Alhamisi, 16 Aprili 2026

MAHAKAMA MOROGORO YAFANYA KIKAO CHA KUSUKUMA MASHAURI YA JINAI, MADAI

Na ASHA JUMA -Mahakama, Morogoro

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Morogoro, imefanya kikao cha robo ya kwanza ya mwaka 2026, chenye lengo la kujadili na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji kazi, hususan katika kusukuma mashauri ya jinai na madai.

Kikao hicho kilichofanyika jana tarehe 15 Aprili, 2026, katika ukumbi mkubwa wa mikutano uliopo Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Morogoro ni sehemu ya vikao vya kitaasisi vinavyolenga kuongeza ufanisi wa utoaji haki na kupunguza ucheleweshaji wa mashauri mahakamani.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Morogoro, Mhe. Rose Ebrahim, aliongoza kikao hicho kiichowahusisha Wadau mbalimbali wa mnyororo wa haki, wakiwemo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Amiri Msumi, Mtendaji wa Mahakama Kuu Morogoro, Bw. Ahmed Ng’eni na Mahakimu.

Wengine walitoka Ofisi ya Mawakili wa Serikali, Chama cha Wanasheria wa Kujitegemea, Ofisi ya Baraza la Ardhi na Nyumba, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, Wasaidizi wa Sheria wa Majaji pamoja na Ofisi za Madalali.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Msumi alipongeza juhudi za Mahakama na Wadau wote kwa ushirikiano wao katika kutekeleza majukumu ya kila siku.

Alieleza hali ya mashauri kwa robo ya kwanza ya mwaka 2026, akisisitiza kuwa bado kuna haja ya kuongeza juhudi zaidi, hususan katika mashauri ya rufaa za madai ambayo yanahitaji msukumo wa ziada.

Mhe. Msumi alibainisha baadhi ya changamoto zinazosababisha ucheleweshaji wa mashauri, ikiwemo kuchelewa kuwasilishwa kwa kumbukumbu kutoka Mahakama za chini, hasa Baraza la Ardhi na Nyumba.

Alieleza kuwa hali hiyo hupunguza kasi ya usikilizaji wa mashauri na hivyo kuathiri utoaji wa haki kwa wakati.

Ili kukabiliana na changamoto hizo, Mhe. Msumi aliainisha mikakati mbalimbali, ikiwemo kusimamia kwa ukaribu hatua zote za awali za maandalizi ya mashauri, kuhakikisha zinazingatia muda uliowekwa kisheria, pamoja na kupanga na kuamua maombi na mapingamizi kwa wakati.

Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mawasiliano na Mahakama ya Rufani ili kusaidia kusikiliza na kumaliza mashauri kwa ufanisi, pamoja na kuhakikisha ufuatiliaji wa karibu wa mashauri yote.

“Mikakati hii pamoja na changamoto hizi inabidi tuzifanyie kazi haraka iwezekanavyo kwa sababu tunashughulika na haki za watu,” alisisitiza Mhe. Msumi.

Kwa upande wao, Wadau waliohudhuria kikao hicho waliipongeza Mahakama kwa hatua ya kutumia mifumo ya kidijitali katika uendeshaji wa mashauri, wakieleza kuwa hatua hiyo imeongeza kasi na uwazi katika utoaji wa huduma za haki.

Baadhi ya Taasisi pia zimeanza kutumia mifumo hiyo ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia yanayoletwa na Mahakama.

Akihitimisha kikao hicho, Jaji Mfawidhi alipendekeza kuwepo kwa mafunzo ya muda mfupi kati ya Mahakama na Wadau wa sekta ya haki ili kusaidia kuongeza ufanisi katika utoaji haki, kuboresha ubora wa maamuzi, kuimarisha ushirikiano, pamoja na kupunguza makosa ya kisheria.

“Elimu hii itasaidia kung’amua vitu gani tunaweza kusaidiana na kujadiliana pamoja na kubadilishana ujuzi,” alisema Mhe. Ebrahim.

Kwa ujumla, kikao hicho kimeweka msingi imara wa kuboresha utendaji wa Mahakama Kuu Morogoro kwa kushirikiana na Wadau wake, kwa lengo la kuhakikisha haki inatolewa kwa wakati na kwa ufanisi zaidi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Morogoro, Mhe. Rose Ebrahim, akiongoza kikao hicho.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Morogoro, Mhe. Amiri Msumi, akisoma taarifa yake katika kikao hicho.

Picha mbalimbali za wajumbe katika kikao hicho.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni