Alhamisi, 16 Aprili 2026

JAJI MFAWIDHI SONGWE ATOA ELIMU YA USUHUHISHI KWA WADAU

Na. ELIUD KIWANGA – Mahakama Songwe

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Gabriel Malata, ametoa elimu ya usuhuhishi kwa wadau mbalimbali wa Mahakama katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe ikiwa ni siku ya kwanza ya kuadhimisha Wiki ya Usuluhishi nchini.

Mhe. Malata alisema kuwa, katika pande mbili zenye migogoro husuluhishwa na upande wa tatu wa mtu anayejulikana kama msuluhishi ambapo msuluhishi huyo anaweza kuwa mtu yeyote, Mchungaji, Sheikh, Baraza la Wazee, Baraza la Kata, au Chombo kingine chochote cha usuluhishi.

Mhe. Malata aliongeza kuwa, usuluhishi unapaswa kutumika kama njia mbadala ili kutatua migogogoro katika familia, migogoro ya kibiashara, migogoro mahali pa kazi na migogoro ya kijamii na pia njia hii imerasimishwa kikatiba, kisheria kikanuni, kimila na desturi, na kwamba siyo Tanzania pekee, usuluhishi pia hutumika kutatua migogoro mbalimbali ya kimataifa. 

Aidha, Mhe. Malata alieleza faida za kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi na kusema kupitia usuluhishi unaokoa gharama na muda kwani usuluhishi huchukua mda mfupi kuliko kesi mahakamani na pia gharama zake ni ndogo ukilinganisha na ada za mahakamani na mawakili.

Vilevile, usuluhishi humaliza migogoro mapema bila kuchelewa hivyo kupunguza msongamano wa kesi mahakamani na kupitia usuluhishi wahusika huzungumza kwa amani na kuelewana hivyo husaidia kudumisha urafiki, undugu na ushirikiano.

Mhe. Malata alisisitiza suala la msamaha kwani kusamehe ni agizo kutoka kwa Mungu, kuto kufanya hivyo ni kwenda kinyume na agizo la Mungu, kwani migogoro haipendezi katika jamii na sio lazima kila mgogoro umalizwe na msuluhishi au kupelekwa kwenye vyombo vya sheria kwa kufanya hivyo huongeza gharama zisizo na misingi.

Mhe. Malata aliwasisitiza viongozi wa Dini waendelee kudumisha upendo, umoja na mshikamano baina ya waumini wao ili waishi kwa upendo na pia aliwakumbusha viongozi hao kuwa wana wajibu wa kuchunga kondoo wao vizuri kwani hilo ni jukumu lao walilopewa na Mungu ili kuepusha migogoro ambayo inaweza kutokea katika jamii.

Aidha, aliwaasa wadau wa usuluhishi kuwa waipokee njia ya usuluhishi na kutoa elimu kwa wanajamii wote kuhusu usuluhishi kama njia mbadala ya kutatua migogoro baina ya pande mbili na pia jamii itambue kuwa usuluhishi au upatanishi ni jambo ambalo lipo kwa mujibu wa dini zetu, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kisheria na pia hata katika mila na desturi zetu.

Mhe. Malata aliwashukuru wajumbe kwa kuhudhuria kikao hicho na pia aliwashukuru kwa michango yao mizuri yenye kujenga amani, upendeo na ushirikiano katika jamii.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Gabriel Malata, akitoa elimu ya usuhuhishi kwa wadau mbalimbali wa Mahakama (hawapo pichani) ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha wiki ya usuluhishi nchini.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songwe Bw. Sostenes Mayoka (kulia) akiwa katika kikao hicho cha wiki ya usuluhishi nchini.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Joyce Minde akifuatilia elimu ya Usuluhishi.

Sehemu ya Wadau waalikwa wakisikiliza kwa makini wakati Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Gabriel Malata (hayupo pichani) akitoa elimu ya usuluhishi.


Sehemu ya Wadau waalikwa wakisikiliza kwa makini wakati Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Gabriel Malata (hayupo pichani) akitoa elimu ya usuluhishi.

(Habari Hii imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni