Ijumaa, 8 Mei 2026

MAHAKIMU NJOMBE PUNGUZENI KUKAA NA MASHAURI MAHAKAMANI KWA MUDA MREFU; JAJI NONGWA

Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe, Victoria Nongwa amewataka Mahakimu wa Mahakama za Wilaya pamoja na za Mwanzo  kutokukaa na mashauri Mahakamani kwa muda Mrefu.

Mhe. Nongwa aliyasema hayo akiwa kwenye ziara ya kikazi aliyoianza tarehe 28 Aprili ,2026 hadi tarehe 4 Mei, 2026, ambapo alisema, “Hakikisheni mashauri yote yanayotokea Polisi yana ushahidi uliokamilika au mashahidi wamepatikana ili mashauri hayo yaweze kusikilizwa na kumalizika haraka ipasavyo na siyo kuchelewesha mashauri hayo bila sababu za msingi na yale mashauri ambayo hayana Mashahidi yasipokelewe mahakamani.”

Aidha, Jaji Nongwa aliwasisitiza Mahakimu kuwa, anatarajia kuona mashauri yanasikilizwa kwa haki, uadilifu na kwa wakati ili kutimiza dhana ya utoaji haki kwa wananchi mapema ipasavyo.

Katika ziara hiyo ya kikazi kwa Mahakama za Wilaya za Ludewa, Wanging’ombe na Makete waliwasilisha taarifa mbalimbali za Mashauri zilizosomwa na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya pamoja na taarifa za Utawala huku Mhe. Nongwa akisikiliza hoja mbalimbali zilizotolewa na watumishi wasio Mahakimu na kuzitafutia ufumbuzi ambazo nyingine zilijibiwa na Viongozi aliombatana nao.

 Akiendelea kuzungumza na watumishi,  aliwasisitiza juu ya umuhimu wa kila mmoja wao kujua  Nguzo Kuu za Mpango Mkakati wa Mahakama na kila mtumishi anatakiwa kujua wajibu wake pamoja na uwajibikaji huku akikemea vitendo viovu vinavyoashiria mazingira ya rushwa pamoja na kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) mahakamani.

Katika ziara hiyo, Jaji Mfawidhi huyo aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Njombe, Mhe. Joseph Luambano, Mtendaji wa Mahakama Kuu Njombe, Bw. Richard Mbambe na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama ambao waliweza kujibu hoja mbalimbali za watumishi pamoja na kutoa neno la shukrani katika ziara hiyo.  


 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya Wanging'ombe (waliosimama). Wa pili kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano, wa kwanza kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Njombe, Bw. Richard Mbambe, wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama na wa pili kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Wanging’ombe, Mhe. James Muhoni.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Lupembe(hawapo katika picha) alipofanya ziara katika Mahakama hiyo hivi karibuni.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe,Mhe. Victoria Nongwa (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Njombe, Mhe. Joseph Luambano (wa pili kulia), wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Njombe, Mhe. Matilda Kayombo, wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama, wa pili kushoto ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Lupembe, Mhe. Godfrey Msemwa na wa tatu kushoto ni anayefata ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Njombe, Bw,Richard Mbambe na waliosimama nyuma ni sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Lupembe.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Njombe Mjini. Kutoka kushoto ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Njombe Mjini, Mhe. Lisa Abel  anayefuata ni Mtumishi aitwaye Bi. Beatrice Liahumi,  nyuma ya kiti upande wa kulia ni Mwandishi Mwendesha Ofisi, Bi. Agusta Msingwa akiwa pamoja na Mwenzake  Mwandishi Mwendesha Ofisi Bi.Sofia Kimena ambapo viti vya nyuma  kulia ni Watumishi wa Mahakama, Bw. Justin Kiduli pamoja na Hashimu.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu ya Tanzania ,kanda ya Njombe,Mhe, Victoria Nongwa (katikati) pamoja na Viongozi wengine wa Mahakama Njombe wakiwa katika picha ya pamoja na  sehemu ya watumishi wa Mahakama ya wilaya Makete.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu ya Tanzania ,kanda ya Njombe,Mhe, Victoria Nongwa (katikati) pamoja na Viongozi wengine wa Mahakama Njombe wakiwa katika picha ya pamoja na  sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Manda alipofanya ziara katika Mahakama hiyo hivi karibuni.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa akimwagilia Mche wa Mparachichi mara baada ya kuupanda katika viunga vya Mahakama ya Wilaya Wanging’ombe alipofanya ziara katia Mahakama hiyo hivi karibuni.  Kushoto ni Ofisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Wanging’ombe,  Bw.Riziki Sanga.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Njombe)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni