Jumatatu, 18 Mei 2026

MAHAKIMU KIGAMBONI, WADAU WA HAKI JINAI WAPIGWA MSASA UANDAAJI WA HOJA ZA AWALI

  • Watumishi wasio Mahakimu nao wapatiwa elimu matumizi ya TEHAMA

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Dar es Salaam

Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya na Mahakama za Mwanzo wilayani Kigamboni kwa kushirikiana na Wadau wa Haki Jinai, Mawakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) wamepatiwa mafunzo ya namna bora ya uandaaji wa hoja za awali, kuzisoma, jinsi ya kuzirekodi, umuhimu na madhara ya kutoweka umuhimu wa hatua hiyo muhimu katika usikilizaji wa mashauri ya jinai.

Mafunzo hayo yalitolewa tarehe 15 Mei, 2026 na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Awamu Mbagwa kwenye ukumbi wa Mahakama ya wazi ya Wilaya ya Kigamboni.

Wakati akifundisha, Mhe. Mbagwa aliwataka washiriki kueleza kwa namna wanavyojua maana na namna ya kuandaa na kushughulikia hoja za awali ambapo washiriki kila mmoja kwa uelewa wake alieleza.

Akitoa mafunzo hayo, Mhe. Mbagwa alianza kwa kueleza historia ya kuanzishwa kwa hatua hiyo ya hoja za awali katika mashauri ya jinai na kueleza lengo la kuanzishwa kwake ilikuwa ni kuharakisha usikilizwaji wa mashauri ya jinai kwa kuwa zile hoja zinazobishaniwa ndizo zinapaswa kuthibitishwa na upande wa mashtaka wakati wa uendeshwaji wa shauri.

Akifundisha kwa mfano, alisema iwapo mshtakiwa hakatai kuwa alikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi upande wa mashtaka hawana sababu ya kumpeleka Mahakamani. Askari Mkamataji huthibitisha kuwa, mshtakiwa alikamatwa na katika hoja za awali mshtakiwa hakupinga kukamatwa kwake.

Mhe. Mbagwa aliwasisitiza Waendesha Mashtaka kuandika hoja muhimu zinazojenga msingi wa shauri na si kuandika mambo ambayo hata kama yakithibitika hayana uzito wowote katika shauri hivyo kuandaa hoja hizo kwa kuzingatia mambo muhimu katika shauri husika (essential facts).

Aidha, Jaji Mbagwa aliwasisistiza Washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia hatua sita muhimu za kufuata wakati wa hatua hiyo muhimu ya kisheria kwa kuzingazita klifungu cha 198 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai. Hatua hizo ni kama Mwendesha Mashtaka kuzisoma hoja hizo, Mahakama kurekodi majibu ya Mshtakiwa, kuandaa muhtasari wa hoja zisizobishaniwa, Mshtakiwa kusomewa hoja zisizobishaniwa na mwisho Mwendesha Mashtaka, Mshtakiwa na Hakimu kuweka saini zao.

Akifungua mafunzo hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kigamboni, Mhe. Mwanakombo Twalib alimshukuru Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Awamu Mbagwa kwa utayari wake na kukubali kujitoa na kufika Kigamboni kuwapatia mafunzo hayo.

Alimueleza pia, Mhe. Mbagwa kuwa, kuna mafunzo yanayohusiana na uandaaji na umuhimu wa hoja za awali kwa Mahakimu na Mawakili wa Serikali huku watumishi wengine wasiokuwa Mahakimu watapatiwa mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo yatatolewa na Ofisa TEHAMA wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Tumaini Malima.

Kadhalika, Mhe. Mwanakombo alimueleza Jaji Mbagwa kwamba, wameamua kuchagua mada hiyo, kwa kuwa Hoja za Awali ni hatua muhimu katika usikilizaji wa mashauri ya jinai. 

“Mhe. Jaji na washiriki wenzangu mtakubaliana na mimi kuwa ‘PH’ ni ‘road map’ ya shauri zima, maana hapa tunaona hoja zinazobishaniwa na zisizobishaniwa,” alisema Mfawidhi huyo wa Mahakama ya Wilaya Kigamboni.

Aliongeza kuwa, mafunzo hayo yamekusudiwa kuwapa uelewa wa pamoja na mambo ya kuzingatia katika hatua hiyo muhimu.

Naye Ofisa TEHAMA wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Tumaini Malima aliwafundisha watumishi wasio Mahakimu namna bora ya kutumia mifumo mbalimbali ya ki-TEHAMA mahakamani ikiwemo matumizi ya Ofisi Mtandao (e-Office, Mfumo wa Kielektroniki wa Menejimenti ya Mashauri (e-CMS), (e-Filling) na mingine.

Kadhalika, Bw. Malima aliwasisistiza watumishi hao kuwapatia nakala za hukumu wateja ambao hawana uwakilishi mahakamani  na hawana akaunti za kuwezesha kupata nakala hizo.

Naye Mkuu wa Mashtaka wa Wilaya ya Kigamboni, Bi. Anita Sinare alimshukuru Mhe. Mbagwa kwa elimu aliyowapatia na kuahidi kuifikisha kwa Mawakili wenzao ambao hawakubahatika kuhudhuria mafunzo hayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kigamboni, Bi. Bibiana Bundala alisema japo yeye sio Mwanasheria lakini mafunzo hayo yamempa uelewa mkubwa kuhusu nini kinapaswa kufanyika katika hatua hiyo muhimu na hivyo, itawezesha kuwabana watumishi walio chini yake na kusimamia ufanyikaji wa hatua hizo muhimu pale shauri linapofunguliwa Mahakamani.

Akitoa salamu za shukrani kwa Jaji Mbagwa baada ya mafunzo hayo, Mhe.  Christina Lugulu alisema kuwa, wamepata chakula cha akili na aliwashukuru wadau kwa kuhudhuria mafunzo hayo. 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Awamu Mbagwa akifundisha Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya na Mahakama za Mwambo Kigamboni pamoja na washiriki wengine wa mafunzo (Wadau wa Haki Jinai) hayo kuhusu mada ya namna bora ya uandaaji wa hoja za awali. Mafunzo hayo yalitolewa tarehe 15 Mei, 2026.


Hakimu Mkazi  Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kigamboni, Mhe. Mwanakombo Twalib (kushoto) akitoa neno la ufunguzi wa mafunzo. Aliyeketi katikati ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Awamu Mbagwa ambaye pia alikuwa Mwezeshaji wa mafunzo hayo na  kulia ni Bi. Pendo Kilusu, Ofisa Utumishi wa Mahakama ya Wilaya Kigamboni.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Awamu Mbagwa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya na Mwanzo Kigamboni mara baada ya mafunzo yaliyofanyika katika Mahakama hiyo tarehe 15 Mei, 2026.


Jaji Awamu Mbagwa (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya watumishi  wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana  Rushwa  (TAKUKURU) na wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) Wilaya ya Kigamboni. Wa pili kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kigambo, Mhe. Mwanakombo Twalib.


Watumishi wasio Mahakimu wakiendelea na Mafunzo ya TEHAMA.

Ofisa TEHAMA wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Tumaini Malima akifundisha kuhusu Mafumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS).

 Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe Awamu Mbagwa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na  Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kigamboni, Mhe. Mwanakombo Twalib (kushoto) na Ofisa Utumishi wa Mahakama ya Wilaya Kigamboni, Bi. Upendo Kilusu (kulia).

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya mwanzo Kigamboni, Mhe. Christina Lugulu  akitoa neno la shukrani kwa Jaji Mbagwa ambaye alikuwa Mwezeshaji wa Mafunzo hayo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni