edward Ole Lekaita, aliitaka
Serikali kueleza lini ujenzi wa Mahakama ya kisasa katika Wilaya hiyo utaanza.
Katika majibu yake, Mhe. Katimba alisema kuwa tayari
mchakato wa kumpata mkandarasi umeanza baada ya kutangazwa kwa zabuni, na hatua
zilizopo sasa ni za majadiliano ya mkataba ili kuruhusu kuanza kwa ujenzi huo.
Serikali imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuhakikisha
inaboresha miundombinu ya Mahakama nchini ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa
haki na kupunguza changamoto zinazowakabili Wananchi katika kupata huduma hiyo
muhimu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni