Jumapili, 26 Aprili 2026

WATUMISHI WA MAHAKAMA KIGOMA WAKUMBUSHWA KUZINGATIA MATUMIZI YA OFISI MTANDAO

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Mkurugenzi wa Kumbukumbu na Nyaraka Mahakama ya Tanzania, Bw. Malimo Manyambula amewasisitiza Watumishi wa Mahakama Kigoma juu ya matumizi ya Ofisi mtandao na kuongeza weledi wa matumizi ya mfumo huo ili kuendana na kasi ya maboresho ya Mahakama. 

Bw. Manyambula alisema hayo tarehe 23 Aprili, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano Mahakama Kuu Kigoma akiwa katika ziara yake ya ukaguzi wa Masjala za Mahakama katika eneo la utunzaji wa kumbukumbu, nyaraka na taarifa zinazozalishwa kila siku katika shughuli zote za Mahakama.

“Watumishi wenzangu nipo kwenye ukaguzi wa kawaida kufahamu changamoto zenu na kuwapongeza pale panapostahili kupongezwa na zaidi kuwasisitiza kuendelea kutumia mifumo hii kwa ufasaha ili kuweza kuhifadhi nyaraka zetu katika mifumo yetu bila kufanya shughuli zetu nje ya mifumo yetu, hata hivyo Kanda ya Kigoma mnafanya vizuri muendelee kufanya hivyo ili mbaki vinara wa matumizi mazuri ya Ofisi mtandao,” alisema Mkurugenzi huyo.

Alieleza kuwa, Kurugenzi ya Usimamizi wa Kumbukumbu na Nyaraka Mahakama ya Tanzania inaendelea na usimamizi mzuri wa Ofisi mtandao kuhakikisha Idara zote zilizopo Mahakamani zinatunza kumbukumbu na nyaraka katika mifumo na mpangilio uliokubalika katika viwango vya utunzaji wa nyaraka pamoja na maelekezo yanayoelekezwa katika miongozo mbalimbali ya utunzaji wa kumbukumbu katika Masjala.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Yusuph Mhoja alimshukuru Mkurugenzi huyo kwa niaba ya watumishi wa Kanda ya Kigoma, kwa ukaguzi wake kwani ndio unaoleta chachu ya kuwa bora zaidi na maelekezo aliyoyatoa ameahidi kuyasimamia ili Mahakama Kuu Kigoma iendelee kuwa kinara katika matumizi bora na sahihi ya Ofisi Mtandao (e-Office).

Aidha, wajumbe waliohudhuria kikao cha kuhitimisha ukaguzi wa utunzaji wa kumbukumbu katika Mahakama hiyo ni Maofisa na Wakuu wa Vitengo pamoja watumishi wanaotumia mfumo huo pamoja na Watunza Kumbukumbu na Nyaraka wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma.

Mkurugenzi wa Kumbukumbu na Nyaraka Mahakama ya Tanzania, Bw. Malimo Manyambula akisisitiza jambo kwa watumishi wa Mahakama Kuu Kigoma alipokuwa akitoa tathmini fupi ya ukaguzi wake.


Mkurugenzi wa Usimamizi wa Kumbukumbu na Nyaraka- Mahakama ya Tanzania, Bw. Malimo Manyambula akisaini katika kitabu cha wageni  alipowasili katika Ofisi ya Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo.


Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo(katikati) akiwa katika maongezi na mgeni wake Mkurugenzi wa Usimamizi wa Kumbukumbu na Nyaraka Mahakama ya Tanzania, Bw. Malimo Manyambula (wa pili kushoto). Kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Yusuph Mhoja na wa kwanza kushoto ni Ofisa Kumbukumbu kutoka Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Bw. Kelvin Mayala wakiwa katika mazungumzo mara baada ya kuwasili Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.
Sehemu ya watumishi waliohudhuria kikao cha tathmini ya ukaguzi wa Mfumo wa Ofisi mtandao ya Mahakama wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi wa Usimamizi wa Kumbukumbu na Nyaraka Mahakama ya Tanzania, Bw. Malimo Manyambula (aliyesimama).

 Mkurugenzi wa 
Idara ya Usimamizi wa Kumbukumbu na Nyaraka Mahakama ya Tanzania, Bw. Malimo Manyambula (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Ofisa Utumishi Mwandamizi, Bw. Festo Sanga (kulia) na Ofisa Kumbukumbu,  Bw. Kelvin Mayala.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni