Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Kibaha
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Angela Bahati ameishauri Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha kutoa elimu hasa ya jinai na elimu ya mirathi ili kuzuia kufanyika kwa makosa.
Mhe. Bahati aliyasema hayo tarehe 22 Juni, 2026 alipokuwa akifanya ukaguzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha-Pwani.
Akizungumza akiwa ofisini kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha, alisema elimu zinazotolewa Mahakamani zinasaidia sana kuzuia kufanyaika kwa makosa kwakuwa wananchi wataelimishwa/watafundishwa sheria na kutambua makosa huenda wengine wanafanya makosa kwa kutojua kama ni makosa.
Jaji Bahati aliongeza kwa kusema kuwa, “tunavyozidi kutoa elimu kwa wadaawa ndio inasaidia kupunguza hata haya matukio mbalimbali.”
Lakini pia amesisistiza mkazo uwekwe kwenye Sheria za Mirathi maana ndio mashauri mengi ambayo wananchi wanakosa uelewa wakieleweshwa watafunga mashauri yao kwa wakati na kupunguza kufungua migogoro mingine kwa sababu mirathi isipofungwa hata baada ya miaka 20 atatokeza mjukuu kuanza kudai kwa sababu mirathi haijafungwa kwa hiyo amewataka kulitafakari na kufanya jitihada.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mahakama kwa kipindi cha mwezi Aprili mpaka Juni, 2026, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukumai amesema katika taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mahakama kwa Mkoa wa Pwani umezingatia Nguzo tatu za Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania yaani Utawala Bora, Uwajibikaji na Usimamizi wa Rasilimali, Utoaji Haki kwa wakati na Kuimarisha Imani ya Wananchi na Ushirikishwaji wa Wadau.
Amesema katika Utawala na Usimamizi wa shughuli za za Mahakama, Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani inasimamaia Mahakama za Wilaya saba (7) na Mahakama za Mwanzo 40.
Katika utekelezaji wa maelekezo ya Viongozi wa juu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani imejitahidi kupanga mashauri kwa kuzingatia muda kwa mujibu wa waraka Na. 4/2018 wa Jaji Mkuu na wateja wanafika kwa muda uliopangwa.
Kuhusu kasi ya uondoshaji wa Mashauri ya Mlundikano amesema inaridhisha, wananchi wanapata huduma katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kulingana na taratibu zilizopangwa na usikilizwaji wa mashauri kupitia mtandao (Video and Audio conferencing) unaendelea kufanyika kipindi cha Aprili hadi Juni na mashauri saba yamesikilizwa kwa njia hiyo ya mtandao.
Aidha, Mhe Lukumai amesema uelewa wa watumishi juu ya Mpango Mkakati na Programu ya maboresho ya Huduma za Mahakama unafanyika kupitia vikao vya kila wiki ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya kazi zinazofanyika ndani ya wiki. Na pia wanaelimisha juu ya sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Katika Nguzo ya Pili ya Mpango Mkakati huo, Mhe. Lukumai amesema kwa kuzingatia maelekezo na maagizo ya Viongozi wa juu na jitihada za kila Hakimu, mashauri yanasikilizwa na kumalizika mapema ipasavyo. Na vilevile yamekuwa yakisajiliwa kwenye mfumo na kuhuishwa kwa wakati, hiyo inawezesha taarifa za mashauri kupatikana kwa urahisi katika mfumo wa ‘e-CMS’ na ‘Data Hub’.
Katika nguzo ya tatu, Mahakama Pwani imeimarisha Imani ya Wananchi na Ushirikishwaji wa Wadau kwa kutoa elimu mbalimbali katika Mahakama kwa kipindi cha Aprili hadi Juni jumla ya mada 10 zilitolewa kwa wadau na wananchi.
Naye Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Bw. Nestory Mujunangoma amesema Mahakama Mkoa wa Pwani haina changamoto kubwa za kukwamisha utendaji wa kazi na kwamba changamoto zilizopo zinatatuliwa kwa awamu.
Akizungumzia kuhusu upungufu wa watumishi, Bw. Mujunangoma amesema nafasi zinaendelea kujazwa kadri ya ajira mpya zinazpotokea. Kwa mfano kwa kipindi cha Januari mpaka Juni wamepokea watumishi wapya takribani 27.
Aidha, Mtendaji huyo amesea, changamoto ya majengo inatokana na uchakavu wa majengo hayo kwa vile ni ya zamani na ofisi inaendelea kufanya ukarabati mdogo mdogo ili shughuli za Mahakama ziendelee kufanyika.
Lakini pia ameeleza kuwa, kwa mwaka huu wanaoumaliza kuna majengo manne mapya hivyo, anaishukuru Mahakama ya Tanzania kwa sababu inaendelea kupunguza uhaba wa majengo.
“Kwa mwaka huu wa fedha unaisha Mkoa umefanikiwa
kupata majengo mapya manne, matatu ya Mahakama za Mwanzo ambazo ni Bungu,
Kimanzichana na Msata ambazo tayari zimeshafunguliwa na Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi na moja la Mahakama ya
Wilaya Kibiti ambalo mwezi huu mwishoni linatarajiwa kufunguliwa rasmi.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ndogo ya Dar es Salaam, Mhe. Angela Bahati akipokea Taarifa ya Utekelezaji ya Mahakama ya Pwani wakati wa ziara yake ya ukaguzi.
Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani, Bw. Nestory Mujunangoma (kulia) akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa Jaji Angela Bahati (hayupo katika picha). Kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Hussein Mushi.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni