Jumatatu, 22 Juni 2026

FROF. OLE GABRIEL AKABIDHI RASMI OFISI KWA MTENDAJI MKUU MPYA WA MAHAKAMA

Na. JAMES BUSANYA & INNOCENT KANSHA - Mahakama

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mstaafu Prof. Elisante Ole Gabriel leo tarehe 22 Juni, 2026 amefanya makabidhiano rasmi ya Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, kwa Mtendaji Mkuu Mpya Dkt. John Antony Jingu.

Akizungumza katika hafla hiyo ya makabidhiano ya Ofisi yaliyofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Prof Ole Gabriel alisema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha kufikia siku hiyo muhimu ya kukabidhi ofisi baada ya kuitumikia Mahakama kwa miaka mitano kama Mtendaji Mkuu. Alieleza kuwa anathamini fursa aliyopewa ya kutoa maneno machache kabla ya kukabidhi rasmi majukumu hayo kwa mrithi wake.

Prof. Ole Gabriel aliongeza kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. Alisema kuwa katika kipindi chote cha utumishi wake katika nafasi hiyo, Serikali alimpa ushirikiano na msaada mkubwa uliowezesha utekelezaji wa majukumu mbalimbali na kufanikisha mageuzi mengi ndani ya Mahakama.

Aidha, alimshukuru Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, pamoja na viongozi wote wa Menejimenti ya Mahakama kwa ushirikiano mkubwa waliompatia katika kipindi chote cha utendaji wake. Pia aliwashukuru aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Emmanuel Tutuba, na Katibu Mkuu wa sasa, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba, kwa ushirikiano wao mkubwa katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Mahakama.

Akizungumzia safari yake ya utumishi wa umma, Prof. Ole Gabriel alisema alianza kazi tarehe 1 Julai, 1991, na kwamba hadi anastaafu anahitimisha safari ya miaka 35 ya kulitumikia taifa. Aliwashukuru waajiri wake wote aliowahi kufanya nao kazi tangu alipoanza utumishi akiwa kijana wa miaka 20.

Vilevile, Prof Ole Gabriel aliwapongeza viongozi mbalimbali waliomlea na kumjengea uwezo wa kiutendaji, akiwemo Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma na Jaji Kiongozi wa wakati huo, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, ambao walimfundisha mambo mengi kuhusu uongozi na utendaji ndani ya mhimili wa Mahakama. Hakuwasahau wazazi wake pamoja na familia yake, hususan mke wake Devotha na watoto wake, kwa msaada na uvumilivu waliompatia katika safari yake ya kazi.

Aidha, Prof. Ole Gabriel alisema kuwa, kustaafu ni jambo jema, lakini kustaafu kwa heshima ni jambo lenye thamani zaidi. Alisema hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati wa kumuapisha Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama Dkt. John Anthony Jingu ilikuwa zawadi kubwa kwake kuliko hata fedha, unaposifiwa na kuagwa vizuri, kuna faraja na manufaa makubwa sana ndani yake kwa kuwa ilionesha kuthamini mchango wake katika utumishi wa umma kitu ambacho kilimpa faraja na heshima kubwa.

Katika hotuba yake, alimpongeza Dkt. Anthony Jingu kwa kuteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu Mpya wa Mahakama ya Tanzania na kuelezea kuwa, uteuzi huo umetokana na uwezo, uzoefu na utumishi wake wa muda mrefu katika nafasi mbalimbali za uongozi. Alieleza kuwa Mahakama imepata kiongozi mwenye uwezo wa kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kuimarisha zaidi utendaji wa Taasisi.

“Mheshimiwa Rais ametuletea mtu ambaye ana uelewa mpana na maarifa ya kiuongozi. Hawa viongozi waliopo mbele yako hapa leo, pamoja na watumishi wengine wote wanaofuatilia hafla hii kwa njia ya mtandao, ndiyo Timu ya Ushindi timu nzuri sana na mahiri ambayo nimekuwa nikiitumia kwa saa 24 kukamilisha majukumu ya mhimili huu. Timu iliyopo ndani ya Mahakama ni timu imara na yenye uwezo mkubwa, ambayo imekuwa msingi wa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi changu cha uongozi. Aliwahimiza viongozi na watumishi wote wa Mahakama kuendelea kumpa ushirikiano Mtendaji Mkuu huyo Mpya kama mlivyonipa mimi,” alisisitiza Prof. Ole Gabriel.

Akieleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wake Prof Ole Gabriel, alisema Mahakama imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za haki. Miongoni mwa mafanikio hayo ni kuanzishwa kwa huduma za Mahakama Inayotembea, kuimarishwa kwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kuboreshwa kwa mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu, kuongezeka kwa kasi ya usikilizaji wa mashauri, pamoja na kuimarishwa kwa uwezo wa ukaguzi wa Mahakama na pia kusimamia miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu na kuboresha taratibu za utendaji kazi, mafunzo na nidhamu kwa watumishi.

Vilevile, Prof. Ole Gabriel alisisitiza umuhimu wa kuendelea kudumisha umoja na mshikamano kati ya Maafisa Mahakama na wasio Maafisa Mahakama. Pia alieleza umuhimu wa ushirikiano kati ya mihimili mitatu ya dola, akibainisha kuwa ushirikiano kati ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Katibu wa Bunge na Katibu Mkuu Kiongozi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na ufanisi wa Taasisi za umma.

Akizungumzia mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Prof. Ole Gabriel alisema Mahakama imepata ongezeko kubwa la bajeti ya maendeleo na matumizi ya kawaida, alieleza kuwa, rasilimali watu zimeongezeka kutoka watumishi 5,725 hadi zaidi ya watumishi 7,000. Mahakimu 377 wameongezeka, Majaji wa Mahakama Kuu wameongezeka kutoka 70 hadi 137, huku Majaji wa Mahakama ya Rufani wakiongezeka kutoka 16 hadi 46.

Kwa upande wa miundombinu, Prof. Ole Gabriel alisema, Mahakama imepata maendeleo makubwa katika ujenzi wa majengo na makazi ya Majaji. Alibainisha kuwa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania lililopo jijini Dodoma ni miongoni mwa majengo makubwa zaidi ya Mahakama duniani likiwa linashika nafasi ya sita na la kwanza barani Afrika.

Miundombinu hiyo, inajumuisha vituo Jumuishi vya utoaji haki sita vimejengwa katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Morogoro, Mwanza, Dodoma na Arusha. Aliongeza kuwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo umewezesha kuokoa zaidi ya shilingi bilioni tatu za Serikali.

Vilevile, Prof. Ole Gabriel amesema kuwa, kwa upande wa maslahi ya watumishi posho mbalimbali za watumishi zimeongezwa wakiwemo madereva na waendesha ofisi zimeongezwa na kuendelea kulipwa kwa wakati bila kuchelewa. Alitoa pongezi kwa Mkurugenzi wa Mipango na Ufuatiliaji waliohusika katika kuhakikisha stahili za watumishi wa kada zote zinashughulikiwa kwa wakati.

Aliwataka watumishi wote wa Mahakama kuendelea kuzingatia nidhamu, uwajibikaji na maadili ya kazi yaliyokuwa msingi wa mafanikio ya Taasisi hiyo. Pia alimkumbusha Mtendaji Mkuu wa Mahakama Mpya Dkt. Jingu umuhimu wa kuendelea kuwajali na kuwasaidia Majaji wastaafu wanapohitaji msaada.

Aidha, Prof. Ole Gabriel alimhakikishia Dkt. Anthony Jingu kuwa ataendelea kumpa ushirikiano na ushauri pale utakapohitajika kwa maslahi ya Mahakama na Taifa kwa ujumla. Alimtakia Mtendaji Mkuu mpya utekelezaji mwema wa majukumu yake na mafanikio katika kusimamia mipango ya kimkakati ya Mahakama.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mstaafu Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa nasaa zake wakati wa hotuba yake ya makabidhiano ya Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania leo tarehe 22 Juni, 2026 jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu Mpya wa Mahakama ya Tanzania Dkt. John Antony Jingu (katikati) akikabidhiwa nyezo na vitendea kazi vitakavyo mwongoza katika majukumu yake na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mstaafu Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) huku zoezi hilo likishudiwa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya (kushoto) mara baada ya makabidhiano rasmi ya Ofisi leo tarehe 22 Juni, 2026 jijini Dododma. 

Mtendaji Mkuu Mpya wa Mahakama ya Tanzania Dkt. John Antony Jingu (katikati) na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya (kushoto) wakimkabidhi Ua maalum lililoandaliwa kama zawadi kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mstaafu Prof. Elisante Ole Gabriel mara baada ya makabidhiano rasmi ya Ofisi leo tarehe 22 Juni, 2026 jijini Dododma. 

Meza Kuu ikiongozwa na Mtendaji Mkuu Mpya wa Mahakama ya Tanzania Dkt. John Antony Jingu (katikati) wakiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya wajumbe wa menejimenti ya Mahakama na sehemu ya watumishi wa Mahakama Makao Makuu.
Mtendaji Mkuu Mpya wa Mahakama ya Tanzania Dkt. John Antony Jingu (katikati) akitia saini Kitabu cha wageni alipowasili ofisini kwake mara baada ya makabidhiano rasmi ya Ofis leo tarehe 22 Juni, 2026 jijini Dododma, wengine ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mstaafu Prof. Elisante Ole Gabriel (akulia) na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mstaafu Prof. Elisante Ole Gabriel (akushoto) akipeana mikono kama ishara ya kuagana na Mtendaji Mkuu Mpya wa Mahakama ya Tanzania Dkt. John Antony Jingu leo tarehe 22 Juni, 2026 walipokuwa wakifanya makabidhiano rasmi ya Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania. 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mstaafu Prof. Elisante Ole Gabriel (akulia) akipeana mikono na Mtendaji Mkuu Mpya wa Mahakama ya Tanzania Dkt. John Antony Jingu leo tarehe 22 Juni, 2026 walipokuwa wakifanya makabidhiano rasmi ya Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania. 

(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni