Jumatano, 27 Mei 2026

WATUMISHI WA MAHAKAMA BUKOBA WAKUMBUSHWA KUTOA HUDUMA BORA KWA WATEJA

  •  Wasisitizwa pia kuzingatia matumizi ya Teknolojia na kujiendeleza kielimu

Na MICHAEL RITTE, Mahakama-Bukoba

Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba wamehimizwa kuendelea kuboresha huduma kwa wateja, kutumia lugha nzuri wanapohudumia wananchi pamoja na kujiendeleza kielimu ili kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani.

Wito huo umetolewa na Viongozi kutoka Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania wakati wa kikao cha utoaji wa elimu ya huduma kwa wateja kilichofanyika tarehe 26 Mei, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba.

Kikao hicho cha mafunzo na majadiliano kililenga kuwakumbusha watumishi umuhimu wa huduma bora kwa wananchi pamoja na matumizi sahihi ya mifumo ya kisasa ya utoaji huduma.

Akizungumza katika kikao hicho, Mmoja kati ya Viongozi kutoka Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Aloyce Katemana alisema, Mahakama ya Tanzania imeendelea kuboresha mifumo yake ya huduma kwa wananchi kupitia Kituo cha Huduma kwa Wateja kinachopatikana kupitia namba maalum ya bure 0800 750 247 inayofanya kazi saa 24 kwa siku, siku saba kwa wiki mwaka mzima.”

Aliendelea kueleza kuwa, Kituo hicho kimeboreshwa kwa kutumia mfumo wa kisasa wa IVR (Interactive Voice Response) unaomuwezesha mwananchi kupata maelekezo ya awali kwa njia ya simu, sambamba na matumizi ya WhatsApp ambayo sasa yana uwezo wa kutoa baadhi ya majibu ya awali automatiki.

“Lengo letu ni kuhakikisha mwananchi hapati shida ya kusafiri umbali mrefu kufuatilia malalamiko, maoni, pongezi au maulizo yake. Tunataka huduma ziwe rahisi kufikika kwa kila mtu,” alisema Mhe. Katemana.

Aidha, alibainisha kuwa Kituo cha Huduma kwa Mteja kiko chini ya Idara ya Ukaguzi wa Mahakama, Mrejesho kwa Umma na Maadili, ambapo kwa sasa mrejesho kutoka kwa wananchi unahusisha maeneo manne ambayo ni maulizo, maoni, pongezi na malalamiko.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania, Dkt. Evetha Mboya ambaye alikuwa Muelimishaji katika kikao hicho, alisema huduma bora huanzia mapokezi ya kwanza kabisa kwa mteja, huku akisisitiza kuwa hata namna mteja anavyopokelewa getini inaweza kujenga au kuharibu taswira ya Mahakama mbele ya wananchi.

Aliwapongeza watumishi wa Mahakama Bukoba kwa mapokezi mazuri waliyoyatoa kwao, lakini pia aliwakumbusha kuwa, bado kuna baadhi ya malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu ucheleweshaji wa huduma na namna ya mawasiliano wanayopata kutoka kwa baadhi ya watumishi.

Alisisitiza kwa kusema kuwa, “Mteja anapokuja mahakamani mara nyingi tayari ana changamoto zake. Wengine wanakuwa wamechoka, wamekasirika au wana mawazo mengi, hivyo jukumu letu ni kumtuliza na kumfanya aone kuwa amesikilizwa.”

Katika mafunzo hayo, Dkt Evetha aliwahizimiza watumishi kutumia lugha ya heshima kwa wananchi, kuwa wasikivu pamoja na kutoa maelezo kwa utulivu hata kwa wateja wanaoonekana kuwa wagumu au wenye hasira.

Pia alikumbusha umuhimu wa kuzingatia sera ya (Open Door Policy) inayosisitiza uwazi na upatikanaji wa Viongozi au Watumishi kwa wananchi pale inapowezekana, ili kuepusha hisia za kunyimwa haki au kubezwa.

Sambamba na hilo, Viongozi hao kutoka Kituo cha Huduma kwa Mteja  walionya dhidi ya vitendo vya rushwa ndogondogo vinavyoweza kujitokeza katika utoaji wa huduma, wakisema mazingira yoyote yanayoweza kumfanya mwananchi ahisi analazimika kutoa fedha ili kupata huduma hayapaswi kuvumiliwa.

Katika kuelezea vigezo vya huduma bora kwa mteja, Mkufunzi alitaja maeneo muhimu yakiwemo kujenga imani kwa wateja (assurance), kutoa huduma kwa haraka (responsiveness), muonekano mzuri wa watumishi na mazingira ya kazi (tangibility), kujali hali ya mteja (empathy), pamoja na kuhakikisha huduma zinakuwa za kuaminika wakati wote (reliability).

Mafunzo hayo pia yaligusia umuhimu wa watumishi kujiendeleza kielimu kutokana na kasi ya maendeleo ya teknolojia, ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidijitali, (biometric) na Akili Unde (Artificial Intelligence) katika taasisi mbalimbali.

“Dunia inabadilika sana, kama hatutaongeza ujuzi wetu, ipo siku mifumo itabadilika na tukajikuta tumebaki nyuma,” alieleza Dkt Evetha.

Kwa upande wake, Mhe. Hamza Marishi aliwasihi watumishi kuifahamu vizuri Taasisi yao pamoja na nyaraka muhimu za Mahakama ya Tanzania ikiwemo Mpango Mkakati wa Mahakama na Mkataba wa Huduma kwa Mteja.

Alisema nyaraka hizo zinaeleza wajibu wa watumishi kwa wananchi pamoja na haki za wateja kupata huduma bora, uwazi na ushirikishwaji.

Katika mjadala wa wazi, baadhi ya watumishi walieleza changamoto wanazokutana nazo katika kujiendeleza kielimu, hususan ucheleweshaji wa malipo ya ufadhili kwa watumishi wanaopata nafasi za masomo.

Baadhi yao waliomba Mahakama kuweka mfumo bora wa mawasiliano kati ya Mwajiri na Vyuo ili wanafunzi wanaodhaminiwa wasipate usumbufu wanapowasili vyuoni.

Mmoja wa washiriki ambaye ni Mlinzi alisema amenufaika na ufadhili wa Mwajiri kwa kupata nafasi ya kusoma katika Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) lakini akaomba nafasi zaidi za kujiendeleza zitolewe kwa Kada mbalimbali kutokana na mabadiliko ya teknolojia na mifumo ya kazi.

Kikao hicho kilihitimishwa kwa watumishi kuaswa kuendelea kulinda taswira ya Mahakama ya Tanzania kwa kutoa huduma bora, kuwa waadilifu, kutumia teknolojia vizuri na kuendelea kujifunza ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

 

Picha ya pamoja. Kuanzia Kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba, Bw. Edward Mbara, wa pili kushotp ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba, Mhe Said Mkasiwa, katikati ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzani, Mhe. Aloyce Katemana ambaye ni Mkufunzi katika kikao hicho, wa pili kulia ni Dkt. Evetha Mboya Kiongozi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja ambaye pia alikuwa Mkufunzi wa Kikao cha utoaji elimu kutoka Kituo hicho na wa kwanza kulia ni Bi. Monica  Kalokola, Ofisa Utumishi Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba wakiwa katika ufunguzi wa kikao hicho na utambulishaji wa watumishi waliohudhuria.

Dkt. Evetha Mboya (aliyesimama) akitoa elimu ya utoaji wa huduma bora kwa wateja kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Bukoba. Walioketi katikati ni Bi Monica Kalokola, Ofisa Utumishi Mahakama Kuu Bukoba na kulia Bw. Rojas Rwanyumba, Ofisa Tawala Mahakama Kuu ya Tanznaia Masjala Ndogo ya Bukoba na nyuma yao  ni baadhi ya  watumishi wa Mahakama waliohudhuria wakisikiliza na kufuatilia kwa umakini mafunzo hayo.


 Elimu ya huduma kwa wateja ikiendelea kutolewa.Walioketi ni Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba wakisikiliza kwa utulivu.
Mtumishi wa Mahakama Bukoba akiuliza swali kwa mtoa elimu ya huduma kwa mteja.

Mhe. Hamza Marishi kutoka Kituo cha Huduma kwa Mteja-Mahakama ya Tanzania akitoa elimu ya huduma kwa wateja kwa watumishi wa Mahakama Bukoba kwenye ukumbi wa Mahakama  Bukoba. Wa pili kulia ni 
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba, Mhe Janeth Massesa, wa pili kushoto ni Mhe. Andrew Kabuka, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Bukoba na wa kwanza kushoto ni Bw. Godfrey Kalugila, Dereva Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba wakifuatilia mafunzo yanayotolewa.
Picha ya pamoja, katikati ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba, Mhe. Lilian Itemba, kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya TanzaniaMasjala Ndogo ya Bukoba, Mhe. Said Mkasiwa na kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Aloyce Katemana. Waliosimama nyuma kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba, Bw. Edward Mbara, kushoto ni Mhe Hamza Marishi kutoka Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania na katikati ni Dkt. Evetha Mboya, Kiongozi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni