Jumanne, 23 Juni 2026

JAJI DKT. MAMBI AKABIDHI OFISI YA JAJI MFAWIDHI TABORA KWA JAJI MUGETA

  •  Uadilifu, Ushirikiano na Uwajibikaji vyasisitizwa 

Na AMANI MTINANGI, Mahakama-Tabora

Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Tabora imeandika ukurasa mpya wa historia kufuatia hafla ya makabidhiano ya Ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tabora iliyofanyika kwenye ukumbi namba 2 wa Mahakama hiyo kati ya aliyekuwa Jaji Mfawidhi, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi na mrithi wake Mhe. Ilvin Mugeta.

Hafla ya makabidhiano ilifanyika tarehe 22 Juni, 2026 na kuhudhuriwa na Majaji, Viongozi na Watumishi wa Mahakama ikibeba ujumbe mzito wa uongozi ukihusu uwajibikaji na mwendelezo wa utendaji bora katika utoaji wa haki.

Akizungumza mara baada ya kupokea ofisi, Mhe. Mugeta alisema amekuta timu imara yenye uzoefu, maadili na moyo wa kazi, jambo linalompa matumaini makubwa ya kuendelea kuimarisha utendaji wa Mahakama katika Mahakama hiyo.

“Sina hofu na timu niliyoikuta hapa. Nimekuta watumishi wenye weledi, uzoefu na moyo wa kujituma. Ninachowaomba ni kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu, nidhamu na kwa kuzingatia miongozo, sheria na taratibu za kazi. Haki inapokuwa msingi wa kazi zetu, imani ya wananchi huongezeka pale sisi watumishi wa Mahakama tunapozingatia maadili,” alisema Jaji Mugeta.

Aliongeza kuwa, maendeleo ya Taasisi yoyote hutegemea ushirikiano wa watumishi wake, huku akibainisha kuwa, mafanikio ya Mahakama si ya mtu mmoja bali ni matokeo ya juhudi za pamoja.

Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Mambi alisema anaondoka akiwa na kumbukumbu nyingi nzuri kutokana na ushirikiano alioupata kutoka kwa watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Tabora.

“Katika maeneo mbalimbali niliyowahi kufanya kazi, Tabora ni mojawapo ya timu bora kabisa kuwahi kufanya nayo kazi. Ninamkabidhi Mhe. Mugeta timu inayojituma, yenye maadili, mshikamano na utayari wa kutekeleza majukumu yake kwa weledi mkubwa. Nina imani ataipokea na kuifikisha katika viwango vikubwa zaidi vya mafanikio,” alisema Jaji Mambi.

Alitumia nafasi hiyo kuwashukuru watumishi wote kwa ushirikiano waliompatia katika kipindi chote cha uongozi wake, akisisitiza kwamba, mafanikio yoyote aliyoyapata yalitokana na kazi ya pamoja.

Naye Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Tabora, Mhe. Martha Mpaze alimkaribisha Jaji Mugeta Mahakama Kuu Tabora na kuahidi kuwa watumishi wataendelea kudumisha ushirikiano na mshikamano katika kutekeleza majukumu yao.

“Kwa niaba ya watumishi wote wa Mahakama Masjala Ndogo ya Tabora, tunakukaribisha kwa moyo mkunjufu. Tunakuahidi ushirikiano wa dhati katika kutekeleza majukumu yako. Aidha, tunamshukuru sana Jaji Mhe. Dkt. Mambi kwa mchango wake mkubwa, uongozi wake wenye hekima na mchango wake uliotukuka ambao umeacha alama chanya katika Mahakama yetu,” alisema Jaji Mpaze.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Tabora, Bw. Emmanuel Munda alimhakikishia Jaji Mfawidhi mpya kuwa watumishi wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya uadilifu, uwajibikaji na weledi wa hali ya juu.

“Tunaahidi kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma bora za Mahakama kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili,” alisema Bw. Munda.

Hafla hiyo iligubikwa na hisia za huzuni kiasi, shukrani, matumaini na ari mpya ya kazi, huku wajumbe wakisisitiza kuwa mabadiliko ya uongozi ni sehemu ya ukuaji wa Taasisi na fursa ya kuendeleza mema yaliyopo.

Kama wasemavyo wahenga, 'Kijiti kimoja hakivunji chawa,' Kauli hiyo ilidhihirika katika hafla hiyo ambapo viongozi na watumishi walionesha dhamira ya kuendelea kushirikiana kwa lengo la kuimarisha utoaji haki kwa wananchi.

Makabidhiano hayo yameacha ujumbe muhimu kwamba uongozi ni dhamana ya muda, lakini maadili mema, uadilifu na utumishi wa umma ni urithi unaodumu vizazi na vizazi.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Tabora, Mhe. Ilvin Mugeta (mwenye miwani) akisalimiana na watumishi wa Mahakama Tabora baada ya kuripoti katika kituo chake kipya cha kazi Mahakama Kuu Kanda ya Tabora. Nyuma yake ni Mhe. Dkt. Adam Mambi aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora ambaye kwa sasa amehamishiwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara.

Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Tabora, Mhe. Ilvin Mugeta akizungumza na watumishi mara baada ya kupokea ofisi. Amesisisitiza umuhimu wa uadilifu, nidhamu na kuzingatia miongozo ya kazi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Manyara, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi akitoa neno la shukrani kwa watumishi wa Mahakama Tabora kwa ushirikiano waliompatia katika kipindi chake cha uongozi.


Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Tabora, Mhe. Ilvin Mugeta (kulia) akipokea taarifa ya makabidhiano ya Ofisi kutoka kwa aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi ambaye amehamishiwa Mahakama Kuu Manyara kwa nafasi ya Jaji Mfawidhi.

 Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Tabora, Mhe. Martha Mpaze akimkaribisha rasmi Jaji Ilvin Mugeta katika familia ya Mahakama Kuu Tabora.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Tabora, Mhe. Rhoda Ngimilanga  akisherehesha shughuli ya Makabidhiano ya Ofisi ya Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Tabora.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Tabora, Bw. Emmanuel Munda akitoa ahadi ya kuendelea kutekeleza majukumu kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji chini ya uongozi mpya.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni