Jumatano, 27 Mei 2026

MAHAKAMA KIGOMA YAWAAGA WATUMISHI WALIOHAMA KITUO, WASTAAFU NA KUWAKARIBISHA WATUMISHI WAPYA

  • Jaji Mfawidhi awapongeza waliohama kwa kazi nzuri na kuwataka wakachape kazi Vituo walivyohamishiwa

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile amewaongoza watumishi na wadau wa Mahakama katika hafla ya kuwaaga watumishi waliohamishwa kutoka Mahakama hiyo.

Hafla ya kuwaaga watumishi hao ilifanyika tarehe 23 Mei, 2026 katika viwanja vya Mahakama Kuu Kigoma.

Mhe. Rwizile amewapongeza Jaji Projestus Kahyoza na Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Singida, Bw. Filbert Matotay kwa uchapakazi wao ulioacha alama kubwa walipokuwa katika Kituo cha Kigoma, alisema kuwa, Viongozi hao ni taa popote walipo maana wanayo maono na ari kubwa ya kutenda kazi kwa ubunifu na weledi mkubwa.

Jaji Rwizilea, alitumia nafasi hiyo kuwapongeza pia jumla ya watumishi sit awa Mahakama hiyo waliostaafu wa utumishi wa Mahakama kwa mujibu wa sheria ambao nao wameagwa katika sherehe hiyo.

“Tunawapongeza sana kufikia umri wa kustaafu utumishi wenu hakika Mahakama Kigoma itauenzi na kuukumbuka utumishi wenu uliotukuka wa kujitoa kwa nguvu zenu, weledi na kujituma mlipokuwa mkitimiza majukumu yenu na hatimaye kustaafu mkiwa na afya njema, muendelee kujishughulisha na kazi zenu binafsi ili muendelee kustawi katika maisha yenu huko muendako,” alisema Mhe. Rwizile.

Ameongeza kwa kuwakaribisha, watumishi walioajiriwa hivi karibuni na kupangiwa katika Kituo cha Mahakama Kigoma.

“Karibuni sana Kigoma tunafanya tofauti, hivyo tunayo imani na matarajio makubwa kwenu mtafanya kazi nasi kwa ushirikiano kupitia maarifa yenu mbalimbali tutasonga mbele zaidi katika shughuli zetu za kila siku,” amesema Jaji Mfawidhi huyo.

Kwa upande wake Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Tabora, Mhe. Projestus Kahyoza alimshukuru Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kigoma, kwa kuwa msaada mkubwa katika kusimamia shughuli za Mahakama hiyo, ambapo amesema kupitia usimamizi wake mzuri ulimfanya kazi zake kuwa rahisi na kujisikia kwamba Kigoma kuwa kituo pekee ambacho amewahi kuhudumu chenye upekee.

Hata hivyo, aliwashukuru watumishi wa Mahakama hiyo kwa upendo na ushirikiano wao, ingawa hana budi kwenda kutumikia kituo kingine, amewataka kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano, weledi na uwajibikaji ili Kigoma iendelee kuwa na sifa yake njema. 

Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Singida, Mhe. Filbert Matotay, aliwashukuru watumishi wote wa Mahakama Kigoma kwa ushirikiano waliompatia alipokuwa Mtendaji wa Mahakama hiyo kwa muda wa miaka miwili, ambayo amehudumu katika Kituo hicho.

Hata hivyo, amesema Kigoma ni kituo cha kwanza kuhudumu kwa nafasi ya Mtendaji hivyo, amejifunza mengi kutoka kwa Viongozi na Watumishi wote, na kuwaomba watumishi wampe ushirikiano Mtendaji mpya ya Mahakama hiyo ili aweze kutumika kuanzia pale alipoishia yeye.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali Mahakama na Serikali, watu binafsi, Mashirika, Taasisi binafsi na za Serikali, watumishi kutoka Mahakama za Wilaya sita, kadhalika kulikuwa na bendi ya muziki kwa ajili ya burudani.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ndogo Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akitoa cheti kwa mmoja kati ya watumishi wastaafu aliyekuwa akihudumu kwa cheo cha Msaidizi wa Kumbukumbu, Bw. Lucas Gervas aliyestaafu utumishi hivi karibuni, Kituo cha Mahakama ya Wilaya Kibondo.

 Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Tabora, Mhe. Projestus Kahyoza (kushoto), Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Singida, Bw. Filbert Matotay na Msaidizi wa Kumbukumbu, Bi. Christina Simoni kwa pamoja wakikata keki ikiwa ni ishara ya kuagana na Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (wa pili kushoto), Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Tabora, Mhe. Projestus Kahyoza (wa pili kulia), Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Singida, Bw. Filbert Matotay (wa kwanza kulia) na Mke wa Jaji Rwizile kwa pamoja wakifurahia jambo wakati wa hafla hiyo iliyofanyika tarehe 23 Mei, 2026.

 Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusufu Kasuka (kushoto) pamoja na Mahakimu wapya wa Mahakama za Mwanzo wakikata keki ikiwa ni ishara ya ukaribisho katika Mahakama hiyo.

Wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA), Tawi la Kigoma wakimuaga mwenzao Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Projestus Kahyoza nakumtakia kila la kheri katika kituo chake kipya.


Sehemu ya Watumishi na Wadau wa Mahakama waliojitokeza katika hafla ya kuwaaga watumishi na kuwakaribisha watumishi wapya na kuwapongeza watumishi waliostaafu utumishi.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma) 

 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni