Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Mkutubi wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Rwechungura Achiles ametembelea Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma kuona hali ya huduma za Maktaba zinavyotolewa pamoja na kutoa elimu kuhusu matumizi ya Mfumo wa Taarifa za Maamuzi, Sheria na Kanuni za Tanzania (TanzLII).
Akitoa elimu ya matumizi ya mfumo wa TanzLII, tarehe 30 Machi, 2026, kwenye ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Kigoma, Bw. Achiles aliwapitisha vema Watunza Kumbukumbu na Msaidizi wa Jaji, ambao ndio wahusika wakuu wa kupandisha nyaraka katika mfumo huo.
“Mfumo huu ni rahisi kutumia ni maktaba mtandao inayotoa fursa kwa wananchi na wadau wa Mahakama kujipatia nyaraka za maamuzi ya Majaji kutoka Kanda zote za Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na Mahakama ya Rufaa, vilevile wanapata kusoma Gazeti la Serikali, Sheria na Kanuni, hotuba za Viongozi wa Mahakama na machapisho mbalimbali ya elimu kwa umma juu ya uboreshaji wa huduma zinazotolewa na Mahakama ya Tanzania katika Kanda na Mikoa yote nchini,” alisema Mkutubi huyo.
Aliongeza kwa kusema kuwa, “Kigoma mnafanya vizuri katika upandishaji wa hukumu na maamuzi ya Majaji, nitawaongezea ujuzi kidogo hasa katika eneo la urekebishaji wa taarifa za nyaraka uliyopandisha kwa ajili ya wasomaji na wapakuwaji wa nyaraka hizo katika mfumo wetu wa TanzLII.”
Kwa upande wake, Msaidizi wa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Hassan Galiatano alimshukuru Bw. Achiles kwa kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mfumo wa TanzLII, kwani itawasaidia kupandisha hukumu na maamuzi ya Majaji kwa usahihi, lakini pia imewaongezea weledi wa kuendelea kutoa elimu ya jinsi gani wananchi na wadau wanaweza kupata nyaraka katika mfumo huo.
Walioshiriki kupata elimu hiyo ya matumizi
sahihi ya mfumo wa TanzLII ni Watunza Kumbukumbu na Msaidizi wa Jaji wa
Mahakama Kuu Kigoma, ambayo imewaongezea weledi wa kutoa huduma za kupakia na
kupakua nyaraka katika mfumo huo.
Mkutubi wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Rwechungura Achiles akisisitiza jambo wakati akitoa elimu ya matumizi ya mfumo wa TanzLII kwa Msaidizi wa Sheria wa Jaji na Watunza Kumbukumbu wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma (hawapo katika picha).
Watunza Kumbukumbu wa Mahakama Kuu Kigoma, wakifuatilia kwa makini elimu iliyokuwa ikitolewa na Mkutubi wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Rwechungura Achiles (hayupo katika picha).
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni