· Rais Mhe.
Dkt. Mwinyi aahidi ushirikiano
·
Ampongeza Jaji Mkuu na kumtakia kila la kheri katika utekelezaji
wa majukumu yake
·
Apongeza pia maboresho ya Mahakama ya Tanzania
· Asema
Mahkama ya Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka Mahakama ya Tanzania
Na MARY GWERA, Mahakama-Zanzibar
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
George Masaju leo tarehe 22 Juni, 2026 amemtembelea Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na kufanya naye
mazungumzo mafupi.
Katika mazungumzo yao, Rais Mwinyi amempongeza Jaji
Mkuu kwa kushika wadhifa huo na kupongeza ushirikiano uliopo baina ya Mahkama
ya Zanzibar na Mahakama ya Tanzania na kusisitiza juu ya umuhimu wa kuuendeleza ili
kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Mahakama kwa manufaa ya wananchi.
“Nami nichukue kwanza fursa hii kukupa pongezi ya
kuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hongera sana na tunataka
kukuhakikishia ushirikiano wetu, bahati nzuri tayari tuna ushirikiano mzuri
sana kati ya Majaji Wakuu wa pande mbili na Watendaji wa Mahakama vilevile wana
ushirikiano mzuri tu, na mimi nimepata fursa mara kadhaa kukutana nao na
nashukuru na ninafurahi kusema kwamba kuna mambo mengi ambayo tunapata msaada
kutoka Mahakama ya Jamhuri,” amesema Mhe. Dkt. Mwinyi.
Amesema kuwa, anatarajia kuona ushirikiano
uliokuwepo ukiendelea ili kupiga hatua zaidi, na kueleza kuwa, “Sisi huku
tumepiga hatua zaidi, sisi huku tumeingia katika maboresho ya miundombinu ya
Mahakama, tunajenga Mahakama ngazi zote. Sasa hivi kwakweli mazingira yamekuwa
mazuri zaidi kuliko miaka ya nyuma, sasa hivi mwelekeo ni kwenda zaidi katika
eneo la TEHAMA, tuna imani kama wakilimudu eneo hilo maana yake mashauri
yatashughulikiwa na wale wananchi ambao hawana uwezo wanaweza kupata haki kwa
haraka zaidi,” amesema.
Rais Mhe. Dkt. Mwinyi amesema, Mahkama ya Zanzibar imekuwa
ikipata msaada kutoka Mahakama ya Tanzania katika maeneo mengi ikiwemo matumizi
ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utendaji wa Mahakama na
kwamba ni eneo muhimu linalopaswa kupewa kipaumbele ili kuharakisha upatikanaji
haki na kuongeza ufanisi.
“Eneo la TEHAMA ni eneo ambalo watu wetu huku
wamekuwa wakijifunza sana upande wa pili na hatua mliyopiga wanataka na wenyewe
waweze kufikia na wanapata ushirikiano wa kutosha,” amesema Mhe. Dkt. Mwinyi.
Amesema Mahkama ya Zanzibar ina fursa ya kujifunza
kutokana na mafanikio yaliyofikiwa na Mahakama ya Tanzania katika matumizi ya
TEHAMA, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kupunguza
gharama za kiutendaji.
Aidha, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imeweka mkazo katika matumizi ya TEHAMA na uimarishaji wa miundombinu ya
Mahakama katika ngazi zote, ili wananchi wapate huduma za haki kwa wakati,
katika mazingira bora na karibu na maeneo wanayoishi.
Akizungumzia ujenzi wa miundombinu ya Mahakama,
Rais Mhe. Dkt. Mwinyi amesema ujenzi wa jengo la Mahakama Kuu Pemba ni
hatua muhimu itakayowezesha Majaji kutekeleza majukumu yao katika mazingira
bora na kuimarisha huduma za kimahakama kisiwani humo.
“Lakini vilevile, kuna eneo la Ujenzi wa
Miundombinu ya Mahakama, tuna Mradi mkubwa wa Mahakama Kuu kule Pemba, umefikia
hatua nzuri na matarajio yetu muda si mrefu tuukamilishe ili tuweze kutoa
nafasi nzuri ya Majaji wa Rufani wanapokuja upande wa pili basi wawe na
mazingira ya kufanyia kazi yanayoendana na kazi wanazozifanya, kwahiyo
nashukuru kwamba ushirikiano ni mzuri, mahusiano ni mazuri, kinachotakiwa ni
kuyaendeleza,” amesisitiza. Rais Dkt. Mwinyi.
Ameongeza kwa kuishukuru Mahakama ya Tanzania kwa
kutambua kazi nzuri zinazofanywa na Serikali ya Zanzibar ambapo amesema,
“Nashukuru kwamba angalau kuna jambo ambalo na sisi mmeona mjifunze kutoka
kwetu, hii ni hatua kubwa kwetu kwa sababu sisi tumeshaweka hiyo ngazi ya rufaa
ambayo ni fanisi zaidi kuliko ilivyokuwa awali.”
Kadhalika, Mhe. Dkt. Mwinyi amemshukuru Jaji Mkuu
kwa kufika kujitambulisha kwake rasmi na amempongeza na kumtakia kila la kheri
Jaji Mkuu wa Tanzania katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu amepongeza ushirikiano
unaotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Mahkama ya Zanzibar.
“Mhe. Rais nashukuru kwa fursa hii ya kukuona,
nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukuwezesha kuwa, Rais wetu wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, yanayofanyika huku
tunayaona, mwenye macho haambiwi tazama, hongera sana,” amesema Mhe. Masaju.
Aidha, Jaji Mkuu amemueleza Rais Mwinyi kuwa,
amefika kumuona kwa kuwa tangu ateuliwe kuwa Jaji Mkuu alikuwa hajafika kumuona
ili amfahamu na endapo ana ushauri wowote amshirikishe ili ayazingatie
anapokuwa anatekeleza majukumu yake ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
“Nafahamu kwamba kama Jaji Mkuu pia ndio Mkuu wa
Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni Mahakama ya
Muungano, yanaweza kuwepo mambo mengine ambayo ungependa kunishirikisha ili
ninapotekeleza majukumu yangu nitekeleze kwa namna ambayo ni ya ufanisi sana
kuimarisha muungano wetu lakini zaidi pia kuharakisha maendeleo ya Zanzibar
kupitia maamuzi ya Mahakama, yaani katika kutekeleza majukumu yetu tutekeleze
kwa namna ambayo hasa kwa mashauri ya Zanzibar pia yanachelewa kupata uamuzi,
yapate uamuzi mapema na haki ipatikane mapema ipasavyo,” amesema Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu amemueleza Rais Mwinyi kuwa, kwa sasa
kuna vikao vya Mahakama ya Rufani vinaendelea Nchi nzima ikiwemo Zanzibar, na
kwamba Mahakama ya Tanzania inashukuru kwa kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa
Jaji Mkuu wa Zanzibar na kumekuwa na mahusiano ya karibu.
“Tunajifunza mengi kutoka Zanzibar, wenzetu kuna
maeneo mengine wamepiga hatua zaidi kuliko ilivyo kwa Bara na kwa mfano huku
Zanzibar pia kuna Mahakama ya Mkoa, kule hakuna Mahakama ya Mkoa kuna Mahakama
inaitwa Mahakama ya Hakimu Mkazi ina mamlaka sawa na Mahakama ya Wilaya,
tunaona kwamba hiyo sio sawa, haiwezekani kwa mfano Mkuu wa Wilaya akawa na
mamlaka sawa na Mkuu wa Mkoa na unakuta hawana kazi pale wanapangiwa kazi na
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya, kwahiyo tunataka kurekebisha sheria,” amesema
Mhe. Masaju.
Aidha, Jaji Mkuu amebainisha kwamba, Muswada
umeshaandaliwa baada ya kuwa wamejifunza kutoka Zanzibar ambapo Mahakama hiyo
haitaitwa tena Mahakama ya Hakimu Mkazi bali itaitwa Mahakama ya Mkoa ili
pamoja na kuwa na majukumu yake ya msingi iweze pia kusikiliza rufaa zinazotoka
Mahakama ya Wilaya.
Mhe. Masaju amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Mwinyi na
kusema kuwa, uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa na Mahkama Kuu Pemba
ni uamuzi wa Hekima na mzuri kwa sababu inawapunguzia watu umbali wa kuja
kupata haki, inawapunguzia gharama, wanapata huduma katika eneo ambalo
wamelizoea.
Mbali na hilo, Jaji Mkuu amesema uamuzi wa ujenzi
wa Mahakama hiyo ni mzuri kwa kuwa pia eneo ambalo haki inapopatikana linapaswa
lipendeze, ili mtu anapofika awe na matumaini.
Katika upande mwingine, Jaji Mkuu amezungumzia
kuhusu Uchumi wa Kidijitali (Digital Economy), ambapo amebainisha kuwa, upande
wa Zanzibar wao ni wepesi kuweka katika utekelezaji mambo mazuri na kuyaweka
katika matumizi mapema.
Ameeleza kuwa, kwa sasa wao wana Kanuni za Ushahidi
wa Kieletroniki ambazo zinatumika hata katika Mahakama za ngazi za chini.
“Sasa hivi miamala mingi ya fedha inafanyika
kielektroniki, na kwa Zanzibar hata Ushahidi wa Kielektroniki sasa unatumika
hata Mahakama za chini kabisa kwa Ushahidi ambao watu wanaandikiana kwenye simu,
kompyuta na kadhalika anaweza akautoa Mahakamani,” amesema Mhe. Masaju.
Kufuatia hali hiyo, Jaji Mkuu amesema kuwa, ameamua
kuboresha Kanuni za Ushahidi za mwaka 1964 zinazotumika katika Mahakama za
Mwanzo ili kuzingatia matakwa ya (Electronic Transcation) kifungu cha 19
ambacho kinaelekeza Ushahidi huo wa kielektroniki utatumika katika Mahakama zote.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo kati yake na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju alipomtembelea Ikulu Zanzibar leo tarehe 22 Juni, 2026.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi (kulia) akimsalimia na kumkaribisha Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju alipomtembelea Ikulu Zanzibar leo tarehe 22 Juni, 2026.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali
Mwinyi akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na Jaji Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 22 Juni, 2026
alipomtembelea Rais Mhe. Dkt. Mwinyi Ikulu ya Zanzibar.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akisisitiza jambo leo tarehe 22 Juni, 2026 alipokuwa akizungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi (hayupo katika picha).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi (kulia) akimsalimia na kumkaribisha Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 22 Juni, 2026 alipomtembelea Rais Mhe. Dkt. Mwinyi Ikulu ya Zanzibar.
Picha ya pamoja. Kulia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na kushoto ni Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju.
(Picha na MARY GWERA,
Mahakama-Zanzibar)






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni