Na ARAPHA RUSHEKE, Mahakama Kuu Dodoma.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga, jana
tarehe 22 Juni, 2026, amefungua mafunzo yanayowakutanisha Maafisa wa Mahakama
na Ustawi wa Jamii kwa lengo la kuimarisha uwezo wa kushughulikia kesi za
unyanyasaji wa kingono na ukatili wa kijinsia kwa kuzingatia hali na mahitaji
ya manusura.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku tatu katika Ukumbi wa Mikutano uliopo Kituo Jumuishi
cha Utoaji Haki, Jaji Tiganga alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu katika
kuimarisha utoaji wa haki wenye kuzingatia utu, heshima na ustawi wa manusura
wa ukatili wa kijinsia.
Alisisitiza kuwa Watumishi
wa Mahakama na Maafisa Ustawi wa Jamii wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha
wahanga wanapata huduma za haki katika mazingira salama na yenye huruma.
Alieleza kuwa Mahakama
ya Tanzania inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha upatikanaji wa
haki kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi, ikiwa ni pamoja na
kuimarisha uwezo wa Watumishi wake kupitia mafunzo ya mara kwa mara.
Jaji Tiganga aliwataka
washiriki kutumia vyema fursa hiyo kwa kushiriki kikamilifu katika mijadala na
kubadilishana uzoefu utakaosaidia kuboresha utendaji kazi wao wa kila siku.
Aidha, aliwahimiza
kuyafikisha maarifa watakayopata kwa Watumishi wenzao katika vituo vyao vya
kazi ili kuongeza manufaa ya mafunzo hayo kwa sekta nzima ya utoaji haki.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Irish Rule of Law International (IRLI) na yanalenga kuwajengea washiriki uelewa wa mbinu zinazosaidia kuepusha kuamsha upya maumivu ya kisaikolojia kwa manusura wa ukatili wa kingono na kijinsia wanapopitia mchakato wa utoaji haki.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala
Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga akizungumza wakati akifungua mafunzo ya
ukatili wa kijinsia Dodoma.
Meza
Kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga (wa
katikati waliokaa). Kulia kwake ni Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu Njombe, Mhe Victoria Nongwa, ambaye pia ni Mkufunzi wa mafunzo
hayo. Aliyeketi kushoto kwake ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe.
Upendo Ngitiri wakiwa kwenye picha ya pamoja na Wakufunzi wa mafunzo hayo.
Meza
Kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga (wa
katikati waliokaa). Kulia kwake ni Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu Njombe, Mhe Victoria Nongwa, ambaye pia ni Mkufunzi wa mafunzo
hayo. Aliyeketi kushoto kwake ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe.
Upendo Ngitiri wakiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo.
Baadhi
ya washiriki waliohudhuria mafunzo hayo ya ukatili wa kijinsia.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni