Jumapili, 31 Mei 2026

TMJA GEITA YAFANYA ZIARA YA KUBADILISHANA UZOEFU MAHAKAMA KUU KIGOMA

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile amewaongoza Wajumbe wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma na Geita katika Mafunzo ya kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi.

Mafunzo hayo yalifanyika tarehe 29 Mei, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama ya Wazi uliopo katika Jengo la Mahakama Kuu Kigoma.

Akizungumza na wajumbe wa TMJA wa matawi hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Rwizile alieleleza lengo la ziara hiyo ni kuwawezesha Majaji na Mahakimu kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma na Geita kuendelea kujinoa kwa njia ya kubadilishana uzoefu ili kuongeza ujuzi katika utendaji kazi wa kila siku sambamba na kuleta tija na ufanisi wa utoaji huduma ya Utoaji Haki mapema ipasavyo.

“Waheshimiwa (Majaji na Mahakimu) kwa kupitia Chama chetu cha TMJA niwakaribishe Kigoma, huku tunafanya tofauti hivyo, kupitia ziara yenu Geita tutajifunza mengi nanyi mtajifunza pia kwani yapo mengi ambayo kwetu sisi yanapatikana Kigoma tu, tumejipanga kuboresha maeneo mengi baada ya hii ziara ya kubadilishana uzoefu katika utendaji wetu,” alisema Mhe. Rwizile.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina alieleza kwa ufupi historia ya maendeleo ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)k atika Masjala hiyo.

Alibainisha kuwa, juhudi za matumizi ya TEHAMA zilianza  kufuatia maelekezo na maono ya Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, alisisitiza kuwa, Mahakama Kuu Geita iwe mfano wa kuigwa katika matumizi ya TEHAMA ndani ya Mahakama.

Mhe. Mhina aliendelea kusema kuwa, Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Prof. Juma alisimamia kwa karibu utekelezaji wa maono hayo kwa kuwahamasisha watumishi na kuwaeleza msimamo wake kwamba matumizi ya karatasi yanapaswa kupunguzwa kwa kiwango kikubwa, kwani Mahakama isiyotumia karatasi inawezekana.

Aidha, alieleza kuwa kutokana na Mahakama za Mwanzo kutokuwa na mfumo rasmi wa matumizi ya TEHAMA, aliwaagiza Ofisa TEHAMA pamoja na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kutafuta njia mbadala za kuondokana na matumizi ya karatasi. Kufuatia maelekezo hayo, timu husika ilibuni mifumo mitano yenye sifa na uwezo tofauti. Baada ya kufanya tathmini, walibaini mfumo mmoja uliokuwa bora zaidi, ambao ndio unaotumika hadi sasa.

Mhe. Mhina aliongeza kuwa, baada ya kushirikisha Mahakama Kuu mbalimbali nchini kuhusu mfumo huo, walipokea ushauri wa kuuboresha kwa kuanzisha Kituo cha Kuhifadhi na Kusimamia Taarifa (Data Center) kitakachowezesha upatikanaji wa taarifa za Mahakama za Mwanzo kwa urahisi badala ya kutegemea mawasiliano ya simu.

Kutokana na ushauri huo, waliibua wazo la kuanzisha (Repository System), mfumo unaomuwezesha kila Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo kupakia (upload) kumbukumbu zote za mashauri anayoyasimamia.

Amesema, Mfumo huo unarahisisha upatikanaji wa nyaraka za mashauri pale rufaa inapowasilishwa katika Mahakama za juu. Vilevile, unawasaidia Majaji, Naibu Wasajili, Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mikoa na Wilaya pamoja na Viongozi wengine wa Mahakama kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa kazi za Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kwa urahisi zaidi, kupitia akaunti maalum zinazowawezesha kuona nyaraka na taarifa zote zilizopakiwa kwenye mfumo huo.

Aidha, ziara hiyo iliongozwa na Jaji Mfawidhi Geita ambaye pia alipata nafasi ya kupanda miti ya kivuli katika Mahakama ya Mwanzo Bangwe, vilevile TJMA pia walishiriki mashindano ya michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mchezo wa Mpira wa Miguu, Kuvuta Kamba, Riadha ya mbio fupi na kukimbia kwenye magunia.

Katika michezo hiyo kipindi cha kwanza Geita ilionekana kuwa kasi sana kwa kushinda bao tatu kwa nunge kutoka timu ya Kigoma. Magoli hayo yalifungwa ndani ya dakika 90.

Sehemu ya Wajumbe wa Chama Cha Mahakimu na Majaji Tanzania kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma na Geita wakisikiliza kwa makini mada iliyokuwa ikiwasilishwa katika kikao hicho cha kubadilishana uzoefu wa utendaji wa kazi kati ya Mahakama Kuu Kigoma na Mahakama Kuu Geita tarehe 29, Mei 2026. Wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile, kulia kwake ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Geita, Mhe. Kevin Mhina, wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi na wa kwanza kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Geita, Mhe.Griffin Mwakapeje. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akifungua kikao kazi cha kubadilishana uzoefu kati ya Wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Geita na Wanachama wa TMJA Kigoma kilichofanyika tarehe 29 Mei, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Geita, Mhe. Kevin Mhina akipanda mti wa kumbukumbu katika eneo la Mahakama ya Mwanzo Bangwe Kigoma wakati wa ziara ya kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi  kati ya TMJA Geita na Kigoma.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa akitambulisha wajumbe wa TMJA tawi la Kigoma, kwenye kikao cha kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masijala ndogo ya Geita, Mhe. Fredrick Lukuna akifanya utambulisho wa wajumbe wa TMJA tawi la Geita kwenye kikao cha kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi kati ya TMJA Geita na TMJA Kigoma kilichofanyika tarehe 29 Mei, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Uvinza, Mhe. Misana Majura akiwasilisha mada ya namna bora ya kusikiliza Mashauri ya Mirathi ikiwa ni sehemu ya kubadilishana uzoefu katika eneo hilo, katika kikao kazi kati ya TMJA Geita na TMJA Kigoma kilichofanyika tarehe 29 Mei, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma.

Picha ya pamoja ya Wajumbe wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma na Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Geita. Aliyeketi katikati ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile,  wa tatu kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Geita, Mhe. Kevin Mhina, wa tatu kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi, wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Geita, Mhe.Griffin Mwakapeje, wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa, wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya Buhigwe na Mwenyekiti wa Tawi la TMJA Kigoma, Mhe. Venance Mwakitalu, wa pili kushoto ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Nyang’hwale,  Mhe. Robert Nyando.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni