Jumapili, 21 Juni 2026

WATUMISHI WA MAHAKAMA KUU DIVISHENI YA ARDHI WAPATIWA MAFUNZO

Na DHILLON UISSO-Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Dar es Salaam

Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, hivi karibuni walipatiwa mafunzo ili kuwakumbusha kuhusu mambo mbalimbali, ikiwemo maadili ya utumishi wa umma.

Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoanza tarehe 18 Juni, 2026, yalijikita pia kuwakumbusha Watumishi hao kuhusu uwekezaj, afya ya kansa ya mlango wa kizazi, uelewa wa mifuko ya jamii na bima ya afya.

Akifungua mafunzo hayo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Elinaza Luvanda, aliwashukuru walioandaa mafunzo hayo na kusema mafunzo hayo ni muhimu kwa Watumishi.

Mhe. Luvanda alisema kuwa fursa hiyo siyo tu kufundishana, bali pia ni jambo la kukumbushana kwakuwa mambo hayo yana zungumzwa mara kwa mara. Pia alizishukuru Taasisi zilizofadhili na kutoa mada  katika mafunzo hayo.

Maada ya maadili ilwasilishwa na Jaji wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Dkt. Eliamani Laltaika, ambapo alisisitiza umuhimu wa maadili kwa Watumishi wa Umma katika kutenda haki kwa Wadau na Wadaawa wa Mahakama kwa ujumla.

Katika kuelezea suala la maadili, Watumishi walipata fursa ya kujifunza maana ya maadili, matawi na umuhimu wa maadili katika utumishi wa umma. Mhe. Dkt. Laltaika pia alifundisha mambo muhimu ya kuzingatia ili kutokuvunja maadili kwa Watumishi wa umma kwa maongezi, vitendo, mavazi na utendaji wa kazi kwa ujumla.

Katika mafunzo hayo, Watumishi pia walipata mafunzo juu ya umuhimu wa kupima afya zao mara kwa mara, hususani kupima saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake.

Mafunzo hayo pia yalihusisha maafisa kutoka UTT, PSSSF na NHIF, ambao kwa ujumla wao walielezea muhimu wa uwekezaji, fao la uzeeni na bima ya afya kwa Watumishi.

Mafunzo hayo yalihitimishwa na Kaimu Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Mohamed Gwae, ambaye aliwashukuru waandaaji kwa kufanikisha mafunzo hayo.

Alieleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwakuwa yanajenga mahusiano bora katika kazi. Mhe. Gwae aliwataka Watumishi kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kama walivyo fundishwa.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Elinaza Luvanda, (wa pili kushoto), wengine ni Majaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Thedora Mwenegoha, Mhe. Dkt. Eliamani Laltaika na Mhe. Monica Otaru.

 

Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Dkt. Eliamani Laltaika, akiwasilisha mada kuhusu maadili kwa utumishi wa umma.

 Watumishi wa Mahakama (juu na chini) wakiwa kwenye mafunzo hayo.

 

Picha za pamoja baada ya kuhitimishwa mafunzo hayo. Katikati waliokaa ni Kaimu Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Mohamed Gwae.

 Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Songea.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni