Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe
Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya
Mahakama ya Njombe imeacha rasmi kutumia karatasi katika huduma za Mahakama zinazotolewazo
kwa wananchi na Mahakama hiyo kuanzia ngazi za Mahakama za Mwanzo mpaka ngazi
ya Mahakama Kuu Njombe.
Hatua
hiyo imefikiwa baada ya kikao kilichofanyika tarehe 25 Mei, 2026 kwenye ukumbi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe.
Katika
kikao hicho cha Mrejesho wa Mafunzo ya Viongozi na Watumishi wa Mahakama Njombe
ambao hivi karibuni walienda Mahakama Kuu ya Geita kufanya ziara ya kujifunza
mambo mbalimbali yenye lengo la kubadilishana uzoefu wa Matumizi ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utoaji haki kwa wananchi.
Kikao
hicho kilifunguliwa na Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Njombe, Bw. Richard
Mbambe ambaye alimkaribisha Mwenyekiti wa kikao hicho Jaji Mfawidhi wa Mahakama
kuu Njombe, Mhe.Victoria Nongwa pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala
Ndogo ya Mahakama Njombe, Mhe. Joseph Luambano kwa ajili ya kutoa mada
mbalimbali za Mafunzo waliyoyapata wakiwa Mahakama Kuu Geita.
Mhe.
Luambano aliwasilisha mada mbalimbali kwa watumishi waliohudhuria katika kikao
hicho pamoja na watumishi waliopo Wilaya za Wanging’ombe, Makete na Ludewa
ambao waliweza kuudhuria kwa njia ya Teknolojia ya video mtandao.
Mhe.Luambano alitoa mada kuhusu kutimiza majukumu ya kila siku ya kazi kwa
kutumia Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) kwa kuanza na Mfumo
wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS)
pamoja na mifumo inayosimamia masuala ya kiutawala hasa mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office)
pamoja na malipo ya uhasibu na manunuzi ya vifaa vya ofisi pamoja na mafuta ya
Magari ya Serikali.
Akiendelea
kutoa mada mbalimbali, kwa upande wa Wahudumu pamoja na Madereva aliwaeleza
kuwa, “kwa sasa suala la kuomba vifaa au mafuta ya magari pamoja na matengenezo
ya magari watumie njia mbadala na siyo kuomba mafuta kwa kuandika kwenye
makaratasi au matengenezo magari hivyo, watumie nakala laini kwa mifumo itakayowezeshwa
katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kila.”
Naye,
Mtendaji wa Mahakama Kuu Njombe, Bw.Mbambe alipata fursa wa kuzungumza na
watumishi na kuahidi kwamba, katika uchakataji wa Mifumo hiyo vifaa vinaitajika
na mwaka fedha wa 2026/2027 watumishi
wote watanunuliwa vifaa vya kisasa ili waweze kuendana na kasi ya teknolojia ya
sasa na kuwasisitiza watumishi waweze kubadilika waendane na mabadiliko ya sasa
katika ufanyaji kazi.
Aidha,
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe.Victoria
Nongwa alifunga kikao hicho ambacho Maofisa Mbalimbali wa Mahakama walipata
fursa ya kuchangia mada mbalimbali pamoja na kuuliza maswali na majibu yalitoka
papo kwa hapo.
Mhe.
Nongwa aliwasisitiza Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kuchapa wenyewe mashauri
wanayoyasikiliza na kuyaweka katika nakala laini ambapo yatakuwa yanahifadhiwa
katika mfumo maalum.
Kadhalika, Jaji Nongwa pia aliwasisitiza pia watumishi ambao sio Mahakimu kuyapokea mafunzo hayo na kuwaeleza kuwa, wawe na utayari wa kubadilika kutoka kwenye majukumu ambayo yalikuwa yanafanywa kwa njia ya kawaida yaani matumizi ya karatasi kwa sasa yaweze kuwa yanafanyika kwa njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kuwa mifumo hiyo inaleta ufanisi na uwazi katika kazi za Mahakama.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya
Njombe,Mhe. Victoria Nongwa (kulia) pamoja Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Obadia
Bwegoge wakimsikiliza Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe ,Mhe.Joseph Luambano (hayupo katika picha) wakati akitoa mada mbalimbali juu ya Mafunzo
waliyoyapata kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Geita.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe.Joseph Luambano (kulia) akitoa mada mbalimbali kwa Watumishi wa Mahakama Njombe (hawapo katika picha) juu ya Mafunzo
waliyoyapata kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Geita kwa kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Bw.Richard Mbambe (aliyesimama) akizungumza na watumishi kuhusu umuhimu wa kuwa na vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Walioketi meza kuu katikati ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa, kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe.Obadia Bwegoge na kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano.
Ofisa TEHAMA wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Bw.Fadhili Lwena akisisitiza juu ya matumizi ya baruapepe za ofisi kwa watumishi wa Mahakama hiyo. Walioketi mbele kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa, anayefuata ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Obadia Bwegoge.
Picha ya juu na chini ni watumishi waliohudhuria katika kikao hicho wakifuatilia kilichokuwa kikijiri katika kikao hicho.
(Habari imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni