Jumanne, 23 Juni 2026

BSAAT YAIKABIDHI MAHAKAMA GARI LA KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA

Na. HALIMA MNETE & INNOCENT KANSHA - Mahakama

       Toyota Hilux mpya kuongeza ufanisi wa ufuatiliaji, tathmini na usimamizi wa shughuli za kimahakama nchini

Mahakama ya Tanzania imepokea rasmi gari jipya aina ya Toyota Hilux 2.4 GD Pick Up Double Cabin kutoka Mradi wa Building Sustainable Anti-Corruption Action Programme (BSAAT) katika hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa ufuatiliaji wa shughuli za mapambano dhidi ya rushwa na kuimarisha utoaji wa haki nchini.

Makabidhiano hayo yamefanyika tarehe 22 Juni, 2026, katika ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, yakihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama, menejimenti ya Mahakama na waratibu wa programu au mradi wa BSAAT pamoja na watumishi wa Mahakama Makao Makuu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya alisema kuwa gari hilo ni nyenzo muhimu itakayosaidia Mahakama kutekeleza kwa ufanisi shughuli za ufuatiliaji na tathmini (Monitoring and Evaluation), hususan katika maeneo ya mbali ambayo awali yalikuwa na changamoto za kufikika.

Mhe. Nkya alisema kuwa, uwezeshaji huo unaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Tanzania ya kuendelea kuimarisha mifumo ya utoaji haki kwa kuhakikisha taasisi za kisheria zinapata rasilimali muhimu za kuboresha utendaji wake.

“Kupatikana kwa gari hili kutaongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa Mahakama kufanya ziara za ufuatiliaji, usimamizi wa shughuli za mradi, uhakiki wa taarifa pamoja na tathmini ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za BSAAT katika maeneo tofauti nchini,” alisema Msajili Mkuu.

Aidha, alibainisha kuwa mchango wa BSAAT ndani ya Mahakama umeleta mageuzi makubwa katika kuimarisha uwezo wa taasisi kushughulikia mashauri ya rushwa kubwa na uhalifu wa kiuchumi kwa ufanisi zaidi.

Mhe. Nkya aliongeza kuwa, miongoni mwa mafanikio yaliyotajwa ni kuimarishwa kwa Programu ya Ulezi na Ushauri wa Kitaaluma kwa Majaji na Mahakimu (Judicial Mentorship Programme), ambayo imeongeza ubadilishanaji wa maarifa, kuimarisha maadili ya kazi na kuboresha usimamizi wa mashauri magumu ya rushwa.

Mbali na hilo, Msajili Mkuu ameeleza kuwa, mradi wa BSAAT umechangia pia kukuza matumizi ya teknolojia kupitia Mfumo wa Tafsiri na Unukuzi wa Kesi (Translation and Transcription System – TTS), ambao umeongeza usahihi wa kumbukumbu za mashauri na kuharakisha mwenendo wa usikilizwaji wa kesi.

Mhe. Nkya alisisitiza kuwa gari hilo si tu chombo cha usafiri, bali ni sehemu ya uwekezaji wa kimkakati unaolenga kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana kupitia BSAAT yanaendelea kudumu hata baada ya mradi huo kufungwa rasmi mwezi Septemba 2026.

“Zaidi ya kuwa nyenzo ya usafiri, gari hili ni uwekezaji wa kimkakati unaolenga kuhakikisha uendelevu wa mafanikio ya BSAAT ndani ya Mahakama,” ameongeza Mhe. Nkya.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa BSAAT Tanzania, Dkt. Boneventure Baya, amesema ushirikiano kati ya mradi huo na Mahakama umeendelea kuzaa matokeo chanya katika juhudi za kujenga taasisi zenye uwajibikaji, uwazi na uadilifu.

Dkt. Baya alisema ni jambo la busara kwa taasisi zinazonufaika na miradi ya maendeleo kuweka mikakati ya uendelevu na uwajibikaji, akisisitiza kuwa Mahakama imekuwa mfano bora kwa kuwa tayari imeandaa mpango mahsusi wa kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana kupitia BSAAT yanabaki kuwa sehemu ya mfumo wa kawaida wa utendaji wake.

“Itakuwa busara zaidi kwa taasisi zinazonufaika na miradi kama huu kuweka utaratibu mzuri wa sustainability na accountability. Mahakama ya Tanzania imeonesha mfano mzuri kwa kuwa tayari imeandaa mpango wa uendelevu na kuhakikisha mafanikio haya yanabaki na kuendelezwa hata baada ya mradi kufungwa,” amesema Dkt. Baya.

Aidha, ameongeza kuwa, Mahakama ya Tanzania imekuwa taasisi ya kipekee katika utekelezaji wa mradi huo, jambo lililopelekea kuwa taasisi pekee iliyoidhinishwa kunufaika na gari hilo kutokana na kiwango chake cha maandalizi, usimamizi mzuri wa rasilimali na dhamira ya kuendeleza matokeo ya mradi.

“Mahakama iko mbele, imejipanga na imeonesha utayari wa kulinda na kuendeleza mafanikio haya. Hii ndiyo sababu imekuwa taasisi pekee iliyokubalika katika mpango huu wa kupata gari,” amesema Dkt. Baya

Makabidhiano hayo yanaendelea kuthibitisha dhamira ya Mahakama ya Tanzania ya kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa haki, huku ikiendelea kujenga mifumo imara ya kupambana na rushwa na kuimarisha imani ya wananchi kwa Mhimili huo muhimu wa Dola.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya akitoa hotuba fupi ya kuushukuru mradi wa BSSAT kwa kutoa gari jipya aina ya Toyota Hilux 2.4 GD Pick Up Double Cabin kwa ajili ya kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa nchini.



Mratibu wa mradi wa BSAAT kutoka Mahakama ya Tanzania Naibu Msajili wa Mahakama Kuu mhe. Richard Kabate akieleza mchango wa BSAAT ndani ya Mahakama umeleta mageuzi makubwa katika kuimarisha uwezo wa taasisi kushughulikia mashauri ya rushwa kubwa na uhalifu wa kiuchumi kwa ufanisi zaidi.

Sehemu ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania walioshiriki zoezi la Mahakama ya Tanzania Kukabidhiwa gari jipya aina ya Toyota Hilux 2.4 GD Pick Up Double Cabin kutoka Mradi wa Building Sustainable Anti-Corruption Action Programme (BSAAT)
Sehemu ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania walioshiriki zoezi la Mahakama ya Tanzania Kukabidhiwa gari jipya aina ya Toyota Hilux 2.4 GD Pick Up Double Cabin kutoka Mradi wa Building Sustainable Anti-Corruption Action Programme (BSAAT)

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Bi. Beatrce Patrick akizungumzia mchango wa BSAAT ndani ya Mahakama wakati akitoa shukrani kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania wakati wa zoezi la kupokea gari jipya aina ya Toyota Hilux 2.4 GD Pick Up Double Cabin kutoka Mradi wa Building Sustainable Anti-Corruption Action Programme (BSAAT)
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya (aliyembele ya Gari kushoto) akikata utepe kuashiria kupokelewa kwa gari hilo huku akishuhudiwa na Sehemu ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania walioshiriki zoezi la Mahakama ya Tanzania Kukabidhiwa gari jipya aina ya Toyota Hilux 2.4 GD Pick Up Double Cabin kutoka Mradi wa Building Sustainable Anti-Corruption Action Programme (BSAAT)


Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya (aliyembele ya Gari kushoto) akipokea funguo kutoka kwa mwakilishi wa BSAAT  kuashiria kupokelewa kwa gari hilo huku akishuhudiwa na Sehemu ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania walioshiriki zoezi la Mahakama ya Tanzania Kukabidhiwa gari jipya aina ya Toyota Hilux 2.4 GD Pick Up Double Cabin kutoka Mradi wa Building Sustainable Anti-Corruption Action Programme (BSAAT)
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya (aliyembele ndani ya  Gari kushoto) akitoa ishara ya kuwasha gari hilo mara baada ya kulipokea.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya wa nane kutoka kulia na Sehemu ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania walioshiriki kwenye zoezi la Mahakama ya Tanzania kukabidhiwa gari jipya aina ya Toyota Hilux 2.4 GD Pick Up Double Cabin kutoka Mradi wa Building Sustainable Anti-Corruption Action Programme (BSAAT) wakiwa kwenye picha ya pamoja.

(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni