Na ARAPHA RUSHEKE, Mahakama Kuu, Dodoma.
Mahakimu na Mawakili
wa Mkoa wa Dodoma wameendelea kupatiwa elimu muhimu kuhusu utatuzi wa migogoro
kwa njia ya usuluhishi, hatua inayozidi kuimarisha mifumo ya haki na kuongeza
ufanisi katika utoaji wa huduma za kisheria nchini.
Mafunzo hayo
yaliyofanyika jana tarehe 15 Aprili, 2026 katika ukumbi wa Mahakama Kuu Dodoma kwenye
Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) yamewakutanisha Wadau mbalimbali wa sekta
ya sheria.
Lengo la mafunzo hay
oni kujengeana uelewa wa kina kuhusu matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa
migogoro (ADR), njia inayozidi kupata nafasi kubwa katika kuhakikisha haki
inapatikana kwa haraka na kwa gharama nafuu.
Akitoa neno la
ukaribisho, Naibu Msajili wa Mahakaa Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Upendo
Ngitiri, aliwahimiza washiriki kutumia ipasavyo jukwaa hilo muhimu kujifunza,
kubadilishana uzoefu na kuimarisha weledi wao katika kushughulikia migogoro ya Wananchi.
Mafunzo hayo
yaliendeshwa chini ya uratibu mahiri wa Jaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Dkt.
Fatma Khalfan, ambaye ameendelea kuonesha uongozi thabiti, weledi wa hali ya
juu pamoja na dhamira ya dhati ya kuendeleza usuluhishi nchini.
Kupitia jitihada zake,
Wadau wa Sheria wameendelea kunufaika na elimu yenye tija, huku akihamasisha
kwa vitendo matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro kama suluhisho
endelevu.
Mada mbalimbali
ziliwasilishwa wakati wa mafunzo hayo na wataalamu wa sheria, akiwemo Mhe.
Thurstone Kombe, Mhe. Sarah Mwalilino, Mhe. Judith Barigenge pamoja na wengine kutoka
Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi nyingine kama CHRAGG.
Mada hizo zilieleza
kwa kina umuhimu wa usuluhishi katika kupunguza migogoro, kuokoa muda na
gharama, pamoja na kuimarisha mahusiano katika jamii.
Akisimamia
majadiliano, Mhe. Dkt. Khalfan
alisisitiza kuwa usuluhishi si tu njia mbadala, bali ni nyenzo muhimu ya
kujenga jamii yenye amani na mshikamano, huku akitoa wito kwa Wadau wa Sheria
kuendelea kuipa kipaumbele.
Washiriki walipata
nafasi ya kuuliza maswali na kuchangia hoja mbalimbali, hali iliyoonesha
mwitikio mkubwa na uhitaji wa elimu hiyo katika jamii ya Wanasheria.
Akitoa neno la
shukrani, Mhe. Zabibu Mpangule aliwashukuru waandaaji pamoja na washiriki wote
kwa ushiriki wao, akibainisha kuwa mafunzo hayo yameongeza thamani kubwa katika
utendaji wao wa kila siku.
Mafunzo hayo yalihitimishwa
kwa hotuba ya kufunga kutoka kwa Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Katiba na
Sheria, aliyesisitiza umuhimu wa kuendeleza elimu ya usuluhishi ili kuhakikisha
Wananchi wanapata haki kwa wakati, kwa ufanisi na kwa amani.
Kwa ujumla, tukio hili limeacha alama kubwa katika Mkoa wa Dodoma, likiwa ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kuifanya Tanzania kuwa kinara wa matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro.
Meza
Kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, ambaye pia ni Mratibu
wa Usuluhishi wa Wiki ya Usuluhishi, Mhe. Dkt.Fatma Khalfan (katikati). Kushoto kwake ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo
Dodoma, Mhe. Upendo Ngitiri na kulia kwake ni Mkurugenzi Msaidizi Kurugenzi ya Usuluhishi(ADR)
Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Felix Chakila.
Mahakimu
pamoja na Mawakili mbalimbali waliohudhuria elimu hiyo ya usuluhishi katika
ukumbi uliopo Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma wakifuatilia kwa makini
mafunzo hayo.
Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Upendo Ngitiri, akitoa neno
la ukaribisho kwa wajumbe hao waliohudhuria elimu ya usuluhishi kwa Mahakimu na
Mawakili.
Meza
Kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, ambaye pia ni Mratibu
wa Usuluhishi wa Wiki ya Usuluhishi, Mhe. Dkt.Fatma Khalfan (katikati) akiwa
katika picha ya pamoja na baadhi ya Mahakimu wa Dodoma walioshiriki mafunzo ya
Mahakimu pamoja na Mawakili kuhusu usuluhishi. Kushoto kwake ni Naibu Msajili
wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Upendo Ngitiri na kulia kwake ni Mkurugenzi
Msaidizi Kurugenzi ya Usuluhishi(ADR) Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Felix
Chakila.
Jaji
wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, ambaye pia ni Mratibu wa Usuluhishi wa Wiki
ya Usuluhishi, Mhe. Dkt. Fatma Khalfan (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya
pamoja na watoa ujumbe maalumu kuhusu elimu ya usuluhish,i ambao pia ni Watumishi
wa Mahakama Dodoma wakati wa mafunzo hayo.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, ambaye pia ni Mratibu wa Usuluhishi wa Wiki ya Usuluhishi, Mhe. Dkt.Fatma Khalfan (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe walioshiriki mafunzo ya Mahakimu pamoja na Mawakili kuhusu usuluhishi.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni