Na. HALIMA MNETE – Mahakama
●
Apongeza mchango wa Prof. Ole Gabriel, asema ueledi, uadilifu
na uwajibikaji vitakuwa msingi wa uongozi wake.
Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John
Anthony Jingu, ameahidi kuendeleza na kuimarisha mafanikio yaliyofikiwa na
Mahakama ya Tanzania kwa kusimamia misingi ya weledi, uwajibikaji na uadilifu
katika utekelezaji wa majukumu ya Taasisi.
Dkt. Jingu ametoa kauli hiyo leo tarehe 22 Juni, 2026 katika
hafla ya kumpokea kumkaribisha na kumkabidhi rasmi Ofisi ya Mtendaji Mkuu, iliyofanyika
katika Ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, ambapo pia
alitoa salamu za shukrani kwa Mtendaji Mkuu anayestaafu, Prof. Elisante Ole Gabriel,
kwa mchango wake mkubwa katika mageuzi na maendeleo ya Mahakama.
Aidha, Dkt. Jingu, ambaye aliapishwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 19 Juni 2026 jijini
Dar es Salaam, alisema uteuzi wake ni heshima kubwa pamoja na dhamana nzito
inayohitaji ushirikiano wa pamoja ili kuhakikisha Mahakama inaendelea
kutekeleza wajibu wake wa kikatiba kwa ufanisi.
“Nitumie fursa hii kumshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa imani aliyonionesha ya kuniteua kushika nafasi hii. Ninaamini
kwa kushirikiana na watumishi wote wa Mahakama tutaendelea kuisaidia taasisi
hii kutekeleza majukumu yake kwa kiwango kinachotarajiwa na wananchi,” alisema
Dkt. Jingu.
Alisisitiza kuwa mafanikio ya Mahakama yanategemea
mshikamano wa watumishi wake pamoja na kujengwa kwa utamaduni wa kazi
unaozingatia maadili ya utumishi wa umma.
“Kwa kushirikiana kwa pamoja tutafanya kazi kwa weledi,
uwajibikaji na uadilifu. Hizi ndizo nguzo zitakazoongoza utendaji wetu katika
kuhakikisha huduma za haki zinaendelea kutolewa kwa ubora na ufanisi,”
aliongeza.
Akizungumzia mchango wa mtangulizi wake, Dkt. Jingu
alimpongeza Prof. Ole Gabriel kwa uongozi wake madhubuti uliowezesha Mahakama
kufikia hatua kubwa ya maendeleo ya kiutendaji na kiutawala.
Mtendaji Mkuu huyo mpya, alisema kabla ya kuanza rasmi
majukumu yake, alifanya tathmini ya kina kuhusu utendaji wa Mahakama ya
Tanzania pamoja na kulinganisha na mifumo ya Mahakama za nchi nyingine, ambapo
alibaini kuwa Mahakama ya Tanzania imefikia kiwango cha juu cha utendaji.
“Nilipata nafasi ya kufanya tathmini kuhusu Mahakama ya
Tanzania na mifumo ya Mahakama katika nchi nyingine. Kwa hakika, Mahakama ya
Tanzania ipo katika kiwango cha juu sana cha utendaji, jambo linaloonesha kazi
kubwa iliyofanywa na uongozi uliopita,” alisema Mtendaji Mkuu Dkt. Jingu.
Aidha, Dkt. Jingu alisema, uzoefu na maarifa ya Prof. Ole Gabriel
yataendelea kuwa rasilimali muhimu kwa Mahakama hata baada ya kustaafu,
akieleza umuhimu wa kuendelea kupata ushauri wake wa mara kwa mara
unapohitajika.
“Prof. Ole Gabriel ni
hazina ya uzoefu na maarifa. Tutaendelea kuhitaji ushauri wake, nasaha zake na mchango
wake katika safari ya kuijenga Mahakama imara zaidi. Tunaamini ataendelea kuwa karibu
nasi,” aliongeza Mtendaji Mkuu.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama
akiwemo Msajili Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania Mhe. Eva Nkya, wajumbe wa
menenjimenti ya Mahakama pamoja na watumishi kutoka idara na vitengo tofauti,
waliomkaribisha Dkt. Jingu na kuonesha utayari wa kuendelea kushirikiana naye
katika kuimarisha utoaji wa huduma za haki nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni