Jumatatu, 22 Juni 2026

JAJI MKUU AKUTANA NA KUFANYA NA MAZUNGUMZO NA RAIS WA ZANZIBAR

·       Rais Mhe. Dkt. Mwinyi aahidi ushirikiano

·   Ampongeza Jaji Mkuu na kumtakia kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu yake

·       Apongeza pia maboresho ya Mahakama ya Tanzania

·       Asema Mahkama ya Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka Mahakama ya Tanzania

Na MARY GWERA, Mahakama-Zanzibar

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju ya leo tarehe 22 Juni, 2026 amemtembelea Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na kufanya naye mazungumzo mafupi.

Mhe. Masaju na ujumbe wake waliwasili Ikulu ya Zanzibar iliyopo Mnazi Mmoja majira ya Saa 4 Asubuhi na kupokelewa na Maafisa wa Ikulu ambao walimuongoza Jaji Mkuu kwenye ukumbi maalum ulioandaliwa kwa ajili ya mazungumzo kati ya Rais wa Zanzibar na mgeni wake Jaji Mkuu wa Tanzania.

Katika mazungumzo yao, Rais Mwinyi amempongeza Jaji Mkuu kwa kushika wadhifa huo na amemuhakikishia ushirikiano sambamba na kupongeza ushirikiano uliopo baina ya Mahkama ya Zanzibar na Mahakama ya Tanzania na kusisitiza umuhimu wa kuuendeleza ili kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya pamoja kwa manufaa ya wananchi.

“Nami nichukue kwanza fursa hii kukupa pongezi ya kuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hongera sana na tunataka kukuhakikishia ushirikiano wetu, bahati nzuri tayari tuna ushirikiano mzuri sana kati ya Majaji Wakuu wa pande mbili na Watendaji wa Mahakama vilevile wana ushirikiano mzuri tu, na mimi nimepata fursa mara kadhaa kukutana nao na nashukuru na ninafurahi kusema kwamba kuna mambo mengi ambayo tunapata msaada kutoka Mahakama ya Jamhuri,” amesema Mhe. Dkt. Mwinyi.

Rais Mwinyi amesema, Mahkama ya Zanzibar imekuwa ikipata msaada kutoka Mahakama ya Tanzania katika maeneo mengi ikiwemo matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utendaji wa Mahakama na kwamba ni eneo muhimu linalopaswa kupewa kipaumbele ili kuharakisha upatikanaji haki na kuongeza ufanisi.

“Eneo la TEHAMA ni eneo ambalo watu wetu huku wamekuwa wakijifunza sana upande wa pili na hatua mliyopiga wanataka na wenyewe waweze kufikia na wanapata ushirikiano wa kutosha,” amesema Mhe. Dkt. Mwinyi.

Amesema Mahkama ya Zanzibar ina fursa ya kujifunza kutokana na mafanikio yaliyofikiwa na Mahakama ya Tanzania katika matumizi ya TEHAMA, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kupunguza gharama za kiutendaji.

Aidha, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mkazo katika matumizi ya TEHAMA na uimarishaji wa miundombinu ya Mahakama katika ngazi zote, ili wananchi wapate huduma za haki kwa wakati, katika mazingira bora na karibu na maeneo wanayoishi.

Akizungumzia ujenzi wa miundombinu ya Mahakama, Rais Dkt. Mwinyi amesema ujenzi wa jengo la Mahakama ya Rufani Pemba ni hatua muhimu itakayowezesha Majaji kutekeleza majukumu yao katika mazingira bora na kuimarisha huduma za kimahakama kisiwani humo.

“Lakini vilevile, kuna eneo la Ujenzi wa Miundombinu ya Mahakama, ukiacha ile ngazi ya Rufani tayari tuna Mradi mkubwa kule Pemba, umefikia hatua nzuri na matarajio yetu muda si mrefu tuukamilishe ili tuweze kutoa nafasi nzuri ya Majaji wa Rufani wanapokuja upande wa pili basi wawe na mazingira ya kufanyia kazi yanayoendana na kazi wanazozifanya, kwahiyo nashukuru kwamba ushirikiano ni mzuri, mahusiano ni mazuri, kinachotakiwa ni kuyaendeleza,” amesisitiza. Rais Dkt. Mwinyi.

Ameongeza kwa kuishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kutambua kazi nzuri zinazofanywa na Serikali ya Zanzibar ambapo amesema, “Nashukuru kwamba angalau kuna jambo ambalo na sisi mmeona mjifunze kutoka kwetu, hii ni hatua kubwa kwetu kwa sababu sisi tumeshaweka hiyo ngazi ya rufaa ambayo ni fanisi zaidi kuliko ilivyokuwa awali.”

Kadhalika, Mhe. Dkt. Mwinyi amemshukuru Jaji Mkuu kwa kufika kujitambulisha kwake rasmi na amempongeza na kumtakia kila la kheri Jaji Mkuu wa Tanzania katika utekelezaji wa majukumu yake.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu amepongeza ushirikiano unaotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Mahakama ya Zanzibar.

“Mhe. Rais nashukuru kwa fursa hii ya kukuona, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukuwezesha kuwa, Rais wetu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, yanayofanyika huku tunayaona, mwenye macho haambiwi tazama, hongera sana,” amesema Mhe. Masaju.

Aidha, amesema uamuzi wa kujenga Mahakama ya Rufani Pemba ni wa busara na kuahidi kusimamia ujenzi huo ili ukamilike kwa wakati, kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma bora za haki na kuwapunguzia gharama za kufuatilia mashauri yao.

Aidha, Jaji Mkuu amemueleza Rais Mwinyi kuwa, amefika kumuona kwa kuwa tangu ateuliwe kuwa Jaji Mkuu alikuwa hajafika kumuona ili amfahamu na endapo ana ushauri wowote amshirikishe ili ayazingatie anapokuwa anatekeleza majukumu yake ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Nafahamu kwamba kama Jaji Mkuu pia ndio Mkuu wa Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni Mahakama ya Muungano, yanaweza kuwepo mambo mengine ambayo ungependa kunishirikisha ili ninapotekeleza majukumu yangu nitekeleze kwa namna ambayo ni ya ufanisi sana kuimarisha muungano wetu lakini zaidi pia kuharakisha maendeleo ya Zanzibar kupitia maamuzi ya Mahakama, yaani katika kutekeleza majukumu yetu tutekeleze kwa namna ambayo hasa kwa mashauri ya Zanzibar pia yanachelewa kupata uamuzi, yapate uamuzi mapema na haki ipatikane mapema ipasavyo,” amesema Mhe. Masaju.

Jaji Mkuu amemueleza Rais Mwinyi kuwa, kwa sasa kuna vikao vya Mahakama ya Rufani vinaendelea Nchi nzima ikiwemo Zanzibar, na kwamba Mahakama ya Tanzania inashukuru kwa kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa Jaji Mkuu wa Zanzibar na kumekuwa na mahusiano ya karibu.

“Tunajifunza mengi kutoka Zanzibar, wenzetu kuna maeneo mengine wamepiga hatua zaidi kuliko ilivyo kwa Bara na kwa mfano huku Zanzibar pia kuna Mahakama ya Mkoa, kule hakuna Mahakama ya Mkoa kuna Mahakama inaitwa Mahakama ya Hakimu Mkazi ina mamlaka sawa na Mahakama ya Wilaya, tunaona kwamba hiyo sio sawa, haiwezekani kwa mfano Mkuu wa Wilaya akawa na mamlaka sawa na Mkuu wa Mkoa na unakuta hawana kazi pale wanapangiwa kazi na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya, kwahiyo tunataka kurekebisha sheria,” amesema Mhe. Masaju.

Aidha, Jaji Mkuu amebainisha kwamba, Muswada umeshaandaliwa baada ya kuwa wamejifunza kutoka Zanzibar ambapo Mahakama hiyo haitaitwa tena Mahakama ya Hakimu Mkazi bali itaitwa Mahakama ya Mkoa ili pamoja na kuwa na majukumu yake ya msingi iweze pia kusikiliza rufaa zinazotoka Mahakama ya Wilaya.

Mhe. Masaju amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Mwinyi na kusema kuwa, uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa na Mahkama Kuu Pemba ni uamuzi wa Hekima na mzuri kwa sababu inawapunguzia watu umbali wa kuja kupata haki, inawapunguzia gharama, wanapata huduma katika eneo ambalo wamelizoea.

“Mhe. Rais nikuhakikishie kwamba tuko makini kuhakikisha kwamba ule Mradi unakamilika mapema ipasavyo ili Mahakama ile ianze kufanya kazi vizuri ikitumia sasa lile jengo la kisasa ambalo unaweza kuweka hata miundombinu mingine ikiwemo miundombinu ya TEHAMA. Mhe. Rais anakusudia alizindue hili jengo kwa pamoja atakapokuwa anazindua hili jengo atakuwa anatumia hiyo fursa kuzindua majengo mengine nane ambayo yamejengwa nchi nzima, kwahiyo ni Mradi mkubwa sana na hatua kubwa sana katika ushirikiano wa hizi Serikali mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,” ameeleza Jaji Mkuu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju amesema matumizi ya TEHAMA ni muhimu sana kwa kuwa tuko katika Uchumi wa Kidijitali (
Digital Economy).


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi (kulia) akimsalimia na kumkaribisha Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju alipomtembelea Ikulu Zanzibar leo tarehe 22 Juni, 2026.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi (kulia) akizungumza na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju alipomtembelea Ikulu Zanzibar leo tarehe 22 Juni, 2026.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na   Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 22 Juni, 2026 alipomtembelea Rais Mhe. Dkt. Mwinyi Ikulu ya Zanzibar.

 Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akisisitiza jambo leo tarehe 22 Juni, 2026 alipokuwa akizungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi (hayupo katika picha).

Picha ya pamoja. Kulia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na kushoto ni Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Zanzibar)



 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni