Jumatatu, 13 Aprili 2026

TUMIENI UJUZI MTAKAOUPATA KUPUNGUZA MLUNDIKANO WA MASHAURI MAHAKAMANI: JAJI RWIZILE

Na FESTO SANGA, Mahakama-Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile amewataka washiriki wa mafunzo ya Usuluhishi kwa Maofisa wa Mahakama wa Kanda za Kigoma, Bukoba, Musoma na Mwanza kutumia ujuzi watakaoupata kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani.

Mhe. Rwizile ameyasema hayo leo tarehe 13 Aprili, 2026 mkoani Kigoma wakati akifungua mafunzo ya usuluhishi yatakayoendeshwa kwa siku tano na kuhudhuriwa na washiriki 16. 

“Tumieni mbinu za usuluhishi kama njia ya utatuzi wa migogoro ili kuongeza ufanisi, kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani, na kuboresha upatikanaji wa haki kwa wananchi” alisema Jaji Rwizile

Aliongeza kuwa, mafunzo hayo ni mwendelezo wa Mafunzo ya Msingi ya Usuluhishi na Mafunzo ya Wakufunzi (ToT) yaliyofanyika mwaka 2025, yaliyowawezesha Maofisa Mahakama kupata mafunzo ya kina kutoka kwa wataalamu wa usuluhishi kutoka Ujerumani kwa lengo la kuandaa wakufunzi wa ndani watakaosambaza ujuzi huo.

Alibainisha kuwa, mafunzo kama hayo tayari yamefanyika Arusha, Dodoma, Dar es Salaam na Mbeya, huku Kigoma ikiwa hatua ya mwisho ya utekelezaji wa awamu hii, inayotarajiwa kuwafikia takribani washiriki 80.

Aidha, alifafanua kwamba, mafunzo hayo yanafanyika sambamba na Wiki ya Usuluhishi Kitaifa, na kueleza kufurahishwa na ushiriki wa washiriki katika Wiki ya Utatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala, akisisitiza kuwa fursa hiyo itaongeza uelewa wa vitendo, kuimarisha upatikanaji wa haki na kuchangia moja kwa moja katika kuongeza ufanisi wa Mahakama, sambamba na kuakisi dhamira ya Mahakama katika kuendeleza mifumo ya utatuzi wa migogoro na kuboresha huduma za haki kwa wananchi.

Naye Hakimu Mkazi na Mratibu wa Mafunzo kutoka Chuo Cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Husna Rweikiza  akizungumza kwa niaba ya Mhe.Dkt. Paul Kihwelo, Jaji wa Rufani na Mkuu wa Chuo alibainisha dhamira thabiti ya Chuo hicho katika kujenga na kuendeleza uwezo wa Maofisa wa Mahakama katika maeneo mbalimbali, ikiwemo usuluhishi, kama sehemu ya juhudi za kuimarisha ufanisi na upatikanaji wa haki.

Kwa upande wake, Bi. Rose Nyatega kutoka Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ Tanzania) alieleza kuwa, mafunzo hayo yanaendeleza mpango ulioanzishwa mwaka 2025, ambapo kundi la Majaji na Mahakimu waliopatiwa mafunzo liliundwa kupitia ufadhili wa GIZ Tanzania chini ya mradi wa PROLA, pamoja na kuendelea kuimarisha ushirikiano na IJA pamoja na Mahakama ya Tanzania katika kuboresha mifumo ya utoaji haki kupitia programu za mafunzo na matumizi ya mbinu mbadala za utatuzi wa migogoro.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ Tanzania), Wawezeshaji wa Mafunzo hayo ya Usuluhishi ni Mhe. Rwizile ,Jaji Mfawidhi Kigoma na Mhe. Fadhili Yohana Mbelwa, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kigoma.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile akifungua mafunzo ya Usuluhishi leo tarehe 13 Aprili, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama Kigoma.

Hakimu Mkazi na Mratibu wa Mafunzo kutoka Chuo Cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Husna Rweikiza akifurahia jambo na washiriki wa mafunzo ya Usuluhishi (hawapo katika picha). 

Sehemu ya washiriki wa Mafunzo wakimsikiliza kwa makini Mgeni Rasmi ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (hayupo katika picha).

Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ  Tanzania), Bi. Rose Nyatega akielezea mpango wa mafunzo ya Usuluhishi.

Washiriki wa mafunzo wakiwa katika majadiliano ya mbinu za Usuluhishi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya Usuluhishi.  Wa pili kushoto ni Naibu Msajili Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigomawa pili kushoto ni Bi. Rose Nyatega kutoka Shirika la Maendeleo la Ujerumani, wa kwanza kulia ni Mhe Aristrida Tarimo  na wa kwanza  kushoto ni Mhe. Husna Rweikiza, Hakimu Mkazi na Mratibu wa Mafunzo kutoka IJA.

(Habari hii imehaririwa na HABIBA MBARUKU, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni