Jumamosi, 9 Mei 2026

KAMATI YA JAJI MKUU UFUATILIAJI NA TATHMINI YAFANYA UKAGUZI MAALUM MAHAKAMA PWANI

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Shinyanga ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Jaji Mkuu ya Ufuatiliaji na Tathmini, Mhe. John Kahyoza amefanya ukaguzi katika Mahakama za Hakimu Mkazi Pwani, Mahakama ya Wilaya Kibaha na Mahakama ya Mwanzo Mailimoja ili kufanya tathmini ya usahihi wa taarifa na namna ambavyo Mahakama hizo zinavyofanya kazi.

Akizungumza mara baada ya kuwasili ofisini kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi, tarehe 07 Mei, 2026, Mhe. Khyoza alisema wao sio Wakaguzi wa moja kwa moja bali wao wanaangalia taarifa za ukaguzi zinazowafikia na usahihi wake na kumtaarifu Jaji Mkuu kama mambo yako sawa, akieleza kuwa hilo ni jukumu mojawapo la kamati hiyo.

Akizungumza na watumishi baada ya ukaguzi, Mhe. Kahyoza alisema mara yake ya mwisho kufika kwenye jengo la Mahakama hiyo ni siku jengo lilipokabidhiwa tarehe 21 Septemba, 2016 ambapo amewapongeza wasimamizi wa jengo hilo, wakuwa wameweza kuzingatia usafi wa jengo. Aliongeza kwa kusema, “Kwahiyo nimefurahi kitu cha kwanza kufika kwenye jengo hili tena nikaridhishwa na usafi kweli niwapongeze sana mnaosimamia na mnaofanya usafi wa mazingira na kuyatunza pia.”

Aliendelea kuwapongeza zaidi na kusema kuwa, usafi ni jambo jema linalotia nguvu na kuna kipindi kulikuwa kuna azimio linalozungumzia utunzaji wa mazingira. Amekumbusha pia alikuwa Jaji Mfawidhi Mwanzilishi wa  Mahakama Kuu Musoma walipanda miti ya vivuli na matunda, jambo ambalo Jaji Mkuu wa kipindi hicho ambacho anakabidhi Mahakama Kuu Musoma alisema makabidhiano yaambatane na mazingira safi.

Akiwaeleza watumishi wa Mahakama hiyo, lengo la ujio wake alisema wao kazi yao kubwa wanaangalia namna Wakaguzi wanavyokagua ili kuona wanachowaambia kama ni sahihi pia wataangalia namna Mahakama za Mwanzo zinavyofanya kazi ili kile wanachoambiwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi kama ni sahihi.

Amesema pia, wameona rejesta ya malalamiko kwenye shughuli za kiutawala japo kwenye masuala ya pesa hawaingii huko sana japo wameona taarifa ya utekelezaji. Alibainisha kuwa, utekelezaji wa Mpango Mkakati hauwezi kufanikiwa bila kujua bajeti na Nguzo ya Kwanza ya mpango huo ambayo ni Usimamizi wa Rasilimali za Mahakama.

Ameongeza kwamba, wakati anasimamia mambo ya utawala alikuwa anatumia neno GAP ambapo ameeleza kuwa, ukilijua neno hilo unaweza kuujua Mpango Mkakati wa Mahakama kwa urahisi.

Akieleza maana ya neno (GAP), Mhe. Khyoza amesema “G inasimamia (Governance) Usimamizi wa rasilimaliwatu, rasilimali fedha na utawala, A inasimamia nguzo ya (Access to Justice and Expeditiousness) na P ni (Public Trust and Stakeholders’ Engagement).

Amesema kuwa, mtu hawezi kuzitekeleza nguzo hizo bila mambo ya utawala kukaa vizuri, kuwepo na pesa bila usimamizi mzuri zitaishia kufanya vitu visivyoeleweka. Pia majengo yasipotunzwa vizuri Jaji au Hakimu hawezi kuendesha mashauri lakini pia haki za watumishi zisipolipwa na kuandaliwa vyeo kupanda pia haiwezekani kufanya kazi vizuri.

Amebainisha kuwa, “Nguzo ya ‘Access to Justice’ ndio nguzo mama kila siku tunashinda nayo.”

Pamoja na ukaguzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Wilaya, Jaji Kahyoza amekagua pia Mahakama ya Mwanzo Mailimoja, ambapo amewashauri Mahakimu wakichapa mwenendo wa mashauri wahifadhi katika Kompyuta ya Masjala na sehemu nyingine. Hiyo itasaidia hata kama haiwezi kupatikana sehemu mojawapo basi itapatikana sehemu nyingine.

Amesema kuwa, kitendo cha mtu mmoja kukaa na mwenendo si kizuri, ikitokea amehama anaweza kuondoka na mwenendo na wakati mwingine inaweza ikawa ngumu kupatikana.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kahyoza amewapongeza Mahakimu wa Mahakama hiyo kwa kuwahi kufika kazini maana matarajio yake ilikuwa ni kufika saa tatu asubuhi hivyo alitoka mapema sana kuogopa foleni lakini hakukuta foleni na kuwahi kufika tofauti na muda lakini aliwakuta Mahakimu na watumishi wengine tayari wameshafika ofisini.

Akizungumza wakati wa kumkaribisha Mjumbe wa Kamati ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Jaji Mkuu, Ofisa kutoka Kurugenzi ya Ukaguzi na Maadili, Mhe. Elias Migella amesema majukumu ya Kamati hiyo ni kufanya ufuatiliaji na tathmini ya huduma katika masuala ya kimahakama na kiutawala. 

Kadhalika, Mhe. Migella alizungumza na watumishi  wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha.

Kamati ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Jaji Mkuu ina wajumbe nane ambao watatembelea Mahakama nchi nzima kwa lengo la kufanya ukaguzi na kurejesha taarifa kwa Jaji Mkuu.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Shinyanga na Mjumbe wa Kamati ya Jaji Mkuu ya Ufuatiliaji na Tathmini, Mhe. John Kahyoza (kulia) akiwasili Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani tarehe 07 Mei, 2026 tayari kwa kuendelea na jukumu la ukaguzi katika Mahakama hiyo. Kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi akimuongoza Jaji Kahyoza.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Shinyanga na Mjumbe wa Kamati ya Jaji Mkuu ya Ufuatiliaji na Tathmini, Mhe. John Kahyoza akisaini kitabu cha wageni alipowasili kwenye Ofisi ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi-Pwani.

Mjumbe wa Kamati ya Jaji Mkuu ya Ufuatiliaji na Tathmini ykutoka Kurugenzi ya Ukaguzi na Maadili, Bw. Elias Migella akimkaribisha Mhe. John Kahyoza ili azungumze na watumishi (hawapo katika picha). 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Shinyanga na Mjumbe wa Kamati  ya Jaji Mkuu ya Ufuatiliaji na Tathimini, Mhe. John Kahyoza akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani na Mahakama ya Wilaya Kibaha mara baada ya ukaguzi katika Mahakama hizo. Kulia ni Mjumbe wa Kamati ya Jaji Mkuu ya Ufuatiliaji na Tathmini ykutoka Kurugenzi ya Ukaguzi na Maadili, Bw. Elias Migella na kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi. 

Baadhi wa watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Shinyanga na Mjumbe wa Kamati  ya Jaji Mkuu ya Ufuatiliaji na Tathimini, Mhe. John Kahyoza (hayupo katika picha).


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Shinyanga na Mjumbe wa Kamati ya Jaji Mkuu ya Ufuatiliaji na Tathmini, Mhe. John Kahyoza (katikati)  akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu Wakazi wa Mahakama ya Mwanzo Mailimoja. Aliyeasimama kushoto mstari wa mbele ni Mjumbe wa Kamati ya Jaji Mkuu ya Ufuatiliaji na Tathmini ykutoka Kurugenzi ya Ukaguzi na Maadili, Bw. Elias Migella na kulia ni  Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi. 

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni