Jumatatu, 22 Juni 2026

JAJI KIONGOZI ATEMBELEA MAHAKAMA YA WILAYA NYASA, GEREZA LA MBINGA

  • Azungumza na Watumishi
  • Afurahishwa na nidhamu ya Wafungwa, Mahabusu

Na FAUSTINE KAPAMA na Noel Daud-Mahakama, Songea

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, leo tarehe 22 Juni, 2026, ametembelea Mahakama ya Wilaya Nyasa na Gereza la Wilaya ya Mbinga, na kuzungumza na Watumishi, Mahabusu na Wafungwa.

Akiwa katika Mahakama ya Wilaya, Mhe. Dkt.  Siyani amepokea taarifa ya utendaji wa Mahakama hiyo, iliyowasilishwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Osmund Ngatunga.

Kabla ya kuzungumza na Watumishi, Jaji Kiongozi alipokea pia changamoto zao na kuzitolea ufafanuzi na majawabu, ikiwepo upatikanani wa miundombinu ya majengo ya Mahakama ya Wilaya na Mahakama za Mwanzo.

Akizungumza na Watumishi hao, Mhe. Dkt. Siyani aliwakumbusha kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii na uaminifu Kadiri inavyowezekana na kuzingatia maadili, huku matendo yao yakiakisi salamu ya Mahakama kuhusu uadilifu, weledi na uwajibikaji.

“Katika zama zetu hizi, kufanya kazi kwa haki ni njia mojawapo ya kulinda miundo mbinu yetu. Watu wasiporidhika na hukumu zenu, ndiyo matukio ya ajabu ajabu wakati mwingine yanatokea,” Jaji Kiongozi amesema.

Mhe. Dkt. Siyani amewataka pia Watumishi hao kutoa huduma kwa Wananchi kwa ufanisi zaidi ili kuongeza imani kwa Mahakama na kushughulikia kero zao zinazoletwa mahakamani mapema ipasavyo, kwani Mahakama ina mchango katika kutunza amani na usalama nchini.

“Hakuna sababu kwa Wananchi kuwa na wasiwasi na Mahakama yetu. Shughulikieni kero za Wananchi. Wananchi wanaleta kero mahakamani kwa njia nyingi, wengine kwa Mkuu wa Wilaya. Mtu ana dai nakala ya hukumu, mtu ana mirathi yake anazungushwa. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kusaidia Mtanzania,” amesema.

Katika taarifa yake, Mhe. Ngatunga alieleza kuwa hapakuwepo na mashauri yaliyobaki kwa mwaka 2025, yaliyofunguliwa Januari hadi Juni, 2026 yalikuwa 208 na mashauri ambayo yamesikilizwa na kumalizika ni 200, yanayoendelea n inane.

Akizungumzia mashauri ya mirathi, ameeleza kuwa kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Juni, 2026, Mahakama za Mwanzo zimefungua, kusikiliza na kufunga mashauri 11, huku katika Mahakama ya Wilaya yamefunguliwa mashauri ya mirathi 11, yamesikilizwa tisa na mashauri mawili bado kusikilizwa.

“Mashauri yote hayajafungwa kwa sababu muda wake wa kufunga bado. Ili kuhakikisha wasimamizi wa mirathi wanatekeleza wajibu wao kwa kufuata sheria, baada ya kuteuliwa kwao, tunawapangia kila mwisho wa mwezi wafike mahakamani kuelekeza namna wanavyoedelea na ukusanyaji na kugawa mali za marahemu,” amesema.

Akiwa kwenye Gereza la Wilaya, Jaji Kiongozi alipokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa Gereza, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Afande Benjamin Masika, ambaye alionesha hali ya Gereza, idadi ya Mahabusu na Wafungwa.

Afande Masika pia alimwelezea Mhe. Dkt.  Siyani miradi mbalimbali inayotekelezwa na Gereza hilo, ikiwemo ufugaji wa samaki na ujenzi wa zahanati.

Baada ya kupokea taarifa hiyo, Jaji Kiongozi amewapongeza Mahakama katika Wilaya ya Mbinga na Nyasa pamoja na upande wa Mashataka kwa kazi nzuri ya kutekeleza sheria, ikiwemo kutozalisha Mahabusu wanaotoka Mahakama za Mwanzo.

Mhe. Dkt. Siyani pia amepongeza ubunifu unaofanywa na Gereza hilo katika maeneo mbalimbali na kushauri kuruhusu ushirikiano na Wadau, jambo litakalosaidia kuchochea maendeleo na kuondoa changamoto zilizopo.

Baada ya mazungumzo hayo, Jaji Kiongozi alikagua miradi hiyo na mazingira ya Gereza na baadaye kuzungumza na Mahabusu na Magereza na kisha kupokea changamoto zao na kuzitolea ufafanuzi na ufumbuzi.

Mhe. Dkt. Siyani ameonesha kufurahishwa na ukweli na nidhamu ya hali ya juu iliyooneshwa na vijana hao wakati wa mazungumzo hayo.

Jaji Kiongozi ataendelea na ziara yake ya kimahakama mkoani Ruvuma kwa kutembelea Magereza mawili ya Mkwaya na Kitai, yote yakiwa katika Wilaya ya Mbinga.

Katika ziara hiyo, Jaji Kiongozi ameambatana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Songea, Mhe. James Karayemaha, Jaji wa Mahakama Kuu Songea, Mhe. Emmanuel Kawishe, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa na Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu Songea, Mhe. Elizabeth Nyembele na Mhe. Asha Waziri.

Wengine ni Mtendaji wa Mahakama Songea, Bw. Allan Mwela, Mahakimu Wakazi Wfawidhi wa Mahakama za Wilaya ya Nyasa na Mbinga Songea na Watumishi wengine wa Mahakama Songea.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, akisalimiana na mmoja wa Watumishi alipowasili kwenye Mahakama ya Wilaya Nyasa mkoani Ruvuma.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, akisaini kitabu cha wageni kwenye ofisi ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Nyasa.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Songea, Mhe. Elizabeth Nyembele (aliyesimama) akitoa utambulisho wa wageni mbalimbali walioambatana na Jaji Kiongozi. Aliyekaa ni Mtendaji wa Mahakama Songea, Bw. Allan Mwela.

Sehemu ya ujumbe ulioomgozana na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, ukiwa kwenye kikao na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Nyasa.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama Wilaya ya Nyasa (juu na chini) wakiwa kwenye kikao hicho.


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, aizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Nyasa (hawapo kwenye picha).

Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (katikati). Wengine kutoka kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Songea, Mhe. Dkt. Emanuel Kawishe, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Songea, Mhe. James Karayemaha, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Nyasa, Mhe. Osmund Ngatunga na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, akisalimiana na mmoja wa Maafisa Magereza baada ya kuwasili kwenye Gereza la Wilaya ya Mbinga.


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, akiwa kwenye picha ya pamoja baada ya ukaguzi wa Gereza la Wilaya ya Mbinga.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni