Jumatatu, 22 Juni 2026

MAHAKAMA KATAVI WAIBUKA KIDEDEA KWENYE BONANZA LILILOANDALIWA NA NPS

Na. ALLY RAMADHANI – Mahakama, Katavi

Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) Kanda ya Magharibi inayojumuisha mikoa ya Katavi, Kigoma na Tabora tarehe 19 Juni, 2026 waliandaa bonanza la kimichezo lililojumuisha michezo mbalimbali kama vile mpira wa miguu, netiboli, kukimbiza kuku, kukimbia na gunia, kuvuta Kamba na kukuna nazi.

Kwa upande wa Mahakama kama mgeni mwalikwa kwenye bonanza hilo, waliondoka na medali za ushindi kwenye michezo ya kukimbiza kuku kwa mtumishi Bi. Jihadat Ntimba, mchezo wa kukuna nazi kwa wanaume alishinda Mhe. Mohamed Shabani, kukimbia na gunia kwa wanaume Bw. Ally Rajab, mchezo wa kuvuta kamba ushindi ukienda kwa NPS, huku mechi ya mpira wa miguu ikiisha kwa suluhu ya bila kufungana baina ya NPS na Polisi Katavi.

Kupitia bonanza hilo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Katavi, Mhe Godfrey Ntemi Isaya amempongeza Mkuu wa Mashtaka Katavi Bw. Theophil Mutakyawa Daniel kwa kuwa mwenyeji wa bonanza hilo lililoikutanisha mikoa hiyo na kupata fursa ya kujumuika pamoja na kubadilishana uzoefu.

“Leo tumepata nafasi ya kufanya mazoezi kwa pamoja ambayo yanatusaidia kuimarisha afya zetu, vilevile mabonanza kama haya yanasadia kuimarisha umoja, upendo, na mshikamano miongoni mwetu na kufanya kazi kama timu…”

… Leo tumepata nafasi ya kukutana kwa pamoja kati yetu sisi Mahakama, NPS, Polisi, TAKUKURU, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Katavi na jamii yetu ya wananchi wa mkoa wetu wa Katavi, ninachotaka kukimaanisha hapa ni kwamba utendaji kazi wetu mzuri kwa jamii yetu utasaidia kuimarisha amani na utulivu tulionao Katavi,” alisema Mhe. Isaya.

Vilevile, kupitia bonanza hilo Katibu Tawala Mkoa wa Katavi Bw. Albert Msovela kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuanzisha huduma za Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Katavi kwa kuwa hapo kabla wananchi wa Katavi walikua wakipata changamoto nyingi wanapofuata huduma hizo Mkoani Rukwa (Sumbawanga).

Aidha, ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa mikoa yote mitatu Kigoma, Tabora na Katavi kwa kitu walichokifanya kwani kinaongeza umoja, mshikamano na upendo miongoni mwao.

Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Katavi, Bw. Theophil Mutakyawa Daniel ametoa shukrani zake kwa wageni waalikwa wote huku akiishukuru sana Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kusogeza karibu zaidi huduma za Mahakama Kuu mkoani Katavi kwani imesaidia kutatua changamoto nyingi zilizokua zinawakumba hasa wananchi mkoani hapo.

Watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi wakiwa katika picha ya Pamoja na baadhi ya viongozi wa Taasisi mbalimbali mkoani Katavi walioketi kwenye viti mbele ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Katavi Mhe. Jaji Godfrey Ntemi Isaya wa pili kushoto, Katibu tawala wa Mkoa Bw. Albert Msovela (aliyekaa katikati mwenye kofia), wa kwanza kulia ni RPO Bw. Theophil Mutakyawa Daniel Mkuu wa Mashtaka Katavi, wa pili kulia ni RPO Bi. Chema, Mkuu wa Mashtaka Tabora na wa kwanza Kushoto ni RPO Bw. Magumbo Mkuu wa Mashtaka Kigoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Katavi Mhe. Godfrey Ntemi Isaya, akiongea na wananchi kwenye bonanza lililoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa Mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi lililofanyika viunga vya Shule ya Sekondari Rungwa iliyopo Mjini Mpanda Katavi.

Mshindi wa Mchezo wa Kukuna nazi kwa upande wa wanaume Mhe. Mohamed Masoud Shabani Mtumishi wa Mahakama Kuu Katavi.

Mshindi wa Mchezo wa Kukimbiza kuku kwa upande wa wanawake Bi. Jihadat Ahmed Ntimba ambaye ni mtumishi wa Mahakama Kuu Katavi.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi Bw. Albert Msovela kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, akitoa shukrani zake kwa washiriki wote wakati wa bonanza lililoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa Mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi lililofanyika viunga vya Shule ya Sekondari Rungwa iliyopo Mjini Mpanda Katavi.


Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Katavi Mhe. Silivia Lushasi, akifuatilia kwa ukaribu wakati wa bonanza lililoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa Mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi lililofanyika viunga vya Shule ya Sekondari Rungwa iliyopo Mjini Mpanda Katavi.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha-Mahakama)



 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni