Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Dar es Salaam
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Amidi wa Mahakama hiyo, Mhe. Iman Abood amefungua mafunzo ya Miliki Bunifu yanayowahusisha Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Mahakama ya Kuu Divisheni ya Biashara lengo likiwa ni kuwapa uelewa zaidi juu ya jambo hilo.
Akifungua mafunzo hayo jana tarehe 11 Mei, 2026 kwenye Hoteli ya Crowne Plaza jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Jaji Kiongozi, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, Mhe. Aboud alisema katika uchumi wa dunia ya leo hati miliki imekua moja ya mali ya thamani zaidi kuendesha uvumbuzi, ukuaji wa viwanda, ubunifu na biashara za kimataifa.
Jaji Abood alisema pia Nchi zinazoongoza kwa uchumi duniani hazijengwi juu ya rasilimali asili tu bali pia mawazo, uvumbuzi chapa, kazi za kisanii miundo na teknolojia za kidijitali ambazo huchangia ushindani na ustawi wa Taifa.
Aliongeza kuwa, kwa Tanzania ulinzi madhubuti na utekelezaji wa haki miliki unaendana moja kwa moja na lengo pana chini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 na msukumo unaoendelea kuelekea ukuaji wa viwanda, uvumbuzi na uchumi unaotegemea maarifa.
Amesema, Mahakama inasimama katikati ya utekelezaji wa hati miliki wakati Mashirika kama vile Tume ya Ushindani (FCC), BRELA, TIRDO na COSOTA hushugulikia masuala ya utawala, Mahakama zinahakikisha kwamba haki inapatikana na kuheshimiwa kikamilifu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Abood alisema kuwa, yeye amemwakilisha Jaji Kiongozi ambaye ndiye alitakiwa kuwepo ila kutokana na majukumu mengine aliyonayo hakuweza kushiriki.
Amesema mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam wakishirikiana na Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara pamoja na Wadau wengine wa Mahakama kama Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Ofisi ya Haki Miliki Tanzania (COSOTA), Tume ya Ushindani (FCC) na wengine ambao wapo mahsusi kwa ajili kuwawezesha Majaji kupata elimu zaidi na pia kubadilishana uzoefu kuhusu Miliki Bunifu. Ameongeza, “kama unavyojua maendeleo kuchelewa sana inategemea na ubunifu.”
“Mahakama kama Watafsiri wa Sheria zinazohusu hayo na kuhakikisha kunakuwa na utekelezaji inabidi kuelewa kwa undani mchakato mzima na nini maana ya Miliki Bunifu wameona ni muhimu sana kupata mafunzo hayo ya siku mbili kwa sababu maamuzi yao sio tu kwamba yatatumika ndani ya nchi bali pia yamechaguliwa kuwekwa kwenye kanzidata (database) ambapo nchi nyingine wanasoma na wanaweza kuyatumia pia,” ameeleza Jaji Abood.
Ameongeza kuwa, mtu anaweza kubuni mradi wake wa kusuka nywele tu na ukachukuliwa na watu wengine wakanufaika wakati yeye ndiye mnufaika wa kwanza. Pia ilielezwa kuwa, kuna watu wanatumia taswira za watu kubuni katika Makampuni mbalimbali na watu wakapelekea shauri na kulalamika kwa hiyo ikaonekana ni ngumu kwa Majaji na Mahakimu kama watoa haki ambao wanatafsiri sheria kutoa hukumu na kuhakikisha zinatekelezeka waelewe kiundani.
Jaji Abood amemnukuu Jaji Kiongozi kuwa, “huu ni mwanzo tu mafunzo haya yataendelea kuwezesha na baadae kuwapata Majaji na Mahakimu wataalam kwenye eneo hili la miliki bunifu. Na kama ikiendelea hivyo watu watahakikisha kwamba hizo miliki bunifu zinalindwa na wawekezaji pia watakaribishwa.”
Amesema, kwa hatua hiyo watu wataamua kuanzisha bidhaa mbalimbali ambazo watabuni pamoja na kumiliki miradi mbalimbali. Hatua hiyo itachochea ukuaji wa uchumi wa nchi na kuhakikisha kwamba wanatimiza lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo.
Akijibu swali aliloulizwa na Mwandishi wa Azam Media kuhusu idadi ya Majaji wenye utaalam wa Miliki Bunifu, Mhe. Abood amesema hana uhakika ni wangapi wana utaalam huo japo amesema wameona shida ni kubwa ndio maana wameona kuna umuhimu na haja ya kufanya mafunzo hayo na wameanza na Dar es Salaam lakini mpango mkakati ni kwamba Majaji wote nchi nzima waweze kupata mafunzo hayo.
Akimkaribisha Jaji Abood, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe Salma Maghimbi amesema wizi halisi wa haki miliki sio tu kutoa nakala bali pia ni unyang’anyi wa haki za ubunifu.
Mhe. Maghimbi amesema, kwa sasa Mahakama zinashughulikia mashauri yanayohusisha alama za biashara, haki miliki, usanifu wa viwanda, viashiria vya kijiografia na siri za biashara. Changamoto mpya kama ukiukaji mitandaoni, uharamia wa kidijitali, maudhui ya akili unde na utekelezaji wa sheria mipakani hizi zinachanganya michakato ya Mahakama licha ya kuwepo mfumo wa kisheria.
“Maofisa wa Mahakama bado wanakabiliwa na mapungufu ya uwezo wa kusimamia, ufundi, kiutaratibu na ushahidi na vipengele vya utekelezaji wa miliki bunifu, hii imewapa nguvu ya kuendesha mafunzo hayo,” amesema Jaji Maghimbi.
Ameeleza kwamba, mpango huo utatoa mwelekeo wa vitendo na wa Mahakama juu ya mada ya haki miliki, taratibu za usajili na athari zake katika mashauri, kuthibitisha ukiukwaji, tathmini ya ushahidi wa kiufundi, muingiliano wa nafuu, changamoto ya kisiasa katika utekelezaji wa haki miliki.
Naye Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Cleophas Moriss amesema, mafunzo hayo yatawasaidia kuelewa kwa sababu mada zimepangwa katika mtiririko ambao utawapatia nafasi ya pekee kuongeza ujuzi kwakuwa mada zimepangwa kumuwezesha mtu kufahamu kuanzia chanzo na chimbuko la haki hiyo na maendeleo yake kitaifa na kimataifa.
Mhe. Morris amesema wataangalia jinsi kanuni zinavyozidi kukua katika tasnia husika na kwa nchi na kimataifa na pia wanaangalia sheria za nchi zimepangwa vipi au zimetengenezwa kwa mtindo gani katika kuleta uwiano wa kikanuni wa kitaifa na kimataifa.
Naye, Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa amesema sio mara ya kwanza wao kutoa mafunzo hayo, wameshawahi kutoa kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani.
“Lengo la kutoa mafunzo haya ni kuwapa elimu Majaji uelewa kuhusu masuala mazima ya miliki ubunifu kwa sababu eneo hili ni geni kidogo hapa nchini na baada ya kuangalia hukumu kadhaa ambazo zimekuwa zikitolewa na Majaji wakaona kuna umuhimu sasa wa kupeana elimu hiyo ili wawe pamoja,” ameeleza Bw. Nyaisa.
Amesema katika maamuzi ya Majaji huwa wanagusa maslahi ya Nchi katika eneo la miliki ubunifu na kwamba zipo hukumu kadhaa ambazo zimetolewa na Majaji zimewasaidia sana katika utendaji wa majukumu yao.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani, Bi. Khadija Ngasongwa amesema wameungana na Mahakama kutoa mafunzo ya miliki bunifu ambazo katika sehemu ya sheria alama ya bidhaa wao ni kama Polisi au Wasimamizi wa kulinda miliki bunifu nchini hasa katika upande wa alama za bidhaa (IPR) imeelezewa katika sheria ambayo kwa sasa wanaifanyia marekebisho.
Amesema katika uzalishaji wa kusajili alama ya bidhaa au nembo
inayofanywa na wakala wa BRELA wao kazi yao wanazirekodi ili waweze kuzitambua
sokoni bidhaa halisi ni ipi na ambayo sio halisi.
Mafunzo hayo ya siku mbili baada ya kufunguliwa wameanza kwa masomo ya muhtasari wa Haki Miliki, Mfumo wa Kisheria wa Taasisi wa Haki Miliki nchini Tanzania, uamuzi na utekelezaji wa haki miliki na umuhimu wa kisheria wa hatua za usajili katika madai. Masomo hayo yamefundishwa na Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Saudine Mwakaje na Wakili Mshirika wa ‘Next Law Advocates’, Bw. Seka Kasera na Msajili Msaidizi/Meneja wa Alama za Biashara na Huduma.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Amidi wa Mahakama hiyo, Mhe. Iman Abood akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo ya Miliki Bunifu jana tarehe 11 Mei, 2026 kwa niaba ya Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo Miliki Bunifu wakifuatailia hotuba ya mgeni rasmi (hayupo katika picha).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akitoa neno fupi wakati wa hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya Miliki Bunifu.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Livin Lyakinana akifanya utambulisho wa washiriki wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Miliki Bunifu.
Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa akitoa salam wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Miliki Bunifu jana tarehe 11 Mei, 2026 jijini Dar es Salaam.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Amidi wa Mahakama hiyo, Mhe. Iman Abood (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wanaoshiriki katika Mafunzo ya Miliki Bunifu (waliosimama baadhi). Walioketi wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi, wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Cyprian Mkeha, wa kwanza kushoto ni Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa na wa kwanza kulia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Bi. Khadija Ngasongwa.
Meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na Wawezeshaji wa Mafunzo ya Miliki Bunifu. Walioketi katikati ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Amidi wa Mahakama hiyo, Mhe. Iman Abood, wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi, wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Cyprian Mkeha, wa kwanza kushoto ni Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa na wa kwanza kulia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Bi. Khadija Ngasongwa.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)










Hakuna maoni:
Chapisha Maoni