Na. CHRISTOPHER MSAGATI - Mahakama, Manyara
Kaimu
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe.
Devotha Kamuzora amejumuika na wadau wa Mahakama katika kuendesha mafunzo ya
Wiki ya Usuluhishi yakiwa na lengo la kuwajengea wadau wa haki madai uwezo wa kusuluhisha
migogoro kwa njia za upatanishi, elimu hiyo ilitolewa katika ukumbi wa wazi wa
Mahakama Kuu.
Akizungumza
wakati wa tukio hilo, Mhe. Kamuzora alieleza kuwa, usuluhishi ni silaha ambayo
inamaliza na kutatua migogoro na matatizo katika jamii kuliko hata kufika mahakamani
na kusikiliza mashauri.
“Tukiachana
na mashauri ya jinai yanayohusu makosa au uhalifu mkubwa, mashauri mengi ya
madai yanaweza kwisha kwa kutumia Suluhu ambazo tunaweza kufanya wenyewe.
Usuluhishi unasaidia sana katika kuokoa muda na gharama ambazo tunaweza kuzitumia
wakati tumefungua mashauri mahakamani,” alieleza Mhe. Kamuzora.
Akitoa
neno la utangulizi, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya
Manyara Mhe. Bernard Mpepo, aliwaasa watu wote kutumia muda wao kusikiliza
elimu ambayo itatolewa kwa sababu ni ya msingi sana na ina tija katika kutatua
migogoro mbalimbali katika jamii.
“Wananchi
wengi mnafika mahakamani kwa ajili ya kutatua migogoro ambayo kimsingi mngeweza
kuimaliza wenyewe kwa sababu mmekosa elimu hii ya usuluhishi. Hivyo, ninawasihi
sana msikilize kwa makini yale ambayo yatakuwa yanafundishwa na wataalamu wetu,”
alisema Mhe. Mpepo.
Naye,
Wakili wa Kujitegemea Bw. Kuyengwa Ndonjekwa alisema kuwa, elimu hiyo ni muhimu
sana kuendelea kutolewa mara kwa mara kwa sababu ina madhumuni ya kupunguza
mzigo mkubwa kwa Mahakama wa kusikiliza mashauri na kuwafanya wananchi wapatane
wenyewe kuliko kuendelea kuleta mashauri mahakamani hususan kwa masuala ambayo
yanaweza kuzungumzika na suluhu ikapatikana.
Kwa
upande wake mdau wa Mahakama Bw. Gwandu Nada ambaye ni mwananchi kutoka katika
Wilaya ya Babati aliushukuru uongozi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara kufanya
elimu hiyo ya upatanishi kuwa endelevu kwani itaisaidia jamii kuokoa muda wa kwenda
mahakamani kutatua migogoro isiyokuwa na tija.
“Mafunzo
haya ni mazuri kwa kuwa yamenifundisha kupatana na washtaki wangu mapema kabla
ya kufikishana katika vyombo vya sheria na ninaahidi kwenda kupatana na wale
ambao nimekosana nao kwa njia ya usuluhishi,” alisema Bw. Nada.
Waliohudhuria
kupata elimu hiyo ni wadau wa Mahakama pamoja na wadaawa waliofika kwa ajili ya
kupata mafunzo ya usuluhishi, Watumishi wa Mahakama Kuu Manyara, Mawakili wa
Serikali, Mawakili wa Kujitegemea, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, Mwakilishi
kutoka Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Ofisi ya Ustawi wa Jamii pamoja
na baadhi ya wananchi.
Kaimu
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe.
Devotha Kamuzora akitoa neno wakati wa utoaji elimu ya Usuluhishi iliyofanyika
katika ukumbi wa Mahakama Kuu. Kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala
Ndogo ya Manyara Mhe. Bernard Mpepo na kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara Mhe. Mariam Lusewa.
Afisa
Huduma kwa Jamii Mkoa wa Manyara Bw. Tumaini Moshi akitoa elimu ya usuluhishi
kwa wananchi waliofika Mahakama Kuu Manyara kupata elimu hiyo.
Mwananchi
wa Wilaya ya Babati akitoa maoni yake wakati wa mafunzo elimu ya Wiki ya
usuluhishi yaliyofanyika katika Ukumbi wa wazi wa Mahakama Kuu Manyara.
Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati Mhe. Victor Kimario akitoa elimu
ya usuluhishi kwa wananchi waliofika Mahakama Kuu Manyara kupata elimu hiyo.
Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Bernard Mpepo kushoto
akizungumza na mmoja wa Wananchi waliofika kupata elimu ya upatanisho kwenye
maadhimisho ya Wiki ya Usuluhishi.
Sehemu
ya wananchi waliohudhuria mafunzo ya wiki ya usuluhishi wakiwa katika picha ya
Pamoja na Meza Kuu wakati wa utoaji elimu ya Wiki ya usuluhishi iliyofanyika
katika Ukumbi wa wazi wa Mahakama Kuu Manyara.
(Habari Hii imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni