Ijumaa, 8 Mei 2026

JAJI MFAWIDHI KATAVI ASISITIZA MATUMIZI YA TEHAMA MAHAKAMA ZA MWANZO

Na. ALLY RAMADHANI – Mahakama, Katavi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Katavi, Mhe. Godfrey Ntemi Isaya amewasisitiza watumishi wa Mahakama za Mwanzo katika Masjala hiyo kutumia Mifumo ya TEHAMA katika shughuli zao za kiutendaji.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Mhe. Isaya alipokuwa kwenye ziara yake ya ukaguzi wa Mahakama ili kuangalia utendaji kazi wa kila siku wa utoaji huduma za haki kwa wananchi, ziara hiyo ya ukaguzi ilifanyika kuanzia tarehe 28 Aprili, 2026 hadi 07 Mei 2026 katika Wilaya za Mpanda, Mlele na Tanganyika.

Katika ziara hiyo, Mhe. Isaya alifanikiwa kutembelea Vituo vyote vya Mahakama za Mwanzo zinazoendelea kujengwa ndani ya Mkoa wa Katavi kama vile Sibwesa, Ugalla na Mamba na kupata wasaa wa kuwasisitiza watumishi wa maeneo hayo kuendeleza na mapambano ya matumizi ya TEHAMA ili kurahisisha utoaji haki kwa wananchi wanaowahudumia.

Kupitia ziara hiyo Mhe. Isaya aliwakumbusha watumishi wa Mahakama za Mwanzo mkoani Katavi kuendelea kutumia Mifumo ya TEHAMA ikiwemo Primary Court App, ili kurahisha utendaji kazi wa Mahakama kwa ujumla.

Aidha, Mhe. Isaya aliongeza kuwa, kazi ya kutoa haki sio jambo dogo hivyo watumishi wasijiingize katika vitendo viovu vinavyoweza kuharibu taswira ya Mahakama na kupunguza imani kwa wananchi,

“Ndugu watumishi nawasisitiza kuwa waadilifu kwa kuwa ndiyo msingi mkubwa wa kutoa haki, hivyo muwe na tabia njema kazini na nje ya kazi na tuendelee kuchapa kazi tuwatumikie wananchi, tuepuke ile hali ya kuwa miungu watu kwenye ofisi zetu na kuongeza kuwa, kila mmoja kufanya kazi kwa bidii na umoja “If people cannot pay you, the nature will,” alisema Jaji Isaya.

Kwa upande mwingine, Mhe Isaya aliwapongeza watumishi wote kwa ujumla kwa kazi nzuri inayofanyika hususani usikilizwaji wa mashauri kwani katika taarifa zote zilizowasilishwa zimeonyesha kuwa mashauri yanafunguliwa na yanaisha kwa wakati.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Katavi Mhe. Godfrey Ntemi Isaya (katikati) akiwa kwenye Picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali wa Masjala hiyo alipotembelea jengo la Mahakama ya Mwanzo Wilaya Mpanda Kituo  cha Ugalla.

Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Katavi, Mhe. Silivia S. Lushasi (aliyesimama) akiongea na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Wilaya Mpanda kituo cha Mpanda Mjini alipokua kwenye ziara ya Mhe Jaji Mfawidhi Kanda ya Katavi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Katavi Mhe. Godfrey Ntemi Isaya (wa kwanza Kulia mwenye suti nyeusi) akikagua baadhi ya mipaka ya eneo la Mahakama ya Mwanzo Wilaya Mpanda Kituo cha Shanwe.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni