Na. SHARIFU MOKIWA-Mahakama, Sumbawanga
Mahakama
Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Sumbawanga imeungana na Masjala nyingine
nchini kuadhimisha Wiki ya Usuluhishi iliyoanza tarehe 13 Aprili, 2026 kwa
kutoa elimu kwa wananchi wanaotembelea mabanda yaliyowekwa Mahakama Kuu
Sumbawanga na Ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sumbawanga ili kupata elimu ya utatuzi wa migogoro
kwa njia ya upatanishi ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utoaji wa haki.
Aidha,
wiki usuluhishi inatumia kaulimbiu isemayo “kutumia
njia mbadala ya utatuzi wa migogoro kama mbinu inayo pendelewa ya kutatua
migogoro nchini Tanzania” kaulimbiu hiyo inasisitiza dhamira ya Mahakama kuhamasisha
jamii kutumia njia za usuluhishi katika kutatua migogoro kwa amani.
Akitoa
elimu ya usuluhishi Jaji Mfawidhi wa Mahakama wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya
Sumbawanga Mhe.Frederick Manyanda akizungumzia umuhimu wa usuluhishi alisisitiza
kuwa ni vyema kufanya usuluhishi kwa sababu unaweza kupoteza kila kitu kwa hoja
za kiutaratibu na kisheria lakini ni faida zaidi pale unapokubali kumaliza
mgogoro nje ya Mahakama kwa upatanishi.
Kwa
upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe.
Pamela Mazengo aliwahakikishia wananchi kuhusu nguvu ya kisheria ya makubaliano
ya usuluhishi baina ya pande zenye mgogoro.
“Tuwatoe
hofu kuwa, makubaliano ya usuluhishi yana nguvu ya kisheria na yanaweza
kutekelezwa kama ilivyo kwa uamuzi wa Mahakama hivyo yale mtakayokubaliana yana
thamani na uhalali wa kisheria,” alisisitiza Mhe. Mazengo
Naye,
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Rukwa Mhe. Kisasila
Saguda akitoa elimu hiyo alisema kuwa, usuluhishi hutoa fursa ya kumaliza
mgogoro kwa amani bila kuwepo mshindi au mshindwa, “usuluhishi husaidia
kumaliza jambo kwa amani bila kuwa na mshindi wala mshindwa wote mnakuwa
washindi kwasababu mmemaliza mgogoro wenu kwa maelewano,” alisema.
Akifafanua
sehemu ya mambo Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Sumbawanga Mhe. Yusuph Sakara
alisisitiza umuhimu wa usuluhishi katika kujenga maendeleo ya kiuchumi, kisiasa
na kijamii ili kuboresha ustawi wa wananchi.
“Tunataka
jamii ipige hatua kimaendeleo, hatuwezi kupiga hatua hiyo kama tunahudhuria mahakamani
siku nzima, hatuwezi kuwa na maendeleo tukiwaza tumerundika mashauri
mahakamani. Usuluhishi ni jambo jema ukifanyika kwa haraka watu wanapata muda
wa kwenda kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo,” amesema Mhe. Sankara
Hivyo
Mahakama inawahimiza wananchi kujitokeza kushiriki katika wiki ya usuluhishi ili
kutatua migogoro kwa njia ya upatanishi, amani na kwa wakati hali itayakayo
chochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Katika
zoezi hilo Wasuluhishi na Wapatanishi walioteuliwa walipata wasaa wa
kushughulikia sehemu ya migogoro iliyowasilishwa na wadau baada ya kupata elimu
miongoni mwa migogoro iliyoshughulikiwa ni pamoja na migogoro ya kifamilia,
kama vile ndoa ambapo pande husika zilipata fursa ya kusikilizana na kuelekezwa
namna ya kufikia makubaliano bila ya kuendelea na mchakato wa kesi mahakamani.
Vilevile
zoezi la kutoa elimu ya usuluhishi linaendelea katika Mahakama ya Wilaya
Kalambo na Mahakama ya Wilaya Nkasi zilizopo Mkoa wa Rukwa.
Jaji
Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Frederick Manyanda
akieleza umuhimu wa usuluhishi wakati akitoa elimu kwa wananchi wakati wa
kuadhimisha wiki ya usuluhishi nchini.
Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Pamela Mazengo
akizungumza na wananchi waliojitokeza kupata elimu ya usuluhishi.
Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Rukwa Mhe. Kisasila Saguda akitoa
elimu ya usuluhishi kwa wananchi.
Wananchi
wakisikiliza kwa makini elimu ya usuluhishi iliyokuwa inatolewa na Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Rukwa Mhe. Kisasila Saguda (hayupo pichani)
Msaidizi
wa Kumbukumbu Bw. Fredrick Mushi akisulusha wananchi walioamua kumaliza mgogoro
wao kwa njia ya usuluhishi.
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Sumbawanga Mjini Mhe.Yusuph Sakara akitoa elimu kuhusu umuhimu wa usuluhishi katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Rukwa
Wananchi
wakisikiliza kwa makini elimu ya usuluhishi iliyokuwa inatolewa na Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Rukwa Mhe. Kisasila Saguda
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni