- Jaji Mkuu abainisha hayo alipoteta na TIArb
- Asema Usuluhishi una faida lukuki ikiwemo kuokoa muda, kupunguza gharama, kujenga & kuimarisha mahusiano.....
Na MARY GWERA,
Mahakama-Dar es Salaam
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju amesema kuwa mahusiano kati ya Mahakama ya Tanzania na Taasisi za Usuluhishi nchini ni ya msingi kwakuwa kwa kufanya hivyo Mhimili huo unatekeleza takwa la kikatiba kwa mujibu wa Ibara ya 107(A)(2)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inaitaka Mahakama kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro.
Mhe. Masaju ameyasema hayo leo tarehe 01 Aprili, 2026 katika ofisi yake ndogo iliyopo Mahakama ya Rufani Tanzania jijini Dar es Salaam wakati alipotembelewa na Wajumbe wa Bodi ya Taasisi ya Wasuluhishi Tanzania (TIArb).
“Viongozi nawashukuru katika hatua hii ya kututembelea Mahakamani, katika hatua hiyohiyo ya kuimarisha mahusiano baina yetu na kama unavyoona Katiba inatupa maelekezo pamoja na kwamba sisi ndio wenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini pia tunatakiwa kukuza na kuendeleza Usuluhishi baina ya watu wanaohusika katika migogoro, kwa hiyo sisi kukutana nanyi ni sehemu pia ya utekelezaji wa maelekezo ya Katiba kwa sababu ninyi mnahusika, lakini pia tuna mahusiano haya ya kisheria kwamba mnaanza kusuluhisha halafu utekelezaji hatimaye unaishia mahakamani,” amesema Jaji Mkuu.
Hivyo, Mhe. Masaju ameeleza kuwa, mahusiano kati ya Mahakama na Taasisi zinazohusika na Usuluhishi si tu ya msingi bali pia yanapaswa kuwa endelevu.
Kuhusu masuala mtambuka yanayohusu ustawi katika utekelezaji wa jukumu la Usuluhishi, Mhe. Masaju amewashauri Viongozi wa TIArb kuzishirikisha pia Wizara za Kisekta zinazohusika na mambo hayo, mfano kuhusu mabadiliko ya Sheria ni vema kushirikisha Wizara ya Katiba na Sheria au Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama ambavyo wanaishirikisha Mahakama, kadhalika Wizara ya Mipango na Uwekezaji inayoongozwa na Mhe. Prof. Kitila Mkumbo.
Jaji Mkuu ameongeza kuwa, Mahakama inaunga mkono utekelezaji wa Usuluhishi unaofanywa na Taasisi hiyo kwa kuwa Usuluhishi una faida nyingi ikiwa ni pamoja na utatuzi wa migogoro mapema, inajenga na kuimarisha mahusiano, inapunguza matumizi ya gharama pamoja na kuokoa muda.
Katika upande mwingine,
Mhe. Masaju amewashauri Viongozi na Wafanyakazi wa Taasisi hiyo kuimarisha
uwezo wa kumudu majukumu yao (competency) kuwa
na uadilifu katika utekelezaji wa jukumu hilo muhimu sambamba na kutatua na
kumaliza migogoro mapema ipasavyo.
“Kwa upande wetu huku Mahakamani tunachukua hatua ya kurekebisha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai na yale majedwali ’ zinarekebishwa na Jaji Mkuu akishirikiana na Waziri mwenye dhamana, tutarekebisha huu mwenendo ili tuondoe vile vifungu vya kiurasimu vinavyofanya migogoro ichelewe kumalizika,” ameeleza Jaji Mkuu.
Kadhalika, Mhe. Masaju
amewaeleza viongozi hayo kuwa, “ninyi ambao mnafanya hii kazi ya Usuluhishi
mnafanya jambo jema na imeandikwa katika Kitabu cha Mathayo sura ya 5 kwamba,
heri Wapatanishi maana wataitwa Wana wa Mungu; kwa hiyo ushauri wangu ni kwamba
muifanye kazi hii kwa nia njema (passion).”
Hata hivyo, Jaji Mkuu
amewataka Viongozi hao kutoka TIArb kuitangaza Taasisi hiyo ili ijulikane na
vilevile wasisite kuishirikisha Mahakama kuhusu jambo lolote kuhusiana na suala
zima la utekelezaji wa jukumu la usuluhishi huku akiwaalika kujumuika na
Mahakama katika Wiki ya Usuluhishi nchini anayotarajia kuizindua tarehe 09
Aprili, 2026.
Kwa upande wake Makamu wa
Rais wa Taasisi wa Wasuluhishi Tanzania (TIArb), Bw. Usaje Mwambene amemueleza
Jaji Mkuu kuwa Taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 1997 lengo likiwa ni
kushughulikia migogoro ya kimkataba, kibiashara na kadhalika.
Bw. Mwambene amesema tangu kuanzishwa kwa Taasisi hiyo imekua kwa kasi na sasa ina jumla ya wajumbe 363 wakiwemo Wanasheria, Wahandisi, Wahasibu, Wafamasia na wengine na pia imejumuisha wajumbe wa kimataifa (international members) ambapo kwa sasa wapo wajumbe sita.
Ameeleza kuwa, Taasisi hiyo pia inatoa ushauri kwenye masuala ya migogoro ya kibiashara na kwamba inahusika kujenga uwezo (capacity building) kupitia mafunzo mbalimbali inayotoa kwa wajumbe waliopo na wapya.
Aidha, Makamu huyo wa
Rais wa TIArb amesema, Taasisi hiyo inaomba ushirikiano wa karibu na Mahakama
hususan katika maeneo ya kujengeana uwezo kupitia mafunzo mbalimbali,
kushirikiana katika baadhi ya matukio ya Kitaasisi ikiwemo Mkutano wa Mwaka wa
Wasuluhishi.
Mazungumzo yakiendelea....

Sehemu ya Washiriki wa Kikao wakichangia na kufuatilia kinachojiri katika mazungumzo hayo.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)












Hakuna maoni:
Chapisha Maoni