Jumatatu, 27 Aprili 2026

WATUMISHI MAHAKAMA KUU DODOMA WALIPATIWA ELIMU KUHUSU AFYA YA AKILI

Na ARAPHA RUSHEKE-Mahakama Kuu, Dodoma.

Watumishi wa Mahakama Kuu Dodoma, hivi karibuni walipatiwa elimu muhimu kuhusu afya ya akili na ustawi wa maisha, iliyogusa moja kwa moja maisha yao ya kazini na nyumbani.

Elimu hiyo ilitolewa katika Ukumbi wa Mikutano kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma na Jaji wa Mahakama Kuu kutoka Masjala Ndogo Dar es Salaam, Mhe. David Ngunyale.

Mbali na majukumu yake ya kusikiliza mashauri mkoani Dodoma, Mhe. Ngunyale aliona vyema kutumia nafasi hiyo kuwajengea uelewa Watumishi hao kwenye eneo hilo.

Kabla ya kuanza zoezi hilo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo, alimpongeza Jaji Ngunyale kwa moyo wa kujitoa na upendo wa dhati aliouonesha kwa Watumishi hao, akisisitiza kuwa afya ya akili ni msingi muhimu wa utendaji bora na maisha yenye mafanikio.

Kupitia elimu hiyo, Watumishi walipata fursa ya kujifunza kwa kina viashiria vya afya ya akili, mbinu za kukabiliana na changamoto za kisaikolojia pamoja na namna ya kujijenga kiakili na kitaaluma.

Si hivyo tu, mada ya uongozi bora (leading skills) iliyotolewa wakati wa zoezi hilo la utoaji elimu iliongeza chachu mpya kwa washiriki wengi, ikiwapa mwanga wa kuwa Viongozi bora katika nafasi zao na katika jamii.

Kilichovutia zaidi ni namna atumishi walivyoshiriki kwa hamasa kubwa, wakionesha wazi kufurahishwa na elimu hiyo ambayo waliieleza kuwa imewafungua macho na kuwapa mwelekeo mpya wa maisha.

Walimshukuru Jaji Ngunyale kwa kuwapatia maarifa yenye tija na yenye kugusa uhalisia wa maisha yao ya kila siku.

Zoezi hilo lilihudhuriwa na Watumishi mbalimbali ana kwa ana wakiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Dkt Fatma Khalfan, pamoja na wengine waliounganishwa kwa njia ya mtandao kutoka wilayani, jambo lililoongeza ushirikishwaji na kuifanya elimu hiyo kuwafikia wengi zaidi kwa wakati mmoja.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Dkt Juliana Masabo (aliyesimama) akimkaribisha Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, Mhe. David Ngunyale, aliyepo kulia kwake, ili kuwapa elimu Watumishi wa Mahakama Kuu Dodoma. Kushoto kwake ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Bw. Bedson Mariba.



Watumishi wa Mahakama Kuu Dodoma wakiskiliza kwa makini elimu ya Afya ya Akili kutoka kwa Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, Mhe. David Ngunyale (hayupo pichani).


 Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, Mhe. David Ngunyale akitoa somo kuhusu afya ya akili kwa Watumishi wa Mahakama Kuu Dodoma.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Simiyu.

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni