Na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 26 Aprili, 2026 amehudhuria Ibada maalum ya shukrani ya kusherehekea kumbukizi ya miaka 80 ya kuzaliwa kwa Bi. Loyce Nyalali, Mjane wa Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Marehemu Francis Nyalali.
Ibada hiyo maalum ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai imefanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro Oysterbay jijini Dar es Salaam ikiongozwa na Paroko wa Kanisa hilo, Padri Bartholomew Mrosso na Padri mwenzake.
Katika mahubiri yake wakati wa ibada hiyo, Padri Mrosso ametoa rai kwa Waumini kumshukuru Mungu kwa uzima kwa kuwa uzima ni zawadi kubwa ambayo kwayo yatupasa kumshukuru Mungu. Amesisitiza kwa kusema, “tumshukuru Mungu kwa uzima kwanza halafu vingine ndio vifuate.”
Kadhalika Padri huyo, amewakumbusha Viongozi kusimamia haki, na kutenda mema kwa walio chini yao na wanaowaongoza.
“Katika Injili ya Jumapili ya leo ya Mchungaji Mwema msingi wake ni Uongozi, namna fulani ya Uongozi ambao Kristo anaudhihirisha kupitia matendo yake mema,” ameeleza.
Ameongeza kuwa, Kiongozi anapaswa kusimama kwa ajili ya wale anaowaongoza hivyo, Uongozi usichukuliwe kama ajira bali kujitoa na kuwajali watu waliopo chini.
Ibada hiyo imehudhuriwa pia na baadhi ya Viongozi wakiwemo Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Joseph Sinde Warioba, Majaji Wastaafu wa Mahakama Rufani na Mahakama Kuu, Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Wakili Tom Nyanduga, Wenza wa Majaji Wakuu Wastaafu akiwemo Mama Marina Juma, Mama Sada Chande pamoja na ndugu, jamaa na marafiki na wageni wengine waalikwa.
Baada ya ibada hiyo, imefanyika sherehe maalum ya kumpongeza Bi. Loye Nyalali iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Kadinali Rugambwa uliopo pembeni ya Kanisa la Mt. Petro jijini Dar es Salaam.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (wa pili kushoto mwenye tai nyekundu) akiwa katika misa ya shukrani ya kusherehekea kumbukizi ya miaka 80 ya kuzaliwa kwa Bi. Loyce Nyalali, Mjane wa Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, marehemu Francis Nyalali. Ibada hiyo imefanyika leo tarehe 26 Aprili, 2026 katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro jijini Dar es Salaam. Kulia kwa Jaji Mkuu ni Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Joseph Sinde Warioba na aliyeketi mbele ni Mama Loyce Nyalali anayeadhimisha miaka 80 ya kuzaliwa kwake.
(Picha na MARY GWERA, Mahakama)



























Hakuna maoni:
Chapisha Maoni