Jumatano, 20 Mei 2026

WATUMISHI WA MAHAKAMA KUU NJOMBE WAFANYA ZIARA YA MAFUNZO GEITA

Na DOTTO NKAJA-Mahakama, Geita

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita, Griffin Mwakapeje, ameipongeza Mahakama Kuu Njombe kwa kufanya ziara ya mafunzo katika Mahakama ya Geita yenye lengo la kubadilishana uzoefu wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utoaji wa haki kwa wananchi.

Mhe. Mwakapeje alitoa pongezi hizo juzi tarehe 18 Mei, 2026 katika Ukumbi wa Mafunzo wa Mahakama Kuu Geita wakati akiwakaribisha wajumbe kutoka Mahakama Kuu Njombe. Alisema kuwa Geita imeendelea kuwa mfano bora katika matumizi ya TEHAMA ndani ya Mhimili wa Mahakama.

“Mmefanya uamuzi sahihi sana kuichagua Mahakama Kuu Geita kama sehemu ya kujifunza matumizi ya TEHAMA, hivyo natarajia mafunzo haya yawe na mafanikio chanya katika kuongeza kasi ya utoaji haki kwa wakati,” alisema Jaji Mwakapeje.

Aidha, aliwashukuru Viongozi wa Mahakama Masjala Ndogo Njombe kwa kujipanga kujifunza kwa vitengo mbalimbali vya Mahakama ili kuongeza ufanisi wa kazi na kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Katika ziara hiyo, mada mbalimbali ziliwasilishwa na menejimenti ya Mahakama Kuu Geita, zikieleza namna mifumo ya TEHAMA inavyotumika kurahisisha utoaji wa haki kwa wakati pamoja na kuongeza uwazi katika utendaji kazi wa Mahakama.

Naibu Msajili wa Mahakama ya Tanzania Masjala Ndogo Geita, Mhe. Fredrick Lukuna, aliwasilisha mada kuhusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa mashauri na namna Mahakama hiyo inavyoendesha shughuli zake bila matumizi ya karatasi.

Alieleza kuwa mfumo huo umeongeza ufanisi, uwazi na urahisi wa usimamizi wa shughuli za Mahakama, huku Viongozi wakipata uwezo wa kukagua mwenendo wa kazi kupitia mfumo huo bila kufika moja kwa moja katika maeneo husika.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Geita, Mhe. Mujuni Muchunguzi, alifafanua jinsi Mahakama za Wilaya zinavyotumia mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa mashauri na shughuli za kiutawala.

Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Nyankumbu, Mhe. Ally Mgomba, alieleza namna Mahakama za Mwanzo zilivyoondokana na matumizi ya karatasi kupitia mfumo maalum uliobuniwa na unaotumika katika Mahakama zote za Mwanzo Masjala Ndogo Geita.

Mada nyingine iliwasilishwa na Winifrida Nghumbu, ambaye alieleza namna huduma ya KIOSK inavyowasaidia wananchi kupata taarifa za kesi, kusajili kesi na kufuatilia mwenendo wa mashauri yao kwa urahisi, hata kwa wale wasio na uelewa wa mifumo ya Mahakama.

Pia, Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Geita, Happiness Mushi, alieleza namna utawala wa Mahakama hiyo ulivyoachana na matumizi ya karatasi kwa kutumia mifumo ya e-Office pamoja na mawasiliano ya barua pepe.

Akitoa neno la shukrani baada ya mawasilisho hayo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Njombe, Mhe. Joseph Luambano, alisema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwao kutokana na mafunzo waliopata kuhusu matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa haki.

“Kufuatia ziara hii ya kubadilishana uzoefu, tumejifunza mambo mengi yenye kujenga na kutuonesha maeneo tunayopaswa kuboresha katika matumizi ya TEHAMA. Tunaahidi kuwa walimu kwa wengine na kuhakikisha haki inatolewa kwa wakati kwa kuzingatia taratibu bila kumuathiri mtu yeyote,” alisema Mhe. Luambano.

Ziara hiyo iliongozwa na Mhe. Luambano, pamoja na Mtendaji wa Mahakama, Liad Chamshama, na watumishi wawakilishi kutoka kada mbalimbali za Mahakama ya Njombe.

Jaji wa Mahakama ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita, Mhe. Griffin Mwakapeje, akifungua mafunzo.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita, Mhe. Fredrick Lukuna, akitoa ufafanuzi juu ya ushirikiano biana ya Viongozi na Watumishi unavyoleta mafanikio katika kuongeza ufanisi wa matimizi ya Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Njombe, Mhe. Joseph Luambano, akitoa neno la shukrani kwa uongozi wa Mahakama Geita.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Geita, Mhe. Mujuni Muchunguzi, akielezea namna Mahakama za Wilaya zilivyoachana na matumizi ya karatasi katika uendeshaji wa kesi na shughuli za kiutawala.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Nyankumbu, Mhe. Ally Mgomba, akilekeza jinsi Mahakama za Mwanzo zilivyoachana na matumizi ya karatasi.

Kaimu Mtendaji wa Mahakama Geita, Bi. Happines Mushi, akielezea namna utawala ulivyoachana na matumizi ya karatasi.

Ofisa Kumbukumbu, Bi. Winifrida Warsha, akiekelezea huduma ya KIOSK inavyowasaidia wananchi kusajili kesi na kuelewa mienendo ya kesi.

Picha ya pamoja ya Watumishi wa Mahakama Kuu Geita na watumishi wa Mahakama Kuu Njombe katika jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Geita.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni