- Ni wakati akiwaapisha Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani
- Awataka Majaji hao kufanya kazi kwa uadilifu, weledi, busara na hofu ya Mungu
- Awataka Majaji hao pia kulinda heshima na uhuru wa Mahakama
Na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa, kwa kutambua
umuhimu wa suala la utoaji haki nchini, Serikali imeendelea na itaendelea
kuchukua hatua stahiki za kuimarisha uwezo wa Mahakama ya Tanzania ili iweze
kusimamia vizuri eneo hilo kwa ufanisi.
Rais Samia ameyasema hayo
leo tarehe 26 Mei, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam katika Hafla ya Uapisho wa
Majaji wapya tisa wa Mahakama ya Rufani aliowateua tarehe 20 Mei mwaka huu.
“Kwa muktadha huo, uteuzi
wa Majaji wa Mahakama ya Rufani ni sehemu ya jitihada hizo za kuongeza ufanisi
katika Mhimili huu muhimu. Tumefanya mengine mengi na ninyi ni mashahidi kwamba
Mahakama zimebadilika kwa kiasi kikubwa, zimeendelea kwa kiasi kikubwa sana
katika miaka hii ya karibuni, kwahiyo sasa ni kuongeza watu wenye dhamira ya
kufanya kazi, wenye uwezo wa kufanya kazi lakini wanaosimama kwenye mstari
mzuri wa haki,” amesema Mhe. Dkt. Samia.
Rais Samia amesema kuwa,
Mahakama ya Rufani ndio ngazi ya juu ya utoaji haki nchini Tanzania, kwahiyo
kila uamuzi unaotolewa na Majaji katika Mahakama hiyo una uzito mkubwa si kwa
wahusika wa shauri pekee bali pia kwa Taasisi, mwenendo wa jamii na tafsiri
pana ya sheria nchini, yote yanawaangalia wao kama Wasimamizi wa Haki nchini.
“Hivyo basi nendeni
mkalinde heshima na uhuru wa Mahakama lakini pia muendelee kuimarisha
uwajibikaji, nidhamu na maadili ndani ya Mhimili huu muhimu, uhuru huu una
umuhimu pale unapoenda sambamba na uadilifu, ufanisi na utendaji wenu
unaoangalia uzalendo kwa nchi yenu, mnapotoa maamuzi Taifa kwanza, Nchi kwanza
halafu ndio mtaenda kwenye mambo mengine,” ameeleza Mhe. Dkt. Samia.
Akizungumza na Majaji hao
mara baada ya kuwaapisha, Mhe. Dkt. Samia amewapongeza Majaji hao kwa kuaminiwa
na kuteuliwa kushika wadhifa huo na kuwasisitiza kufanya kazi kwa uadilifu,
weledi, busara na hofu ya Mungu kama viapo vyao vinavyowataka.
“Vilevile niwapongeze
Majaji wote mlioapa leo, dhamana mliyopewa ni kubwa na ya heshima kwa Taifa
letu katika kuwatumikia wananchi, hongereni sana. Uteuzi wenu unatokana na
uzoefu, weledi na utumishi mliuonesha katika kutumikia nafasi zenu mbalimbali
mlizotumikia, nazikumbuka sura nyingine hapa nilishaziapisha nadhani leo mara
ya pili kama sio ya tatu, ina maana kipindi nilichokuwepo mimi ulishapanda,
ukapanda, umepanda katika ngazi hii ya leo...” amesema Rais Samia.
Amesema pia, uteuzi wa
Majaji hao ni ishara kwamba wamefanya kazi nzuri na Tume ya Utumishi wa
Mahakama imetambua kazi yao na imewapendekeza kupandishwa katika ngazi hiyo,
kwahiyo ana imani kwamba kwa heshima hiyo waliopewa Majaji hao, watafanya kazi
wa bidii zaidi.
“Nendeni mkaongeze nguvu
katika Mahakama ya Rufani, kwa kutambua umuhimu wa haki kama msingi wa amani,
utulivu lakini pia maendeleo ya Taifa letu na ustawi wa wananchi kwa ujumla,
haki ndio inashinda katika yote haya,” amesisitiza Mhe. Dkt. Samia.
Kadhalika, Rais Samia
amewataka Majaji hao kuitumikia Nchi kwa uadilifu, weledi na uzalendo kama
walivyoapa, huku akisisitiza kwa kusema kuwa, “mmeapa mtafanya kazi bila
upendeleo, huba, chuki. Sasa bila upendeleo, bila upendeleo kwa sababu kazi
yenu ina Kanuni zake, sasa kuna hili suala la huba na chuki, hicho ndio
ninataka mkajitazame vizuri ndani yenu katika kutoa maamuzi ya hukumu zenu.”
Mkuu huo wa Nchi
ameongeza kuwa, dhamana waliyopewa Majaji hao sio ya cheo tu bali pia ni wajibu
wa kulinda haki za Watanzania katika maamuzi yote wanayofanya wakumbuke kuwa
kwa kuwatumikia Wanadamu ni kumtumikia Mungu.
“Nimeshawaambia mara
kadhaa kwamba kwa hapa duniani, ukiacha Mungu anayesimamia haki za wote,
wengine ambao Mungu amewateua kusimamia haki za wenzenu ni ninyi Majaji, katika
ngazi zenu tofauti tofauti. Kwahiyo mnafanya kazi kubwa na mna dhima kubwa kwa
Nchi hii katika kutenda haki, kuhakikisha haki za wananchi zinapatikana lakini
si tu za wananchi hata haki ya kusimamia Taifa lenu iko mikononi mwenu, kwahiyo
wale wenzetu wanasema ‘the service to humanity is serving to God’ mnapohudumia
wananchi kusimamia haki mnatumikia kazi ya Mungu pia,” amesisitiza Rais Samia.
Majaji walioapishwa ni
Mhe. Imani Daudi Aboud, Mhe. Rabia Hussein Mohamed, Mhe. Dkt. Yose Joseph
Mlyambina, Mhe. Immaculata Kajetan Banzi, Mhe. Cyprian Phocas Mkeha, Mhe.
Yohane Bokobora Masara, Mhe. Dkt. Juliana Laurent Masabo, Mhe. Abdi Shaaban
Kagomba na Mhe. Ibrahim Mzee Ibrahim.
Kwa mujibu wa taarifa ya
Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Herbert, baada ya uapisho
wa Majaji hao tisa (9), idadi ya Majaji wa Rufani imeongezeka kutoka 37 hadi 46 sawa na majopo 15.
Viongozi mbalimbali wamehudhuria katika hafla ya uapisho ambao ni pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju, baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdallah, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera (Mb), Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe. Daniel Sillo (MB), Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila na wengine.
Mhe. Rabia Hussein Mohamed akiapa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo tarehe 26 Mei, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (kushoto) akimuapisha Mhe. Immaculata Kajetan Banzi kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo tarehe 26 Mei, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (kushoto) akimuapisha Mhe.Cyprian Phocas Mkeha kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo tarehe 26 Mei, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mhe. Yohane Bokobora Masara akiapa mbele ya Rais Samia (hayupo katika picha) kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo tarehe 26 Mei, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mhe. Dkt. Juliana Laurent Masabo akiapa mbele ya Rais Samia (hayupo katika picha) kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo tarehe 26 Mei, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisaini hati ya kiapo cha Jaji Kagomba baada ya kumuapisha yeye pamoja na wenzake nane kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo tarehe 26 Mei, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mhe. Ibrahim Mzee Ibhrahim akiapa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania mbele ya Rais Samia (hayupo katika picha) leo tarehe 26 Mei, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi (wa kwanza kushoto), Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (wa pili kushoto), Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdallah (wa pili kulia) na Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe. Daniel Sillo (wa kwanza kulia) wakiwa katika Hafla ya Uapisho wa Majaji wapya tisa wa Mahakama ya Rufani leo tarehe 26 Mei, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Majaji na Watanzania kwa ujumla mara baada ya kuwaapisha Majaji wapya tisa wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo tarehe 26 Mei, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Viongozi mbalimbali wa Mahakama waliohudhuria hafla ya Uapisho wa Majaji wapya tisa wa Mahakama ya Rufani leo tarehe 26 Mei, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam. Aliyeketi kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Amidi wa Mahakama hiyo, Mhe. Augustine Mwarija, katikati ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani.































Hakuna maoni:
Chapisha Maoni